#WC2018: Kombe la Dunia lafichua uzuri wa Russia

Muktasari:

  • Bosi huyo wa soka aliyasema hayo jana katika Ikulu ya Kremlin, walikoandaliwa hafla maalumu ya shukrani na pongezi na Rais Russia, Vladimir Putin.

Moscow, Russia. Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino, amesema fainali za Kombe la Dunia zimefichua mambo mengi mazuri ya Russia ambayo wengi walikua hawayajui.
Bosi huyo wa soka aliyasema hayo jana katika Ikulu ya Kremlin, walikoandaliwa hafla maalumu ya shukrani na pongezi na Rais Russia, Vladimir Putin.
Alisema hakika fainali hizo zimewafanya watu wengi kuiona nchi tofauti na walivyokuwa wakiisikia au kuidhani kabla ya kufika na sasa wote wamejikuta wanaipenda Russia.
Aliwafagilia wananchi wa Russia kwa ujumla wao kwa kuzifanya fainali za mwaka huu kufana na kwamba hakukua na matukio yoyote ya kihalifu wala bughudha dhidi ya wageni.
Mbali ya Putin katika hafla hiyo alikuwepo pia kiongozi wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani, ambaye nchi yake ndiye mwenyeji wa fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2022.
“Kwa hakika leo mimi nimekua mtu mwenye furaha isiyo kifani, sote tumezama katika kuipenda Russia, tumefahamu mengi ambayo hatukuyajua kabla, bila shaka miaka minne ijayo sote tutaipenda hivi na kuifurahia Qatar,” alisema Infantino.
Naye Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani, alisema kama ilivyo kwa Russia, anaamini kuwa fainali za Qatari zitafana zaidi kwani wamejifunza mengi kutoka kwa Russia, hivyo wataboresha kila upungufu waliouona.