#WC2018: Drogba aikubali VAR

Moscow, Russia. Mshambuliaji wa zamani wa timu ya Chelsea na nahodha wa Ivory Coast, Didier Drogba, ametofautina na wengi kuhusiana na teknolojia inayowasaidia waamuzi, maarufu kama VAR akisema imesaidia kutoa haki kwa washambuliaji.

Wakati makocha, wachezaji, wachambuzi na mashabiki wengi wa soka wakipinga matumizi ya VAR, Drogba alisema anaamini zimesaidia kutoa haki zilizokuwa zikiachwa na waamuzi wasaidizi hasa wanapochezewa vibaya na pia zimemaliza mzozo wa mabao.

“Mnaweza mkanifikiria nazungumza kwa kuwa nilikua mshambuliaji zamani, lakini kusema kweli kwangu VAR imesaidia, angalia penalti ngapi hazikuonekana na waamuzi wasaidizi lakini teknolojia zimeweza kutoa penalti, yapo mapungufu kwenye teknolojia hii lakini nadhani yatamalizika taratibu,” alisema.

Alisema yeye alikua kati ya watu walioamini kuwa Neymar alistahili kupewa penalti katika mechi dhidi ya Costa Rica, lakini alipotizama kwa makini marudio ya tukio hilo lilipoonyeshwa na VAR kupinga penalti iliyotolewa na mwamuzi alibadili mtazamo.

“Kweli VAR imesaidia kuleta ufumbuzi, mfano tukio la Neymar mwamuzi alimpa penalti lakini VAR ikathibitisha kuwa hakukuwa na nguvu za kutosha kumwangusha mchezaji huyo, hili kila mmoja limemridhisha,” alisema na kuongeza.

"Hakika ni maamuzi kama haya yaliyokosekana kwa muda mrefu, ilikua mwamuzi akikosea mmeumia, kuwa na VAR katika Kombe la Dunia hivi sasa umekuwa ni uvumbuzi na uboreshaji bora zaidi katika soka ya sasa, ni mabadiliko muhimu sana katika mchezo huu,”. BBC SPORT.