#WC2018: Tunisia yaanza kufungasha virago Kombe la Dunia

Ubelgiji imejihakikishia nafasi ya kutinga 16 bora baada ya kuifunga Tunisia mabao 5-2 kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Spartak jijini Moscow nchini Russia.
Mabao ya Ubelgiji yaliwekwa wavuni na Romelu Lukaku (2) na Eden Hazard (2) huku Michy Batshuayi akiweka msumari wa mwisho dakika za majeruhi.
Upande wa Tunisia waliweka wavuni mabao mawili kupitia kwa wachezaji wake Wahbi Khazri na Dylan Bronn.
Ubelgiji wamejiimarisha zaidi kileleni baada ya kufikisha pointi sita wakifuatiwa na alama 6 wakifuatiwa na England wenye pointi 3.
Matokeo hayo yanafuta ndoto za Tunisia kusonga mbele kwenye fainali hizo kutokana na kupoteza mchezo wake wa kwanza Kundi G walipotandikwa mabao 2-1 na England.
England watashuka dimbani kesho Jumapili kumenyana na Panama ambayo inaburuza mkia kwenye kundi hilo.
Mechi zingine za kundi hilo zitapigwa Juni 28, ambapo England itacheza dhidi ya Ubelgiji, huku Tunisia itakuwa na kibarua mbele ya Panama.
Tunisia inaungana na timu za Misri, Morocco ambazo  tayari zimepoteza nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya 16 bora.
Senegal na Nigeria ndiyo timu za Afrika ambazo kwa sasa zinaonekana kubebea matumaini ya Waafrika, kusonga mbele hatua ya 16 bora.