#WC2018: Kocha asema Sweden imekosa bahati

Sochi, Russia. Bao lililopatikana katika dakika za nyongeza na kuwapa ushindi mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia Ujerumani, limemuumiza kocha wa Sweden, Janne Andersson, ambaye alisema sasa anaamini bahati inahusika kwenye soka.
Andersson alisema ameumizwa sana kupoteza mchezo huo uliopigwa dimba la Sochi Olympic stadium, akisema waliwabana vizuri Ujerumani kiasi cha kuwalazimisha kubaki langoni mwao kwa kipindi kirefu kutokana na kushindwa kuipenya ngome yao.
“Nimestaajabu na kuumia sana kuupoteza mchezo huu, kwa sababu tuliwadhibiti vizuri Ujerumani,  hawakuwa na madhara kwetu, kipa wetu alikua likizo kwa kipindi kirefu hakupata kashikashi, tumepoteza mchezo dakika ya mwisho ni huzi,”alisema Kocha huyo.
Katika mchezo huo uliopigwa Sweden ndio walioanza kujipatia bao lililofungwa na Ola Toivonen, katika dakika ya 32, ambalo lilidumu hadi mapumziko.
Ujerumani waliopata tabu sana katika mchezo huo kutokana na hofu ya kupoteza mchezo na kuyaaga mashindano hayo, ilisawazisha katika dakika ya tatu ya kipindi cha pili kwa bao la Marco Reus.
Mabingwa hao watetezi waliingia katika wakati mgumu baada ya mlinzi wao Jerome Boateng kulimwa kadi nyekundu katika dakika ya 82 lakini walifanikiwa kujipatia bao la ushindi katika dakika ya tano ya muda wa nyongeza mfungaji akiwa Toni Kroos.
Kocha Andersson, alisema watapambana kusaka ushindi katika mchezo wa mwisho wa makundi watakapocheza na Mexico mchezo anaoamini utakua na upinzani mkubwa kwa kuwa kila timu itataka kushinda ili kutinga raundi ya pili.