Mexico bana, acheni tu wafurahie ushindi

UNAAMBIWA hivi, mashabiki wa Mexico wamesababisha tetemeko la ardhi huko baada ya timu yao kuichapa Ujerumani katika mchezo wao wa kwanza kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia.

Katika mechi hiyo, Mexico waliwachapa Ujerumani ambao ni mabingwa watetezi bao 1-0 na kuzua taharuki kubwa kwa wababe hao wa Ulaya kuwafanya mashabiki wao kuibua upya mjadala wa Leroy Sane, kwa nini ameachwa na kocha Joachim Low.

Lakini, kinachoelezwa, Mexico walikuwa na sababu ya kushangilia kuliko kawaida baada ya kuwa timu inayoshikilia rekodi ya kuchapwa mara nyingi kwenye historia ya fainali za Kombe la Dunia.

Kwa taarifa yako tu, Mexico ndiyo nchi iliyoonja uchungu wa kufungwa mara nyingi kwenye mechi za Kombe la Dunia baada ya kufanywa hivyo mara 25. Hivyo, walikuwa na kila sababu ya kushangilia kupita maelezo baada ya kupata ushindi, tena kwa kuichapa Ujerumani.