Bao la Senegal ni utata mtupu aisee

HAKUNA kitu kitamu kwa Senegal kwenye historia yao ya Kombe la Dunia kama vile walipowachapa waliokuwa mabingwa watetezi Ufaransa kwenye mechi ya ufunguzi mwaka 2002 kule Korea Kusini na Japan.

Miaka 16 baadaye, Simba wa Teranga, wamerudi tena kwa mwanzo mzuri katika fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea Russia.

Hilo lilitokea Moscow kwenye mechi yao dhidi ya Poland, ambayo ilikuwa na straika wake Robert Lewandowski.

Poland, ambayo imeanza kampeni yake kwenye kusaka ubingwa wa dunia ikiwa timu namba nane kwenye chati za viwango vya dunia, iliduwazwa kwa kipigo hicho kutoka kwa Senegal.

Senegal walipata bao la kuongoza kwenye dakika ya 37 tu baada ya shuti la Idrissa Gana Gueye kumbabatiza Thiago Cionek na kutinga kwenye nyavu, likiwa bao la kujifunga.

Hilo lilikuwa bao la hovyo kuruhusu kufungwa. Lakini, bao la pili la Senegal lilikuwa la hovyo zaidi kutokana na utata wake. Wakati mechi ikianza kuchanganya, Poland wakipanda mbele kwenda kusaka bao la kusawazisha, kilitokea kitu kilichowavuta nyuma na kuchapwa bao jingine.

Grzegorz Krychowiak alipiga pasi ya nyuma, ambayo ilinaswa na Mbaye Niang na kwenda kufunga. Lakini, kilichotokea ni kwamba Niang alikuwa nje ya uwanja akiomba kuingia ndani baada ya kutoka kupatiwa huduma baada ya kuumia.

Beki wa Poland, Jan Bednarek, hakuwa amemwona Niang akiingia uwanjani, hivyo aliacha mpira uliokuwa umerudishwa na Krychowiak umfikie kipa Wojciech Szczesny, lakini Niang aliuwahi mpira na kufunga.

Kinachoonekana ni kwamba Niang aliingia uwanjani na kukutana na bahati hiyo huku wapinzani wake wakiwa hawafahamu kama mchezaji huyo ameruhusiwa kurudi uwanjani.

Mabao hayo mawili yalikuwa mlima mrefu kwa Poland na hivyo kujikuta ikipoteza mechi hiyo kwa kipigo cha 2-1. Mwamuzi wa mechi alikuwa Nawaf Shukralla na mchezaji bora wwa mechi ni beki wa Senegal, Kalidou Koulibaly.