Wametupia kwenye nyavu zao bwana

SIKU ya sita kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea Russia ilishuhudia mambo mengi ya kushitua. Japan imekuwa nchi ya kwanza kutoka Asia kuifunga timu ya Amerika Kusini kwenye fainali za Kombe la Dunia baada ya kuichapa Colombia mabao 2-1.

Siku hiyo hiyo, ilishuhudia kadi nyekundu ya haraka zaidi kutolewa katika historia ya fainali za Kombe la Dunia wakati Carlos Sanchez alipotolewa dakika ya tatu tu.

Usiku kulikuwa na mechi, Russia ikiwa timu ya kwanza kutinga hatua ya 16 bora baada ya kuichapa Misri 3-1, lakini mechi hiyo ilishuhudia bao la tano la kujifunga kwenye fainali hizo tangu zilipoanza hadi kufika sasa.

Makala hii inahusu mabao matano ya kujifunga yanayoitwa Boko kwenye fainali za Kombe la Dunia hadi sasa.

5. Thiago Cionek-

Poland v Senegal

Senegal ndiyo timu pekee ya Afrika iliyoshinda mechi yake kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Hiyo ilikuwa kwenye mechi yake dhidi ya Poland katika mechi ya kwanza ya kundi lake. Hata hivyo, siku hiyo, Senegal ilikuwa na bahati baada ya Poland kujifunga kupitia kwa Thiago Cionek baada ya kubatishwa kwa shuti la Idrissa Gueye. Bao la pili pia la Simba wa Teranga lililofungwa na Niang lilikuwa na utata mkubwa, lakini yote kwa yote ni uwezo wa timu hiyo ya supastaa, Sadio Mane kukusanya pointi tatu muhimu.

4.Oghenekaro Etebo- Nigeria v Croatia

Nigeria haikucheza vizuri mechi yake ya kwanza dhidi ya Croatia. Wakali hao wanaofahamika pia kwa jina la Super Eagles, hawakuwa na madhara yoyote kwa wapinzani wao kwa dakika zote 90.

Kwenye mechi hiyo walichapwa 2-0 kutokana na kufanya makosa ambayo walishindwa kuyazuia. Luka Modric na wachezaji wenzake, walipata msaada pia kuweza kuongoza 1-0 baada ya Eteno kujifunga. Kisha Ekong akafanya makosa kwa straika Mandzukic na refa akaamuru ipigwe penalti iliyowalaza kabisa Nigeria na hivyo wanakabiliwa na mtihani mzito na lazima waifunge Iceland ili kufufua matumaini ya kusonga mbele.

3.Aziz Behich- Australia v Ufaransa

Ufaransa iliichapa Australia 2-1 katika mechi yao ya kwanza ya Kundi C. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa dunia kushuhudia VAR ikitumika kumsaidia refa kwenye fainali za Kombe la Dunia, baada ya Antoine Griezmann kufunga bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti iliyoamriwa baada ya kupitia picha za video. Lakini, Australia ikapata penalti baada ya beki wa Ufaransa, Samuel Umtiti kuunawa mpira ndani ya boksi. Baada ya hapo, shuti la Paul Pogba lilimbabatiza Aziz Behich na kwenda wavuni.

2.Ahmed Fathy-

Misri v Russia

Matumaini ya Misri yatakuwa yamekufa rasmi kama Uruguay iliichapa Saudi Arabia jana Jumatano. Hii ni kwa sababu ya kipigo kutoka kwa Russia kuifanya isiwe na pointi yoyote. Hivyo, kama Uruguay itakuwa imeshinda, basi itaungana na wenyeji kutinga kwenye raundi ya pili. Mechi ya Misri ilikuwa kali na hadi mapumziko hakukuwa na bao lolote, kabla ya Ahmed Fathy kujifunga.

Bao hilo liliruhusu mengine matatu kwa haraka, huku Misri ikipata bao moja tu lililofungwa kwa penalti na Mohamed Salah.

1.Aziz Bouhaddouz- Morocco v Iran

Bao linalouma zaidi la kujifunga kwenye fainali za huko Russia ni lile la Aziz Bouhaddouz wa Morocco.

Hii ni kwa sababu limefungwa kwenye dakika za mwisho sana za mchezo. Kila mtu alikuwa akiamini kuwa mchezo huo utaisha kwa sare tasa.

Mechi hiyo ilionekana kama inakwenda kumalizika kwa matokeo ya 0-0 na ikiwa kwenye dakika za majeruhi na hapo, Iran ikapata bao lililoipa ushindi.

Bouhaddouz alijaribu kuokoa mpira huo na matokeo hayakuwa mazuri kwa upande wake na hivyo, akajikuta anatikisa nyavu zake mwenyewe.