Mchezaji akodi ndege ili kukiona kichanga

Moscow, Russia. Mlinzi wa timu ya Taifa ya Denmark, Jonas Knudsen, aliamua kukodi ndege binafsi kutoka Moscow kurudi nyumbani kwa ajili ya kumuona mtoto wake mchanga, aliyezaliwa kabla ya muda.

Knudsen alipokea taarifa kuwa mkewe amejifungua mtoto wa kike mara baada ya kumalizika kwa mechi yao ya kwanza ya Kombe la Dunia 2018 waliyoibuka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya Peru Juni 16 mwaka huu.

Mchezaji huyo mwenye miaka 25, alistaajabu sana kusikia mkewe Trine amejifungua wakati muda wake wa kujifungua ulikua bado kwa wiki kadhaa.

“Tunafurahi kuona Knudsen akirejea kumuona mkewe nyumbani tunapenda kuona mtu anayeshulikia zaidi ubinadamu,” alisema kipa wa Denmark, Kasper Schmeichel.

Aliongeza kusema katika kikosi chao wapo wachezaji wengi wenye watoto ndio maana wanajali ubinadamu na kwamba wanajua namna ambavyo mwenzao alivyoipokea taarifa hiyo ya kupata mtoto, akisema bila shaka ilikua taarifa yenye huzuni na furaha kwa namna moja ama nyingine.

Mlinzi huyo anayeitumikia klabu ya Ipswich ya England, alirejea Russia jana tayari kwa ajili ya kuitumikia Denmark katika mchezo wa leo watakapokipiga dhidi ya Australia mjini Samara ukiwa ni mchezo wa pili wa fainali za Kombe la Dunia 2018.