Jinsi Wawa, Mkenya wanavyoipasua Yanga

ETI kuna habari gani huko Jangwani? Naam! Yanga mpya inakuja taratibu.

Ndio, achana na habari za redio mbao, mpaka sasa unaambiwa nyota watano tayari wapo hatua nzuri ya kujiunga na Yanga.

Sasa kama hujui ni kwamba mara baada ya nyota hao wapya kutua Jangwani, moja kwa moja watainga kikosi cha kwanza hivyo kuwaondoa baadhi ya wachezaji waliokuwamo katika kikosi hicho kwa msimu uliopita.

Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara hawataki kabisa kusajili mchezaji wa kukaa benchi jambo ambalo limewafanya waendeshe mambo yao kisomi na kutafuta nyota ambao wataongeza kitu klabuni hapo badala ya kuwabeba tu ilimradi.

Kwa taarifa yako tu ni kwamba mpaka sasa hakuna mchezaji aliyesaini klabuni hapo baada ya Kocha Mkuu Mwinyi Zahera kuomba awafanyie tathmini wote wanaokuja, ila habari za uhakika ni kwamba nyota watano tayari wapo hatua nzuri za kujiunga nayo.

MCHONGO ULIVYO

Kazi kubwa zaidi inafanywa katika eneo la kipa baada ya Mkameruni, Youthe Rostand kuchemka ambapo sasa Mkenya, Farouk Shakalo, ndiye amefanikiwa kwenye mazungumzo ya kutua klabuni hapo, ambapo atakuja na Kocha wa Makipa mpya, Razack Siwa, anayetokea pia Kenya.

Awali, Yanga ilizungumza kwa kifupi na kipa Mkongomani, Vumi Ley Matampi, lakini mabosi wa timu hiyo wamebadili gia angani baada ya Siwa kuwaambia Shikalo anaweza kuwa mbadala mzuri zaidi wa Rostand.

Safu ya ulinzi ya Yanga itapanguliwa na ujio wa beki Muivory Coast, Sergie Wawa, ambaye alishakubaliana kila kitu na mabosi wa timu hiyo na sasa anasubiri tu tiketi ya ndege ili aweze kutua.

Wawa alilithibitishia Mwanaspoti kwa nyakati tofauti juu ya mazungumzo yake na Yanga kuwa yamekwenda vizuri na anafurahi kuja nchini kutengeneza pacha ya uchezaji na beki kisiki, Kelvin Yondani.

Mabingwa hao mara tano wa Kombe la Kagame pia wako kwenye hatua nzuri za kumalizana na kiungo, Felly Mulumbu wa Bandari ya Kenya atakayesaidiana na Mkongomani mwenzake, Papy Tshishimbi ambaye amekuwa tegemeo klabuni hapo.

Kocha wa Yanga, Zahera bado anamtamani kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko, lakini ameomba mabosi wa timu hiyo watafute fundi mwingine wa mpira ambaye atakuwa suluhisho la muda mfupi wakati huu Kamusoko akiendelea kuimarika.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga ndiyo inatarajiwa kuwa na mabadiliko makubwa zaidi kwani straika Mzambia, Obrey Chirwa tayari ametimka klabuni hapo ambapo sasa nafasi yake itazibwa na straika Mbenini, Marcelin Koupko.

Ujio wa winga wa zamani wa timu hiyo, Mrisho Ngassa, unatarajiwa pia kuletea uelekeo mpya wa safu ya ushambuliaji ambapo ataanza kwenye kikosi cha kwanza sambamba na Yusuf Mhilu ama Raphael Daudi kulingana na uzito wa mechi husika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, ameendelea kusisitiza kuwa mambo mazuri yanakuja klabuni hapo, hivyo mashabiki wa timu hiyo wasibabaike na usajili wa mbwembwe unaofanywa na wapinzani wao.

“Tuko makini na kazi yetu. Wachezaji wapya watakuja kulingana na mapendekezo ya kocha, tunataka kuwa na timu ya ushindani zaidi,” Nyika amekuwa akisisitiza kila wakati.

CHIRWA ATIBUA

Katika hatua nyingine, straika wa Yanga, Chirwa yupo Misri akimalizia dili lake la kutua katika moja ya klabu za huko jambo ambalo Mwanaspoti liliripoti wiki moja na ushei iliyopita, huku ikilezwa dili hilo linaweza kuifanya Yanga itibue mipango yake ya usajili na kuilazimisha isajili mastraika wawili wapya.

Bosi mmoja wa Yanga ambaye yupo ndani ya kamati ya usajili, alisema kwa sasa wanabadili gia ya usajili na kwamba watalazimika kusajili mastraika wawili wa maana badala ya mmoja kama walivyokubaliana awali.

Akili hiyo inatokana na Yanga kubakiza nafasi tatu pekee katika kukamilisha idadi ya wachezaji 30 wanaohitajika kikanuni katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika huku kukikosekana fursa ya kuziba nafasi ya mchezaji anayeondoka.

Mwanaspoti linafahamu kuwa kuondoka kwa Chirwa pamoja na Donald Ngoma ambaye amehamia Azam baada ya mkataba wake kuvunjwa, kutaifanya klabu hiyo kukosa washambuliaji wawili ambao waliorodheshwa awali.

Kuziba nafasi hizo, Yanga italazimika kusajili mastraika wa kigeni wawili watakaoungana na Amissi Tambwe huku nafasi moja ikisubiri maamuzi ya Kocha Mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera katika kuamua asajili kipa, kiungo au winga.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Nyika alisema kwa kifupi kwamba wamepata taarifa kuwa Chirwa yuko Misri kupitia mitandao na kwamba wanasubiri taarifa rasmi ili kujua wanaamua kipi katika kuondoka kwake.

“Hatuna taarifa rasmi kwamba Chirwa ameondoka tunaona tu katika mitandao lakini hakuna kinachoharibika,” alisema.