#WC2018: Wazee wa makombora Russia 2018

Muktasari:

  • Croatia wenyewe walipiga mashuti saba kwenye goli la England. Hivyo ndivyo Croatia walivyojaribu ambapo kwa mechi nzima walipiga mashuti 18, ambapo 11 yalipita mbali na goli la Waingereza.

MOSCOW, RUSSIA. UNAWEZAJE kushinda kwa takwimu hizi? England kwa dakika 120 ilizocheza na Croatia kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia usiku wa juzi Jumatano kule Moscow, Russia, ilipiga mashuti mawili tu kulenga goli la wapinzani wao.

Croatia wenyewe walipiga mashuti saba kwenye goli la England. Hivyo ndivyo Croatia walivyojaribu ambapo kwa mechi nzima walipiga mashuti 18, ambapo 11 yalipita mbali na goli la Waingereza.

England wao, mashuti yao ya jumla yalikuwa 10, manane yalipita mbali na goli.

Wakati fainali hizo za Kombe la Dunia zikitarajia kufika tamati keshokutwa Jumapili kwa fainali itakayozikutanisha Ufaransa na Croatia, hii ndiyo orodha ya timu tano zilizopiga mashuti mengi kwenye fainali hizo na kuacha kumbukumbu ya kipekee kabisa.

 

5.Ufaransa - mashuti 75, mabao 11

Wakati kikosi cha Les Bleus kikifanikiwa kutinga fainali yake ya tatu kwenye Kombe la Dunia ndani ya miaka 20, kimekuwa na kikosi bora kabisa huko Russia jambo linalowafanya wapewe nafasi ya kubeba ubingwa.

Kwenye michuano hiyo kwa mechi sita ilizocheza, Ufaransa imepiga mashuti 75, huku mashuti yake 24 yakilenga goli na kuvuna mabao 11. Staa wake, Antoine Griezmann, ndiye aliyehusika kwenye mabao mengi, akifunga matatu na kuasisti mawili, huku akiwa amepiga mashuti 17, tisa yakiwa yamelenga goli.

 

4.England - mashuti 81, mabao 12

Kikosi cha Three Lions kilikuwa na matarajio makubwa ya kufika fainali na pengine kubeba ubingwa katika fainali hizi za Kombe la Dunia kabla ya ndoto zake kumalizwa na Croatia, iliyowachapa 2-1 kwenye mchezo wa nusu fainali.

Kwenye fainali hizo za Russia, England imekuwa na rekodi nzuri, ikipiga mashuti 81, huku 20 yakiwa yamelenga goli na kufunga mabao 12 katika mechi zake sita ilizocheza.

Straika wake, Harry Kane, ndiye aliyehusika kwenye mabao mengi, akifunga sita katika mashuti 11 aliyopiga, huku sita yakilenga goli.

 

3.Ubelgiji - mashuti 94, mabao 14

Kwenye fainali hizi za Kombe la Dunia, Ubelgiji ndiyo timu iliyofunga mabao mengi zaidi baada ya kufunga mara 14. Ubelgiji ikiwa na mastaa matata kabisa; Eden Hazard, Kevin De Bruyne na Romelu Lukaku, yenyewe imepiga mashuti 94, huku 36 yakiwa yamelenga goli katika mechi sita walizocheza hadi walipotolewa na Ufaransa hatua nusu fainali.

Straika wake, Lukaku, amehusika kwenye mabao matano, amefunga manne na kuasisti moja katika mashuti tisa aliyopiga huku matano yakilenga goli.

 

2.Croatia - mashuti 100, mabao 12

Mario Mandzukic, Ivan Perisic, Luka Modric na Ivan Rakitic yakitajwa hayo majina basi moja kwa moja unajua Croatia wanahusika. Kwenye fainali hizi za Kombe la Dunia, Croatia imeshatinga fainali na inasubiri kukipiga na Ufaransa keshokutwa Jumapili.

Kwenye mechi zake sita ilizocheza hadi sasa, Croatia imepiga mashuti 100, huku 26 yakiwa yamelenga goli na kuvuna mabao 12. Mastaa wake; Modric, Mandzukic na Perisic ndiyo waliohusika kwenye mabao mengi zaidi, kila mmoja akihusika mara tatu, huku Modric akiwa amepiga mashuti tisa na manne yakilenga goli.

 

1.Brazil - mashuti 103, mabao 8

Mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia, Brazil, wameondoshwa kwenye fainali za mwaka huu mapema, lakini wenyewe wakiacha rekodi ya kupiga mashuti mengi zaidi, wakifanya hivyo mara 103, huku mashuti yao 38 yakiwa yamelenga kwenye goli.

Hasara waliyoipata Brazil ni kwamba kwenye mashuti yao hayo waliyopiga 34 yaliyolenga goli kwenye mechi tano, wamevuna mabao manane tu.

Supastaa wao aliyehusika kwenye mabao mengi ni Philippe Coutinho, akihusika kwenye mabao manne, mawili ya kufunga na mawili mengine ameasisti, huku akipiga jumla ya mashuti 14, nane yakilenga golini kwa wapinzani.