#WC2018: VAR zinazingua - Kocha Hareide

Muktasari:

  • Kocha Hareide amefunguka hayo baada ya kunyang’anywa tonge mdomoni na VAR katika mchezo wa jana ambao uliisha kwa sare ya bao 1-1 na Australia.

Moscow, Russia. Kocha wa Denmark, Age Hareide, ameungana na makocha wengine pamoja na baadhi ya wachambuzi wa soka wanaoponda mfumo wa teknolojia ya video inayosaidia waamuzi maarufu kama VAR.

Kocha Hareide amefunguka hayo baada ya kunyang’anywa tonge mdomoni na VAR katika mchezo wa jana ambao uliisha kwa sare ya bao 1-1 na Australia.

Katika mchezo huo Denmark ilikua ikiongoza kwa bao 1-0 kabla ya VAR kumstua mwamuzi wa mchezo huo Antonio Mateu, kuwa mchezaji wa Denmark ameunawa mpira na hivyo ni penalti.

Mwamuzi Mateu ambaye baada ya tukio hilo aliruhusu mpira uendelee kuchezwa, alibadili maamuzi na kuizawadia Australia tuta lililozaa bao la kusawazisha na mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Maamuzi hayo kwenye mchezo huo wa kundi C uliopigwa saa 9:00 alasiri kwenye dimba la Samara Arena, uliwafanya wachambuzi wengi kujenga hoja ya kuendelea kushutumu matumizi ya VAR wakisema yanavuruga ladha ya mchezo na kuwanyima ushindi wale wanaostahili.

“Kama ukiangalia kwa makini utabaini kuwa mwamuzi Antonio Mateu, alikua karibu kabisa na tukio na aliruhusu mchezo kuendelea lakini VAR ikamfanya abadili uamuzi sidhani kama Yussuf Poulsen aliushika mpira kwa makusudi yeye aliruka juu na mpira kumgonga,” alisema.

Denmark waliouanza kampeni zao kwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Peru, watalazimika kushinda mchezo wa mwisho dhidi ya Ufaransa, au waombe Dua, Peru iichape Australia mabao mengi ili wao waungane na Ufaransa kutinga hatua ya 16 bora.