#WC2018: Suker ampigia Modric chapuo tuzo ya Ballon d'Or

Muktasari:

  • Kauli ya Davor Suker, ambaye alikiongoza kikosi cha dhahabu cha Croatia, kilichoishtua dunia, katika michuano ya kombe la Dunia mwaka 1998, iliyofanyika huko Ufaransa, imekuja wakati ambapo taifa hilo linajiandaa kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia ya soka lao.

Moscow, Russia. Wakati joto la mechi ya nusu fainali ya pili, kati ya England na Croatia, ikiendelea kupanda, Rais wa Shirikisho la Soka la Croatia, amesema kiungo na nahodha wa timu ya taifa ya Croatia, Luka Modric anastahili kubeba tuzo ya Ballon d'Or.
Kauli ya Davor Suker, ambaye alikiongoza kikosi cha dhahabu cha Croatia, kilichoishtua dunia, katika michuano ya kombe la Dunia mwaka 1998, iliyofanyika huko Ufaransa, imekuja wakati ambapo taifa hilo linajiandaa kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia ya soka lao.
Croatia ambayo imekuwa na fomu ya kutisha hasa ikichagizwa na uwepo wa Luca Modric, Mario Mandzukic na Ivan Rakitic, inakutana na wajukuu wa Malkia wa England, usiku wa leo katika mechi ya pili ya nusu fainali, itakayopigwa katika dimba la Luzhniki, kuanzia saa tatu na kama watavuka watakutana na Ufaransa iliyotangulia fainali.
Akizungumza na waandishi wa habari, Suker alisema hakuna kinachomzuia Modric kubeba tuzo, hasa ikizingatia kuwa wapinzani wakubwa ambao ni Ronaldo, Neymar, Messi, De Bryune na Hazard wameshatolewa nje ya michuano hii.