#WC2018: Neymar chini ya ulinzi

Muktasari:

  • Alisema nia yake ni kuhakikisha Neymar hapati nafasi ya kuichezesha timu jambo litakalowapa nafasi ya kupata ushindi katika mechi yao  itakayopigwa leo saa 9:00 alasiri mjini St Petersburg.

St Petersburg, Russia. Kocha wa Costa Rica, Oscar Ramirez, amesema amewaandaa wachezaji wawili kwa ajili ya kumdhibiti mshambuliaji mahiri na nahodha wa Brazil, Neymar.

Alisema nia yake ni kuhakikisha Neymar hapati nafasi ya kuichezesha timu jambo litakalowapa nafasi ya kupata ushindi katika mechi yao  itakayopigwa leo saa 9:00 alasiri mjini St Petersburg.

Kocha huyo ameelezea kuumizwa na matokeo ya kipigo cha bao 1-0 walichokipata kutoka kwa Serbia, wakati Brazil ilianza kampeni yake kwa kutoka sare ya bao 1-1 na Uswisi.

Katika mchezo uliopita wa Brazil na Uswisi, mwamuzi wa mechi hiyo alishindwa kumlinda Neymar ambaye alichezewa rafu nyingi kiasi cha kutoneshwa maumivu ya mguu yaliyomuweka nje ya uwanja kwa takriban miezi mitatu.

“Bila shaka Neymar ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa bila kumuwekea ulinzi maalum itakua ngumu kuizuia Brazil, kwa hiyo tunamuwekea ulinzi maalumu wa wachezaji wawili,” alisema.

Kocha huyo mwenye miaka 53 aliyasema hayo mapema leo wakati akitangaza kikosi chake kitakachoshuka dimbani baadaye leo.