#WC2018: Mwamuzi wa fainali Ufaransa Vs Croatia huyu hapa

Muktasari:

Katika mechi hiyo ya kibabe na kisasi, Pitana mwenye umri wa miaka 43, atasaidiwa na Hernan Maidana na Juan Belatti, mwamuzi wa mezani akiwa ni Bjorn Kuipers huku safu ya meza ya teknolojia ya video (VAR), ikiongozwa na mholanzi, Erwin Zeinstra.

Nairobi. KUELEKEA mechi ya kukata na shoka ya fainali ya Kombe la Dunia 2018, Shirikisho la soka duniani (FIFA), limemteua Muargentina Nestor Pitana kusimama kati kupuliza kipyenga, katika mechi ya fainali, itakayofanyika siku ya jumapili, Julai 15, kati ya Ufaransa na Croatia.
Katika mechi hiyo ya kibabe na kisasi, Pitana mwenye umri wa miaka 43, atasaidiwa na Hernan Maidana na Juan Belatti, mwamuzi wa mezani akiwa ni Bjorn Kuipers huku safu ya meza ya teknolojia ya video (VAR), ikiongozwa na mholanzi, Erwin Zeinstra.
Ndio, Pitana mwenye umri wa miaka 43, ndiye aliyepewa jukumu la kumaliza ubishi kati ya Ufaransa na Croatia, ambao wanakutana kwa mara nyingine kwenye michuano hii baada ya miaka 20 ya kusubiri kwani mara ya mwisho walikutana kwenye Kombe la Dunia 1998, na Ufaransa wakatamba kinoma!
Wawili hao walikutana kwenye hatua ya nusu fainali ambapo Davor Suker na wahuni wenzie walioyoka kumtandika Ujerumani 3-0, walichapika kinoma mbele ya Didier Deschamps huyu huyu na wafaransa wenzake, muuaji akiwa ni Lilian Thuram, aliyetupia mara mbili kufuta bao la kuongoza la Suker. Unakumbuka lakini?
Baada ya kusubiri kwa miaka 20, Julai 15, Suker ambaye kwa sasa ni Rais wa Soka nchini Croatia, atakuwa jukwaani akiwa na suti matata, kushuhudia vijana wake wakihenyeka katikati mwa dimba la Luzhniki, wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 81,000, wakiwa na lengo la kulipiza kisasi na kurudisha heshima.
Mbali na kisasi hicho cha watoto wa mama Kolinda Grabar-Kitarović, ulimwengu wa soka  utashuhudia dakika 90 za kazi ya Nestor Pitana ambaye ndiye aliyechezesha mechi ya ufunguzi ya michuano hii, kati ya wenyeji Russia na Saudi Arabia. Kwa kifupi alifungua mlango wa kuingilia na ndiye atakayetoa idhini ya watu kuondoka Russia.
Kama hiyo haitoshi ni kwamba, Muargentina huyu, ndiye aliyechezesha mechi ya robo fainali ya kwanza kati ya Ufaransa na Uruguay na ndiye aliyekuwa pilato katika mchezo wa hatua ya 16 bora kati ya Croatia na Denmark. Ni kwamba, Pitana ni mshikaji wa Ufaransa na Croatia. Wanajuana!
NESTOR PITANA NI NANI?
Néstor Fabián Pitana, mwenye umri wa miaka 43, alizaliwa Juni 17, mwaka 1975, huko Corpus Argentina na ni mmoja wa marefa wanaoheshimika duniani na mwalimu wa michezo ya sarakasi (Gymnastic Teacher).
Kabla ya kuamua kuwa mwamuzi wa soka, historia inaonesha kuwa, Pitana mwenye urefu wa futi sita, aliwahi kucheza soka, kabla ya kugeukia mpira wa kikapu na baadae kushika filimbi. Kingine ni kwamba mwamuzi huyu asiyependa masihara, pia ni mcheza filamu. Unashangaa?
Habari ndio hiyo. Mwaka 1997, akicheza pamoja na waigizaji mashuhuri duniani, akiwemo mkongwe Luis Brandoni, Diego Torres na mwanadada mtata Laura Novoa, Pitana alihusika katika picha la La Furia 'The Fury' ambapo alikuwa mmoja wahusika wakuu.
Mwaka 2007, aligeukia fani ya uamuzi ambapo ilimchukua miaka mitatu tu kukabidhiwa beji ya FIFA. Tangia hapo, Pitana  ametumika katika mechi nyngi za Copa Libertadores, ikiwemo mechi ya nusu fainali kati ya Gremio na Barcelona SC.
Katika fainali za Kombe la Dunia 2014, FIFA ilimteua Pitana kuwa mmoja wa waamuzi wa michuano hiyo, ikiwa ni Mara yake ya kwanza. Akachezesha mechi jumla ya mechi nne, ukiwemo mchezo wa robo fainali kati ya Ufaransa na bingwa wa mwaka huo, Ujerumani.
Mwaka huu, nyota ya mwamuzi huyu, imeendelea kuwaka baada ya kukabidhiwa majukumu mazito ya kutupatia bingwa wa Dunia, akiweka rekodi ya kuwa Muargentina wa pili kuchezesha mechi ya fainali baada ya Horacio Elizondo, aliyechezesha mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 2006, kati ya Brazil na Ujerumani.