#WC2018: Hawazungumzwi, ila balaa lao uwanjani usipime

Muktasari:

  • Ndani ya mchezo huo kuna mawili; kupendwa na mashabiki kiasi cha  kuzungumziwa sana, au kuna wale ambao hatawafanye mambo mazuri kiasi gani, hawazungumzwi.

SOKA ni mchezo wa hadharani, hakuna kificho. Kila kinachofanyika ndani ya uwanja kinaonekana bayana. Kama mchezaji fulani ni mahiri,  ataonekana tu kwa umahiri wake.

Ndani ya mchezo huo kuna mawili; kupendwa na mashabiki kiasi cha  kuzungumziwa sana, au kuna wale ambao hatawafanye mambo mazuri kiasi gani, hawazungumzwi.

Basi katika kuelekea fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza Alhamisi ijayo kule Russia, kuna mastaa watakuwapo kwenye mikiki mikiki hiyo, lakini hawazungumzwi sana licha ya kuwa mahiri kweli kweli ndani ya uwanja.

 

Roberto Firmino (Brazil)

Ukitaka kujua makali ya huyu jamaa, waulize Mohamed Salah na Jurgen Klopp huko Liverpool. Firmino ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na hakika hakuna kocha ambaye hatahitaji kuwa na huduma yake ndani ya uwanja.

Hazungumzwi sana, amewazidi hata Gabriel Jesus na Philippe Coutinho, lakini ni staa ambaye atakwenda kuwatoa kimasomaso Brazil huko Russia.

 

Sadio Mane (Senegal)

Mohamed Salah alipotua pale Anfield, basi Sadio Mane alisahaulika kabisa. Habari zake zilikuwa si nyingi licha ya kwamba ana uwezo mkubwa ndani ya uwanja na hilo alilionyesha kwa uchache tu kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid.

Mane atakuwapo kwenye fainali za Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Senegal, nenda kaone shughuli yake, utaipenda.

 

Angel di Maria (Argentina)

Amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Argentina katika kipindi cha miaka 10, lakini hazungumzwi sana tofauti na ilivyo kwa nyota kama Lionel Messi, Gonzalo Higuain na Sergio Aguero.

Di Maria hatajwi kwenye orodha ya wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Argentina, lakini ukweli kama kuna mchezaji ambaye Messi atahitaji zaidi msaada kutoka kwake, basi ni staa huyo wa PSG.

 

Douglas Costa (Brazil)

Kwenye kikosi cha Brazil wanatajwa nyota wengi akiwamo Neymar, Philippe Courinho na wengineo Fred na Willian, lakini wanamsahau mtu mmoja matata kweli kweli, Douglas Costa.

Shughuli ya winga huyo si ya kitoto. Kasi yake na uwezo wa kupiga chenga huku mpira ukionekana kutii miguu yake, vinabaki kumfanya kuwa mchezaji wa kwenda kumtazama huko Russia.

 

Corentin Tolisso (Ufaransa)

Watu wengi wanawazungumzia N'Golo Kante na Paul Pogba kwenye eneo la kiungo la kikosi cha Les Bleus huko Ufaransa na kumsahau mtu anayeitwa Corentin Tolisso.

Tolliso amekuwa na msimu mzuri kweli kweli huko Bayern Munich na ndiyo maana Didier Deschamps amemwingiza kwenye kikosi chake. Nenda kaone mambo yake huko Russia.

 

Leon Goretzka (Ujerumani)

Kuachwa kwa Leroy Sane kwenye kikosi cha Ujerumani kumeshtua wengi sana, lakini wamesahau kuwa kuna fundi mwingine anaitwa Leon Goretzka ni balaa huyo mtu.

Uzuri wa huduma ya Goretzka, ambaye msimu ujao atakuwa kwenye kikosi cha Bayern Munich, ni hodari wa kufunga akiwa umbali wowote ule wa kutoka goli la wapinzani.

 

Christian Eriksen (Denmark)

Fundi wa mpira kutoka Denmark. Kiungo matata kwenye kikosi cha Tottenham na hakika shughuli yake itakwenda kuonekana wazi huko Russia. Eriksen si mtu wa kumpa nafasi ya kupiga shuti anapokuwa mbele ya goli lako, atakuadhibu. Hazungumzwi sana, lakini nenda kamuone na pasi zake huko Russia.

 

Son Heung-min (Korea)

Dunia iko kimya na inajifanya haimfahamu wala haimuoni huyu jamaa. Son ni moja ya wachezaji wenye vipaji ambao wanategemewa kuibeba Korea Kusini na kuleta ladha katika fainali za Kombe la Dunia za huko Russia.

Son amekuwa na msimu mzuri sana huko kwenye klabu yake ya Tottenham Hotspur kwa msimu uliopita.