#WC2018:Kambi za Hispania na Ureno huko Russia, raha tupu

Muktasari:

Mambo yamenoga na sasa kila timu imeshafahamu itakwenda kujichimbia wapi kwa ajili ya kufanya mazoezi na sehemu ya shughuli nyingine wakati wa maandalizi yao ya mechi wakati watakapofika kwenye fainali hizo za Russia.

WEWE mambo iko huko unaambiwa. Ligi hazijaisha, lakini Russia imeshapanga kambi ya kila timu itakayokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika kwenye ardhi ya nchi hiyo miezi miwili ijayo.


Mambo yamenoga na sasa kila timu imeshafahamu itakwenda kujichimbia wapi kwa ajili ya kufanya mazoezi na sehemu ya shughuli nyingine wakati wa maandalizi yao ya mechi wakati watakapofika kwenye fainali hizo za Russia.


Serikali ya Russia imetangaza vituo vyote 32 ambavyo timu hizo zitafikia. Sehemu hizo zimekamilika zikiwa na vyumba vya kulala, viwanja vya mazoezi, gym, mabwawa ya kuogelea na kumbi za kufanyia mikutano. Hivyo kama wewe ni shabiki wa Ureno au Hispania na unataka kuwashuhudia mastaa wa timu hizo kabla hawajenda uwanjani, basi zifuatazo ndizo sehemu zitakapofikia:

Ureno watakuwa huko Saturn, Moscow
Kituo hicho kimejengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 11.5. Sehemu hiyo ina uwezo wa kuchukua wanamichezo 130 kwa wakati mmoja. Pia, kuna viwanja vingine viwili vya mpira kwa ajili ya kufanyia mazoezi.  
Eneo hilo pia lina hoteli yenye vyumba vizuri vya kulala, eneo la kufanyia mazoezi ya viungo (Gym), bwawa la kuogelea na ukumbi kwa ajili ya kufanyia mikutano. Miongoni mwa wachezaji nyota ambao wamewahi kufanya mazoezi na kukaa katika eneo hilo ni pamoja na Roberto Carlos, Samuel Eto'O na Lassana Diarra.

Hispania watajificha kwenye akademia ya FC Krasnodar
Timu ya taifa ya Hispania itafikia kwenye eneo la akademia ya FC Krasnodar. Eneo hili ambalo bado linaendelea kujengwa ndipo yatakuwapo makazi ya mabingwa hao wa dunia wa mwaka 2010.
Eneo hilo lina viwanja viwili vya wazi kwa ajili ya kufanyia mazoezi na viwanja vitatu vya ndani kwa ajili ya mazoezi ya kujificha. Mbali na viwanja hivyo, eneo hilo lina vyumba vizuri vya kulala pamoja na huduma zote za kibinadamu. Eneo hili linamilikiwa na timu ya FC Krasnodar na wanalitumia kwa ajili ya kulea vipaji vya mchezo wa soka nchini Russia.