Labda kocha wa Mbao ana vitu ambavyo hatuvifahamu

Muktasari:

Mara zote ambazo Yanga wamekwenda Mwanza kucheza na Mbao huwa wanaambulia kipigo bila ya shida. Simba pia wamekuwa wakipata wakati mgumu wakicheza na Mbao. Nadhani kocha wa Mbao anajua jinsi ya kucheza mechi kubwa.

SAA sita kabla ya mwaka huu haujaingia siku ya juzi Jumapili, Yanga walikuwa wakichezea kichapo cha mabao 2-0 safi kutoka kwa Mbao FC. Sikusikia malalamiko. Niko mbali, Afrika Kusini. Sikuiona mechi, lakini najishawishi kwamba kilikuwa kipigo safi kwa sababu sikusikia malalamiko.

Nadhani kocha wa Mbao, Etienne Ndayiragije ana kitu ambacho hatukifahamu. Binafsi simfahamu. Mara chache nimeongea naye katika simu. Amenikosha katika mambo mawili makubwa. Kwanza ni jinsi anavyozihenyesha timu ambazo zinatumia mabilioni ya pesa katika usajili.

Mara zote ambazo Yanga wamekwenda Mwanza kucheza na Mbao huwa wanaambulia kipigo bila ya shida. Simba pia wamekuwa wakipata wakati mgumu wakicheza na Mbao. Nadhani kocha wa Mbao anajua jinsi ya kucheza mechi kubwa.

Kwamba Mbao inashindwa kuchukua ubingwa kwa sababu haitambi kwa vibonde nadhani hii ni topiki yenye wigo mpana kwa sababu tunajua jinsi ligi yetu inavyokuwa na mambo mengi.

Lakini pia jumlisha na ukweli kwamba maandalizi ya Mbao kucheza na timu nyingine ni tofauti na maandalizi ya Mbao kucheza dhidi ya Simba, Yanga na Azam FC.

Lakini kikubwa zaidi kutoka kwa kocha wa Mbao inaonekana ana mbinu zaidi za soka kuliko suala la kutegemea uwezo wa mchezaji mmoja mmoja. Katika dirisha kubwa lililopita wachezaji wake walimegwa na klabu za Simba na Yanga. Hapo hapo, Asante Kwasi alikwenda Lipuli ya Iringa.

Hata hivyo, bado amebakiza vijana wadogo ambao wameungana tena na kucheza vema kama kawaida. Hili ni suala la kocha zaidi kuliko wachezaji. Katika klabu zetu kubwa, kuna suala la wachezaji zaidi kuliko kocha.

Mara nyingi wachezaji mahiri huwa wanawabeba makocha katika klabu zetu.

Na ndio maana ikitokea timu imeyumba kidogo basi kocha anafukuzwa, kama ilivyo kwa Joseph Omog pale Simba. Labda wanaamini kina Emmanuel Okwi, John Bocco, Shiza Kichuya na wengineo wanawapa pointi tatu zaidi kuliko ilivyo kwa kocha.

Hata hivyo, kwa jinsi ninavyoyaangalia aina ya makocha kama huyu wa Mbao ni wazi wakati mwingine hawawezi kufanya vizuri katika timu kubwa. Sababu zipo wazi, lakini sababu kubwa zaidi inaweza kuwa mazingira ya kazi yake.

Klabu za Simba na Yanga zinaweza kumuwania na kumleta jijini lakini hazitaweza kumpa uhuru wake kama anavyofanya kazi akiwa na Mbao FC.

Makocha wa aina hii wanaweza kufanya kazi zaidi na wachezaji vijana wanaotaka kutoka kimaisha kuliko wachezaji ambao wameshaweka Shilingi 50 milioni na zaidi katika akaunti zao.

Kocha wa namna hii hawezi kufanya kazi kwa kupangiwa kikosi chake, kwa kudharauliwa na wachezaji mastaa ambao wanawasikiliza zaidi matajiri waliowaleta klabuni kuliko kuwajibika kwake moja kwa moja kama nidhamu ya soka inavyohitajika ndani na nje ya uwanja.

Makocha wa klabu kubwa za hapa nchini wengi wamekubali kuishi chini ya vivuli vya mabosi wao. Nadhani ni kwa sababu ya njaa. Kuna makocha wengi duniani wasio na kazi kuliko walio na kazi, wengi wakipoteza ajira zao inawachukua muda mrefu zaidi kuzipata tena.

Si ajabu Simba na Yanga zimepoteza makocha wengi wenye uwezo kama kocha wa Mbao kwa sababu makocha hao hawakukubali tu kusimamiwa kijeuri katika kazi zao za kila siku.

Wapo makocha wengi wenye misimamo ambao walifika nchini na wakaamua kuondoka baada ya kuhisi ujinga umetawala katika utawala wa klabu zao.

Kocha wa Mbao anaonekana kuwa aina ya makocha ambao wanaweza kutusaidia katika soka la vijana. Ni wakati wa TFF au klabu zetu kubwa kumchunguza kwa makini.

Sio tu kwa sababu anazifunga timu kubwa, hapana, kwa sababu anaonekana anaweza kutengeneza kundi la wachezaji hata kama baadhi yao wakiondoka.

Makocha wa namna hii hawapo wengi sana katika dunia ambayo makocha wanapenda zaidi kutumia noti za mabosi wao kuliko kitu chochote kile.

Kama unampata kocha ambaye anaweza kupata ubora wa mchezaji bila ya kutumia pesa nyingi, basi ni jambo jema zaidi.