Yondani, Kichuya wanaonyesha udhaifu wa soka letu

Muktasari:

  • Ndege anazununua Rais Magufuli leo, zilipaswa kununuliwa miaka 20 nyuma. Hata hivyo, waliokuwepo wala hawakuhangaika.

RAIS John Magufuli anapambana kununua Bombadier kwaajili ya Shirika letu la ndege (ATCL). Inashangaza sana. Vitu vilivyotakiwa kufanywa miaka ya 1990 ndio vinafanywa leo.

Ndege anazununua Rais Magufuli leo, zilipaswa kununuliwa miaka 20 nyuma. Hata hivyo, waliokuwepo wala hawakuhangaika.

Nchi yetu imekosa watu wenye weledi. Wengi wanapenda kuendesha mambo yao kienyeji na ndio maana wanapata tabu kubwa enzi hizi za JPM. Kilio kila kona.

Uwepo wa watu wengi wanaofanya mambo kienyeji, umesababisha soka letu kuendelea kuendeshwa kienyeji tu. Mambo mengi yanayofanyika kwenye soka letu ni tofauti na wanavyofanya wenzetu katika nchi zenye maendeleo.

Tumeshindwa kulifanya soka letu kuwa biashara. Tumeshindwa kuvuta watazamaji viwanjani. Tumeshindwa kutengeneza timu imara na sasa tunafeli hata kwenye mambo ya kawaida. Ndio maana unakuta wachezaji wetu wanatumikia mikataba yao hadi dakika za mwisho. Ajabu hilo linatokea kwa wachezaji wa kawaida na hata wale muhimu. Yaani mchezaji nyota wa timu anakaa hadi dakika ya mwisho ya mkataba wake ndipo mazungumzo ya mkataba mpya yanaanza.

Inawezekanaje watu kama Kelvin Yondani na Shiza Kichuya wanaachwa mikataba yao imalizike? Kuna watu wanafanya mambo kienyeji sana katika soka letu. Maelezo ya kijinga utakayopewa mchezaji ameomba kwanza amalize msimu ndipo tuzungumze. Ujinga ulioje.

Kuna sababu nyingi ambazo zimetufikisha hapa tulipo leo. Sababu ya kwanza ni kukosa watu wanaofanya kazi zao kwa weledi. Katika nchi za wenzetu mchezaji muhimu kama Kichuya hawezi kwenda hadi mwisho wa mkataba wake.

Labda kama anataka kuondoka, vinginevyo angepewa mkataba mpya mapema. Wenzetu wanaweza hilo kwa kuwa wanakubali kuwa mchezaji husika anastahili kupewa mkataba mnono. Hapa kwetu hatutaki hilo. Bado tunataka Kichuya apewe fedha ya usajili sawa na miaka miwili nyuma wakati anajiunga na Simba. Hilo haliwezekani. Pesa aliyopewa Kichuya kwa mara ya kwanza inapaswa kuwa mara mbili ama zaidi sasa. Wenzetu wanaheshimu hilo. Pesa aliyosajiliwa Mohammed Salah na Liverpool, siyo ambayo atapewa sasa wakati anaongezewa mkataba mpya. Lazima apewe fedha nyingi zaidi. Hilo ndio soka la kisasa.

Soka la kisasa linatoa zawadi kwa wanaofanya vizuri na kuwaadhibu wanaofanya vibaya. Hawa kina Kichuya na Yondani tunapaswa kuwapongeza. Tunawapongezaje? Ni kuwapa mikataba mipya minono.

Kitu kingine cha ajabu kwenye soka letu ni timu kutokubali kufanya maboresho ya mikataba. Kwa mfano, Kichuya alisajiliwa Simba mwaka juzi, akawa analipwa Sh1.5 milioni. Pamoja na kufanya vizuri kwenye msimu wa kwanza, unaweza kukuta hakuongezewa mshahara.

Kichuya alipaswa kupewa mshahara zaidi mara tu baada ya kumalizika kwa msimu uliopita. Hilo lingewezekanaje? Ni kwa kumpa mkataba mpya. Ilifahamika wazi kuwa mkataba wake ungekwisha msimu huu. Kiwango chake kilikuwa juu hivyo alipaswa kupewa mkataba mpya. Sijui Simba inawaza nini.

Yondani naye utakuta fedha aliyokuwa akilipwa miaka mitatu nyuma ndiyo anayomlipa mpaka leo. Miaka mitatu iliyopita, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ndio alikuwa beki tegemeo zaidi klabuni hapo.

Kwa sasa upepo umebadilika. Yondani ndiye tegemeo.

Sababu nyingine ya kipuuzi ambayo imetufikisha hapa tulipo ni utamaduni mbovu wa kuuza wachezaji. Timu zetu bado hazijawa na roho nyeupe katika kuuza mastaa wake. Wachezaji wengi wakitaka kuondoka inabidi wasubiri mikataba yao imalizike. Mara nyingi zinakuja ofa na kupigwa chini. Nasikia kwa Kichuya ilikuwa hivyo hivyo. Kuna timu ya Misri ilileta ofa, kaipigwa chini. Kwa Yanga ndio kuna tatizo zaidi. Nilifarijika mwaka jana ilipokubali kumuuza Saimon Msuva kwenda Difaa El Jadida. Kipindi cha nyuma Yanga ingegoma kumuuza Msuva. Kwenye mazingira hayo kwanini asitake mkataba wake umalizike, atazame fursa na ndio asaini mkataba mpya? Iliwahi kumtokea Mrisho Ngassa. Alitakiwa na Free States ya Afrika Kusini mwaka 2014 lakini Yanga ikagoma kumuuza. Ilibidi asubiri mkataba wake umalizike ndipo aondoke. Huu ndio ujinga wa soka letu.

Mambo mengi yaliyopaswa kufanyika kwa weledi yanafanyika kipuuzi. Mabadiliko mengi yaliyopaswa kufanyika zamani, yanafanyika sasa.Inaumiza mno.