NINACHOKIAMINI: Yatosha sasa, miaka 20 ya mapambano ya Wambura TFF

Muktasari:

Ukisoma vitabu mbalimbali vitakuelekeza kufanya hivyo. Vitakutaka upambane katika maisha ya kila siku, vitakutaka usikate tamaa, vitakushawishi kupambana.

KUNA watu hawakubali kushindwa katika maisha. Iwe amekosea au hajakosea, lakini kuna watu wanajua kupambana mpaka dakika ya mwisho.

Ukisoma vitabu mbalimbali vitakuelekeza kufanya hivyo. Vitakutaka upambane katika maisha ya kila siku, vitakutaka usikate tamaa, vitakushawishi kupambana.

Lakini si watu wote wanaoweza kupambana, watu wengi katika maisha hukata tamaa mapema, ni wachache sana wanaopambana wakidai haki zao au jambo lolote wanaloliamini.

Nimewaona watu hao katika maisha ya kisiasa, kibiashara, kijamii na maeneo mengine mbalimbali. Ni wapambanaji kwa kila kitu. Hawakubali kuanguka kirahisi, na hata walipoanguka kuna waliosimama tena.

Kuna watu nisingependa kuwataja hapa, ambao wamefanikiwa katika mambo mbalimbali, lakini ukisoma historia zao walianguka na baadaye wakarudi baada ya kufanya jitihada kubwa.

Bila shaka unawaweza kuwajua makocha wa klabu mbalimbai duniani ambao walifanya vibaya katika timu zao, lakini wakafanya vizuri baada ya kupambana kwa nguvu.

Kwa ujumla katika maisha, hatupaswi kuridhika, tunapaswa kupambana kama tunataka kufanikiwa, kwa sababu maisha haya bila mapambano unaweza kujikuta hufiki popote.

Miongoni mwa watu katika soka nchini ninawajua wanafahamu kupambana ni Michael Wambura. Huyu jamaa ni mbishi, ni mpambanaji na kwake kuanguka na kuinuka ni sehemu ya maisha yake ya kila siku.

Akiwa hana umaarufu sana, alimshinda Ismail Aden Rage kuwa katibu mkuu katika Uchaguzi wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Licha ya kuwa alikuwa tayari ameingia kwenye michezo ikiwa ni pamoja na kuwa katika kamati ya marekebisho ya Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru), Wambura hakuwa anafahamika sana miongoni mwa wapenzi.

Lakini alipambana na hata kumshinda Rage, ambaye alikuwa anashikilia nafasi ya ukatibu mkuu wa TFF wakati huo chini ya uenyekiti wa Muhidin Ndolanga.

Licha ya misukosuko kadhaa aliyoipata baadaye na hata kuondolewa nafasi ya ukatibu mkuu FAT, bado Wambura aliendelea kupambana na mwenyekiti wake wake, Ndolanga.

Ilikuwa moto kwelikweli, Ndolanga na Kamati ya Utendaji walimsimamisha Wambura, baada ya siku chache Wambura naye akamsimamisha Ndolanga. Ilikuwa ni pambano la uzito wa juu.

Kutokana na vurugu hizo, Serikali iliingilia kati na baadaye Fifa ikaja, ikaundwa kamati ya muda, hatimaye, Ndolanga na Wambura wakapatana na kila mmoja akarudi kwenye nafasi yake pale FAT.

Baada ya miaka kadhaa, Wambura aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya muda ya klabu ya Simba, kabla ya jina lake kuenguliwa kwenye uchaguzi wa klabu hiyo ya Msimbazi.

Wambura alipambana na akaenda kwenye mahakama za kawaida kuzuia uchaguzi huo jambo ambalo lilimgharimu.

Klabu hiyo ilimfuta uanachama na akajikuta katika malumbano na TFF kutokana na madai ya maadili kwa makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokabidhi ofisi.

Miaka minane ya uongozi wa Leodegar Tenga, ilimtupa nje ya soka Wambura, lakini aliendelea kupambana nje ya uwanja na ndio maana haikuwa ajabu kuona akirejeshwa katika soka baada ya Jamal Malinzi kushinda urais wa shirikisho hilo mwaka 2013.

Wambura alirejea kwa nguvu zote, akarudi kwenye kamati za Simba, akashinda uenyekiti Mkoa wa Mara, kabla ya kuibuka na ushindi wa nafasi ya makamu mwenyekiti wa TFF katika uchaguzi mjini Dodoma mwaka jana.

Kabla ya mwaka moja, tayari amekumbwa na mabalaa mengine, amejikuta akifungiwa maisha kujihusisha na soka huku, akishindwa pia katika rufaa yake kwenye kamati ya rufani ya maadili.

Vita ya Wambura haikuanzia jana wala juzi, ilianza miaka 20 iliyopita, amepambana huku akianguka, akisimama, akianguka na kusimama.

Ni kama anapambana na kadamnasi mbele yake, lakini hakubali kushindwa

Najua kuwa atapambana sana katika suala hili, lakini nngependa kumshauri tu kuwa sasa imetosha.

Ni muda muafaka kwa Wambura afanye kazi nyingine, nadhani soka halimtaki, yeye analitaka.

Apumzike sasa.