Yanga imefuta aibu, ila Cecafa ijipange upya

KUNA usemi unaosema kuwa mwanadamu wa sasa hawezi kuibua kitu kipya kwani vitu vyote vilishazinduliwa tangu miaka hiyo ya nyuma.

Anachoweza kufanya mwanadamu wa sasa ni kuendeleza tu kile kilichovumbuliwa miaka ya nyuma. Ndio maana hata kwenye mawasiliano ya simu zamani ilikuwa tunatumia simu zilizokuwa zinakaa kwenye meza huku zikiwa zimeunganishwa kwa waya lakini sasa mambo yamebadilika. Lakini ni simu ileile ya mawasiliano. Ilishavumbuliwa. Ukuaji wa teknolojia umesababisha kuwepo kwa simu za mkononi ambazo zimemuwezesha mtu kuwasiliana na mwenzake bila ya kuunganiswha na waya wa simu hivyo aliyevumbua mawasilino ya simu miaka hiyo ndiye aliyefanya kazi kubwa zaidi kuliko huyu aliyeendeleza teknolojia hiyo.

Hata maendeleo ya soka ni hivyo hivyo kwani hakuna kitu kipya ambacho mtu anaweza kuja nacho leo hii ambacho hakijafanyika katika sehemu nyingine duniani.

Hivyo hata sisi ambao bado hatujafanikiwa kufikia maendeleo katika mchezo huo lakini tuna nia ya dhati, tunatakiwa kuangalia na kuiga kwa wenzetu waliofanikiwa ili kujua njia walizipitia na kuwafikisha hapo walipo.

Na hasa kuwaangalia wale ambao wanamazingira yao ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni yanashabihiana na mazingira yetu ili iwe rahisi kuiga kile walichokifanya na kuweza kufikia mafanikio waliyoyafikia.

Kwa mfano unaweza kuona nchi zilizo kusini mwa Bara la Afrika kama vile Swaziland, Zambia, Angola, Afrika Kusini zimefanikiwa kuingiza timu zao katika hatua ya makundi katika mashindano ya ngazi ya klabu bingwa barani Afrika.

Timu za Township Rollers ya Botswana, Zesco ya Zambia, Primero de Agosto ya Angola, Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini ni timu zilizo kwenye nchi wanachama wa Shirikisho la soka kwa nchi za kusini mwa Afrika la COSAFA ambazo zipo katika hatua ya makundi ya kombe hilo kwa ngazi za vilabu Barani Afrika.

Mafanikio haya ya klabu kutoka katika nchi hizo ni matokeo ya jitihada za pamoja za Shirikisho hilo la Cosafa zilizoanza miaka mitano iliyopita pale lilipoanzisha programu mbalimbali za vijana kwa nchi wanachama wake kuanzia mafunzo maalumu ya makocha wa soka la vijana hadi kufikia kuwepo kwa ligi za taifa za vijana kwenye nchi wanachama wake.

Matokeo ya jitihada hizo ndio hayo ambayo leo hii tunaona klabu kutoka katika nchi hizo ambazo zilikuwa hazifanyi vema katika mashindano haya zikifanikiwa kwa kiwango hicho.

Wakati kwa sisi wengine hasa klabu kutoka Ukanda wa Cecafa utaona kuwa, katika makundi manne (4) yaliyopangwa na CAF yenye jumla ya timu 16 zilizoingia katika hatua hiyo, kuna timu moja tu ya Kampala City Council (KCC) ambayo inatoka katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati.

Na ukiangalia katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) ambayo Yanga imeuingia katika hatua ya makundi, utaona kuwa, kuna jumla ya timu tatu tu kutoka katika ukanda wetu wa Cecafa ambazo ni Rayon Sport ya Rwanda iliyoitoa Cota do Sol ya Msumbiji, Gor Mahia ya Kenya iliyoiondoa Supersport ya Afrika Kusini.

Ni timu hizo tu kutoka ukanda wa Cecafa zinazoshiriki katika hatua hiyo ya makundi hivyo kuonesha tofauti katika ya ukanda wetu na ukanda wa Cosafa ambao huko nyuma timu za ukanda huo hazikuwa zikifanya vizuri katika mashindano haya.

Ukiangalia mafanikio hayo kwa klabu za soka kwa nchi za Kusini mwa Afrika na kisha ukaangalia njia waliyopitia na kuwafanikisha japo katika hatua hiyo waliyofikia utaona kuwa ni jitihada za pamoja ambazo zimekuwa zikisimamiwa na COCAFA.

Hakuna ubishi kwamba juhudi za COSAFA ndizo zilizosaidia kwa kiwango kikubwa kukua kwa soka katika nchi hizo kwani ingekuwa kila nchi inafanya jitihada zake binafsi kama tunavyofanya katika ukanda wetu wa Cecafa nchi na klabu hizo zisingeweza kufika hapo zilipofika.

Mafanikio waliyoyafikia Zambia katika mashindano ya Vijana kuanzia U-17, U-20 na hadi klabu za Zanaco na Zesco ni matokeo ya jitihada hizo za Cosafa.

Hivyo ni wakati wa kuiga kutoka kwa kwa nchi hizo kwani kuna vitu vingi ambavyo sisi tunafanana nao hivyo haiwezi kuwa tabu kuiga ili kufika pale tunapotaka kufika.

Wenzetu wanataka kuona mabadiliko siku zote, lakini Ukanda wa Cecafa, wenyewe hauna mwamko, labda hawa viongozi waondoke, akina Nicholaus Musonye ambaye labda anataka kutawala kama alivyokuwa Issa Hayatou wa CAF.