Wameitwa baba kabla hawajafika hata miaka 20

KWA wachezaji wa vipaji, soka limewafanya kuwa na pesa nyingi wakiwa na umri mdogo sana. Kitendo cha kuwa na pesa kimewafanya kujibebesha majukumu mazito wakiwa bado na miaka ya utoto.

Ni majukumu mazito kwa sababu baadhi ya wachezaji hao walianza kuitwa baba wakiwa kwenye umri hata miaka 20 hawakuwa wamefika. Hawa hapa mastaa watano maarufu walioitwa baba wakiwa chini ya umri wa miaka 20.

5.Raheem Sterling (miaka 18)

Haitakuwa kosa kusema kwamba supastaa wa Manchester City, Raheem Sterling alikuwa na maisha yenye uchagu mwingi wakati yupo mdogo. Mara mbili zima alikutwa na hatia ya kuwafanyia unyanyasaji wanawake wawili tofauti.

Kumekuwa na uvumi kwamba Sterling ana zaidi ya toto mmoja kutoka kwa wanawake tofauti. Lakini, staa huyo wa England, mtoto wake anayefahamika ni mmoja tu, binti Melody Rose Sterling, aliyezaliwa mwaka 2012. Utambulisho wa mama yake Melody bado haufahamiki hadi sasa.

4.Anthony Martial (miaka 18)

Staa wa Manchester United, Anthony Martial ana mabinti wawili, Peyton na Toto Martial aliozaa na mrembo Samantha. Martial alikutana na Samantha akiwa na umri wa miaka 17 tu na mwaka mmoja, Samantha alipata ujauzito wa mtoto wao wa kwanza Peyton, hivyo Martial akawa baba akiwa na umri mdogo sana, hata miaka 20 hajafika. Hata hivyo, uhusiano huo wa Martial na mrembo Samantha umevunjika huku mama huyo akidai patna wake amebadilika tangu alipohamia kwenye klabu ya Manchester United akitokea AS Monaco.

3.Jack Wilshere (miaka 19)

Baada ya kusikia tu taarifa za ujauzito, Wilshere aliapa kwamba atakuwa bega kwa bega na patna wake, mrembo Lauren Neal kwa ajili ya mtoto wao. Septemba 29, 2011, Archie Jack Wilshere alizaliwa kumfanya Jack kuwa baba kipindi ambacho alikuwa na umri wa miaka 19 tu. Wapendanao hao, Jack na Lauren walifanikiwa kupata mtoto wawili, safari hii akiwa wa kike, Delilah Grace Wilshere, ambaye alizaliwa Septemba 26, 2013. Hata hivyo, wazazi hao waliachana na Wilshere alinasa kwenye penzi la mrembo mwingine, Andriani Michael.

2.Neymar (miaka 19)

Staa wa Brazil, Neymar ana mtoto wa kiume anayeitwa David Lucca Da Silva Santos, aliyezaa na mchumba wake wa zamani mrembo Carolina Nogueira Dantas. Lucca alizaliwa Agosti 24, 2011 huko Sao Paulo, Brazil. Kipindi hicho, Neymar alikuwa na umri wa miaka 19. Mrembo Carolina Dantas, ambaye alikuwa mwanafunzi wa chuo alikuwa na umri wa miaka 17 tu wakati anajifungua.

Mtoto Lucca kwa sasa anaishi na mama yake baada ya wazazi wake kutengana, kila mmoja kuchukua njia zake, lakini Neymar amekuwa akimtembelea mara kwa mara kumchukua kwenda kuponda naye raha.

1.Eden Hazard (miaka 19)

Akiwa na umri wa miaka 14 tu, Eden Hazard alimpenda mrembo mmoja aliyefahamika kwa jina la Natasha Van Honacker. Mapenzi yao yaliongezeka na kujikuta wakiwa pamoja na wawili hao walipata mtoto wao wa kiume Yannis Hazard mwaka 2010, wakati huo supastaa huyo wa Chelsea akiwa na umri wa miaka 19 tu. Wawili hao walioana mwaka 2012 na sasa wana watoto watatu. Hazard anatokea kwenye familia yenye wanasoka wengi tu, hivyo halitakuwa jambo la kushangaza kama watoto wake wanaamua kujihusisha na mchezo huo pia.