Walishakuja makocha wakali, haikusaidia tuvumilie tu

UTEUZI wa kumpata kocha yeyote duniani katika mchezo wa soka haujawahi kuwa na usahihi kwa asilimia mia moja. Kwamba kocha mpya atakuwa na kitu tofauti kabisa na aliyetangulia.

Siku zote ujio wa kocha mpya ndani ya timu hulenga kuimarisha timu ili kuipa mafanikio zaidi, hapo kikubwa ni kuipa timu mataji, hayo ndo matumaini ya kila mtu.

Lakini kwa sababu wanayemwajiri kocha ni binadamu wasiojua ya mbele, basi siku zote kinachotakiwa ni kuvuta subira na kuomba Mungu kocha mpya afanikiwe.

Suala hapa ni kocha wa timu ya Taifa, Taifa Stars, ambaye kila mpenda mpira wa miguu nchini anaomba afanikiwe kwani kufanikiwa kwake ni furaha yetu wote na kufeli kwake bado kutaendelea kutuumiza wote pia.

Baada ya uteuzi wa kocha mpya wa Stars, Emmanuel Amunike, kutangazwa, kumekuwa na maneno mengi kama ilivyo kawaida ya watu wa mpira. Hoja zinajengwa kuhusiana na uzoefu na mafanikio yake.

Wapo wanaosema hana uzoefu kwenye eneo la ukocha na kuwa hajapata mafanikio akiwa kocha mkuu hasa ngazi ya wakubwa, wengine wanasema ni kweli ana mafanikio makubwa kwenye ngazi ya uchezaji, lakini hawezi kuyabadili mafanikio hayo kuja kwenye eneo la ufundishaji.

Bado nawakumbuka makocha waliokuwa na takwimu kubwa kuanzia kwenye uchezaji hadi ngazi ya kufundisha waliowahi kuja nchini. Achilia makocha wakubwa waliopita Stars, kuanzia wazawa hadi wageni miaka hiyo ya akina Ray Gama , Joel Bendera na wengineo tuje kwa hawa wa miaka ya 2000 kuanzia Marcio Maximo alipoanza kufundisha akiwa kocha mgeni aliajiriwa Stars kwa utaratibu wa kisasa.

Mbrazili Maximo ana sifa kubwa ukiangalia wasifu wake kulinganisha na wa Amunike. Maximo angalau aliyejitahidi kuubadili mtazamo wa Watanzania kuhusiana na timu ya taifa, alitufanya tuipende Stars.

Alibadili mtizamo wa thamani ya Stars hata kwa wachezaji kuitambua timu ya Taifa kuwa ni kubwa kuliko klabu.

Ndio Maximo alikuja kama bahati na akajenga misingi mizuri namna ya kuisimamia timu ya taifa. Misingi ya namna ya kuwapata wachezaji wake, namna ya kuitambua timu yetu na kuipa thamani.

Ni yeye ndiye angalau alipata mafanikio kiasi, chini yake Tanzania ilijitangaza na ilicheza michezo mingi dhidi ya mataifa makubwa ya Afrika kama Cameroon, Senegal, Ivory Coast, Misri, Afrika Kusini bila kusahau kucheza na Brazil, moja kati ya mataifa makubwa kisoka duniani.

Maximo alipata mafanikio ya kutosha hasa pale alipoiwezesha Stars kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) kule Ivory Coast mwaka 2009. Mafanikio tosha.

Baadaye wakaja makocha wengine ambao kwa ujumla wasifu wao ni mkubwa pia kuliko wa Amunike. Alikuja Jan Poulsen, hakufanya kitu kabisa labda tumkumbuke kwa kuiwezesha Kilimanjaro Stars kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mwaka 2011 jijini Dar es Salaam, lakini huku kwenye michuano mikubwa AFCON na Kombe la Dunia hakuwa na jipya kabisa.

Haikuwa hivyo hata kwa aliyemfuatia, Kim Poulsen, ambaye alijitahidi angalau kuwa na mwelekeo wa ujenzi wa timu ya taifa ya baadaye, kweli aliwajengea uwezo vijana wa Ngorongoro Heroes na kupanda timu ya wakubwa na wakawa wanafanya vizuri.

Vijana kama Frank Domayo, Salum Abubakar, Thomas Ulimwengu, Juma Abdul na wengineo ambao walikuja kuisaidia Stars na kuwa tegemeo la nchi.

Alipoondoka Kim, pale Stars ikapelekwa Mart Noij. Ni kocha mwenye wasifu mkubwa kumpita Amunike huku akiwa na uzoefu wa soka la Afrika. Huyu naye hakufanya vizuri Stars, aliendelea kuididimiza nchi na kuishusha kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).

Bila shaka uteuzi wa kocha wa timu ya taifa unaendana na bahati, hauendani sana na nini kocha huyo amekifanya huko nyuma.

Nchi yetu ina changamoto kubwa hasa tunapozungumzia uundwaji wa timu ya taifa. Wachezaji wetu wengi hawajaundwa kwenye ubora mkubwa, hata kama wapo wanaocheza nje ya nchi.