MAONI: Walichofanya Zanzibar Heroes hakipaswi kuachwa bila kukemewa

Muktasari:

Missanga alitarajiwa kuzikwa jana kijijini kwao mkoani Singida atakumbukwa na mashabiki wa michezo kwa mchango wake kama mchezaji, kiongozi na pia mwanasiasa enzi hizo akikitumikia kiti cha Ubunge, Jimbo la Singida Kusini.

AWALI ya yote tunaungana na wanafamilia ya michezo nchini kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na rafiki wa aliyewahi kuwa Kiongozi wa Chama cha Soka Tanzania, FAT (sasa TFF), Alhaji Mohammed Missanga aliyefariki dunia.

Missanga alitarajiwa kuzikwa jana kijijini kwao mkoani Singida atakumbukwa na mashabiki wa michezo kwa mchango wake kama mchezaji, kiongozi na pia mwanasiasa enzi hizo akikitumikia kiti cha Ubunge, Jimbo la Singida Kusini.

Tunaamini Watanzania wapenda michezo na watu wa kada nyingine wataendelea kumwombea katika safari yake ya Akhera, lakini pia wakiendeleza yote mazuri aliyoyachangia katika kulikuza soka la Tanzania.

Muhimu ni kuiombea familia, ndugu na jamaa za marehemu Missanga kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao, lakini pia tukiwakumbusha kuwa, kila nafsi itaonja na mauti na kazi ya Mungu haina makosa.

Baada ya hilo, turejee kuwapongeza vijana wa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes kwa kuitoa kimasomaso Tanzania baada ya kutinga hatua ya Nusu Fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea nchini Kenya.

Kilichofanywa na Zanzibar Heroes ni kama kutufuta machozi Watanzania Bara kufuatia timu wawakilishi wetu, Kilimanjaro Stars kuchemsha na kufurushwa michuanoni kwa aibu bila kutarajiwa.

Kili Stars ambayo jana ilikuwa ikikamilisha ratiba kwa kuvaana na wenyeji, imetia aibu na kuwakera wadau wa michezo, huku vidole vya lawama vikielekezwa kwa Kocha Mkuu, Ammy Ninje na vingine uongozi wa TFF.

Kwa hakika hata Mwanaspoti tumesikitishwa na kufanya vibaya kwa Kili Stars kwani wakati timu inaondoka ilitoa matumaini makubwa ya kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania hata kama maandalizi yao yalikuwa ya zimamoto.

Kila mmoja aliyekuwa akiifuatilia, aliamini, kasi ya wachezaji wa Ligi Kuu, ushindani wa msimu huu hata timu ya taifa ingekuwa bora, lakini ni tofauti kabisa.

Kili Stars ilikuwa tofauti na ndugu zao wa Zanzibar, lakini ni Zanzibar Heroes iliyoweza kuthibitisha ule usemi wa umdhaniaye ndiye, siye.

Pongezai kwa vijana wa Zanzibar na tunawatakia kila la heri ili ikiwezekana warejee na ubingwa wa michuano hiyo.

Hata hivyo, pamoja na kuwapongeza vijana wa Kocha Hemed Morocco, pia tumesikitishwa na kitendo kilichofanywa na baadhi ya nyota wa timu hiyo kwa kushangilia ushindi wao dhidi ya Kili Stars kwa namna ya udhalilishaji.

Matusi na maneno ya kuudhi dhidi ya ndugu zao kwa sababu tu ya ushindi wa mabao 2-1 haukubaliki na tarajio letu ni kusikia na kuwaona viongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na hata wale wa TFF kuchukua hatua kwa wahusika.

Miongoni mwa nyota waliokuwa wakishangilia ushindi huo kidhalilishaji ni pamoja na wachezaji wanaocheza soka katika klabu za Ligi Kuu Bara, jambo ambalo haliingii akili kama wachezaji hao walifanya hivyo wakiwa timamu.

Watu waliowatolea matusi na kauli za kuudhi ndio wanaowalipa mishahara na kuwafanya waonekane kwa Kocha Morocco na kuitwa katika kikosi cha timu hiyo, ndio hao hao wanaowafanya wapate riziki zao za kila siku Tanzania Bara.

Hatutaki kuwahukumu, lakini tusingependa kuona uhuni kama huo unajirudia kwa wachezaji wa timu ya taifa kushindwa kudhibiti furaha zao za ushindi na kutukana kama mashabiki wa kihuni kwenye mechi za mchangani.

Huku ni kuwakosea adabu Watanzania wote waliowatuma kwenda Kenya katika michuano ya Chalenji na pia kujidhalilisha wenyewe na kujitoa thamani mbele ya viongozi, makocha na hata mashabiki wanaowafuatilia katika Ligi ya Bara.

Tunaamini huenda waliteleza, lakini bado hiyo haitufanyi tuliache hili lipite kama matukio mengine yasiyo ya kiungwana yanayofanywa na wachezaji wetu ambao wanapaswa kuwa mfano kwa chipukizi wanaojifunza kutoka kwao.

Tutawapongeza Zanzibar kwa hatua yao, lakini hatuwezi kuyafumbia macho hayo waliyoyafanya kwa kuwa si ya kiungwana na wala si ya kispoti.