MAONI YA MHARIRI: Wadau wa ngumi wanyoe ama kusuka ndani ya BFT

Muktasari:

Kama hakuna mashindano yoyote makubwa yanayohusisha mchezo huo kwa nia ya kuwapa nafasi wenye vipaji kuonyesha umahiri wao

NGUMI za Ridhaa Tanzania zipo Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU). Hakuna lugha nyepesi ya kuuzungumzia mchezo huo, zaidi ya kusema hivyo. Ngumi zina hali mbaya, ingawa wanaousimamia mchezo huo hawapendi hata kidogo kusikia hili likisemwa. Wanapenda kusikia wakisifiwa kwa kazi nzuri waliyofanya katika mchezo huo na kwamba ngumi zipo juu, ingawa kiuhalisia hata wao wenyewe wanajua kabisa kuwa mchezo huo umedorora kwelikweli kwa miaka ya karibuni.

Kama hakuna mashindano yoyote makubwa yanayohusisha mchezo huo kwa nia ya kuwapa nafasi wenye vipaji kuonyesha umahiri wao, utawezaji kusema ngumi zipo juu?

Kama kwa miaka kadhaa sasa mchezo huo umeshindwa kutuma mabondia katika michezo ya kimataifa na kurejea na medali, ni vipi watu wasiamini kuwa ngumi zimedorora?

Bahati nzuri ni kwamba mwaka 2018 umeangukia kwenye Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Riadha Tanzania (BFT) ambao utafanyika wikiendi hii mjini Dodoma.

Mchakato wa uchaguzi huo umezidi kupamba moto kwa wagombea mbalimbali kujitokeza kuwania nafasi zinazogombewa kwenye kinyang’anyiro hicho na wengi wa waliojitokeza ni viongozi wanaomaliza muda wao.

Wadau wa mchezo huo na hasa wanachama wa BFT watakaoshiriki uchaguzi huo kwa kupiga kura, ni wakati wao wa kuamua moja, kusuka ama kunyoa kwa kufanya maamuzi magumu yatakayoukomboa mchezo huo.

Wao ndio wenye jukumu la kuzipandisha ngumi nchini ama kuzizika kabisa kulingana na turufu za kura zilizopo mikononi mwao.

Ieleweke wazi, tunaposema wanachama wa BFT wanatakiwa kusuka ama kunyoa, haimaanishi kama tunawapinga viongozi wanaomaliza muda wao kurejeshwa madarakani ama kutaka kuwapigia kampeni wagombea wengine waliojitokeza.

Kama wadau wakuu wa michezo ikiwamo mchezo huo wa masumbwi, tungependa kuona wapiga kura wa BFT wanawachagua viongozi wanaoamini wanaweza kuzitoa ngumi mahali zilipo kwenda kwingine, bila kujali watawachugua wagombea gani?

Muhimu wao ni kutambua kuwa ngumi zinahitaji ukombozi, bila kujali ukombozi huo utafanywa na viongozi wanaomaliza muda wao ama wapya, kinachitakiwa ni kwamba waliojitokeza wana dhima ya kweli ya kuinua mchezo huo?

Inawezekana kabisa viongozi wanaomaliza muda wao walikuwa na dhamira nzuri kwa mchezo huo, lakini wakaangushana wenyewe kwa wenyewe kutokana na misimamo yao ama mitazamo ya ufanisi wa kazi. Hivyo kama watapewa ridhaa na kuungana na viongozi wengine wapya wanaweza kuzikomboa ngumi.

Kadhalika inawezekana wagombea wapya wanaojitokeza, hawana nia kweli ya kuzisaidia ngumi, ndio maana tumewaachia wapiga kura wa BFT kufanya maamuzi sahihi kwa manufaa ya mchezo huo.

Tunaamini mpaka kufika Jumamosi siku ya kufanya maamuzi kwenye sanduku la kura, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa BFT watakuwa wameshawapima vya kutosha wagombea kwa sababu tunajua watajitokeza mbele yao kwenye kampeni zao.

Wawasikilize, wawahoji na kuwapima wagombea hao na kujiridhisha kama ni kweli wanataka kuingia BFT ili kuwaletea mapinduzi kwenye mchezo huo?

Kama watabaini kuwa vigezo na dhamira yao ni ya kweli, basi wasisite kuwachagua kwenye Uchaguzi wa Jumapili ili BFT izaliwe upya na kuanza amshaamsha za kurejesha heshima na hamasa ya mchezo huo kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

Ngumi zina utamu wake, zina mashabiki wake na zimekuwa zikiwapa riziki wenye vipaji kuonyesha umahiri wao, wengine wakibahatika kupata ajira na kujiinua kimaisha kupitia mchezo huo.

Rekodi na historia za ngumi hizo nchini zinaonyesha hivyo. Mabondia wengi nyota wanaotamba ama waliowahi kutamba kwenye ngumi za kulipwa, wametokea kwenye ngumi za ridhaa.

Ndio maana mapema tumeanza kuwakumbusha wapiga kura wa BFT kwamba huu ni muda wa kufanya tathmini kisha kuchukua hatua kwa maendeleo ya mchezo wao. Kama si hivyo ni kuzidi kuua ngumi.