Wachezaji wapatiwe semina elikezi za maisha

Muktasari:

  • Pia, wafanyakazi ndio wenye kuamua wazalishe au wasizalishe chini ya usimamizi wa viongozi wa taasisi husika.

WAFANYAKAZI ni watu muhimu katika taasisi yoyote ile kuanzia za umma hadi binafsi zikiwemo zile za kidini.

Pia, wafanyakazi ndio wenye kuamua wazalishe au wasizalishe chini ya usimamizi wa viongozi wa taasisi husika. Ndio maana leo hii utasikia wafanyakazi wa taasisi fulani wakienda mji katika hoteli fulani kwa ajili ya kufanyiwa semina ya mafunzo ya kazi zao ili kuboresha utendaji wa kazi wanapokuwa kazini.

Na kwa viongozi utasikia kuna semina elekezi kwa ajili kuwafanya viongozi kukumbusha mambo katika utendaji wao. Hivyo umuhimu wa semina katika eneo lolote lile na kazi ni mkubwa kwa kuwa huwezi kumtenganisha mwanadamu na asili yake aliyoumbwa nayo, ambayo ni asili ya kusahau, hivyo semina huchukua nafasi ya kumkumbusha mfanyakazi majukumu yake.

Masheikh na Mapadri kuwakumbusha waumini kuacha kufanya mambo mabaya yaliyokatazwa na Mungu na kufanya mema.

Hii ni sawa na semina ninazozizungumzia hapa kwa kuwa wasipofanya hivyo asili ya mwanadamu ya kusahau, hutamalaki kuyateka maisha ya mwanadamu na kujikuta akishi kwa kufanya makosa kila siku .

Bahati mbaya wachezaji wetu wa Kibongo hukosa nafasi hiyo ya kupatiwa elimu ya semina katika sehemu zao za kazi, hivyo kujikuta wakiachwa peke yao na kukosa kukumbushwa juu ya majukumu yao ya kuchezaji. Pia, kukumbushwa kuhusu kazi hiyo na maisha yao baada ya kuacha kucheza soka.

Ni kweli makocha wa klabu huwa na wajibu wa kuwafundisha soka na kuwaelekeza mambo mengine yanayoendana na mchezo huo ili kutunza vipaji vyao na kuzisaidia timu zao, lakini maelekezo na mafunzo ya makocha kwa wachezaji huishia katika kumuwezesha mchezaji kuitumikia timu kwa muda huo tu, na kufikia malengo ya jumla ya timu huku malengo binafsi ya mchezaji yakibakia kwa mchezaji mwenyewe.

Kwa mfano, Emmanuel Okwi, John Bocco na Shiza Kichuya wametimiza malengo ya jumla ya timu yao na kutwaa ubingwa msimu huu chini ya usimamizi wa Kocha Pierre Lechantre ambaye amewasimamia vema hadi mwisho wa msimu wa ligi. Ukija kwenye malengo ya mchezaji mmoja mmoja ambayo kila mmoja hutakiwa kujiwekea kila mwaka, je, wamefanikiwa?

Na kama wamefanikiwa ni kwa kiasi gani?

Kusimamia malengo ya mchezaji mmoja mmoja sio jukumu la kocha ni jukumu la mchezaji mwenyewe kwani malengo hubadilika kila msimu kadiri miaka ya mchezaji inavyozidi kusogea mbele huku malengo ya jumla ya timu yoyote ile huwa hayabadiliki.

Mathalani, malengo binafsi ya mchezaji mwenye umri chini ya miaka 24 ni tofauti na mwenye umri wa zaidi ya miaka 28 kwani mwenye chini ya miaka 24 lazima awe na lengo binafsi la kuendelea hata kama timu itataka kumuendeleza lakini ni mchezaji kwanza ndiye mwenye wajibu wa kusimamia lengo hilo la kujiendeleza huku mchezaji mkongwe moja kati ya malengo binafsi ni kuangalia kile atakachokwenda kukifanya mara baada ya kumaliza kucheza mchezo wa soka.

Uwepo wa malengo haya binafsi na jinsi ya kuyasimamia katika utekelezaji wake ndicho kitu kinachokosekana kwa wachezaji wengi hapa nchini wanaocheza katika Ligi Kuu na ligi za chini hivyo ni ni wajibu wa viongozi saskutoa elimu kupitia semina kwa wachezaji wanaocheza soka kwa sasa kuhusu maisha ndani ya soka na maisha nje.

Kwani elimu ya maisha nje ya soka inahusisha malengo binafsi ya mchezaji ambayo hayamuhusu kocha wake. Ni muhimu viongozi klabu wakatenga muda wa wachezaji kuhudhuria katika semina zinazohusu mambo ya maisha ukiachilia semina zinazotakiwa kufanyika katika timu zao wakiwa kambini. Kwani kutokuwepo kwa semina hizo kunawafanya waishi katika dunia yao peke yao inayohusisha mchezo wa soka tu wakati dunia ya sasa ni ya utandawazi inahitaji jicho la biashara katika kila eneo.

Ndio maana leo hii unawaona wachezaji kama kina Dani Alves wa PSG na Mturuki, Nuri Sahini wa Borussia Sortmund wakijihusisha elimu ya biashara katika Chuo Kikuu cha Havard cha Marekani ili wapate elimu ya biashara.

Wachezaji hao wanatambua biashara ni sehemu muhimu ya maisha ambayo mwanadamu yeyote hawezi kuikwepa, hivyo ni lazima awe na elimu ya biashara ili aishi baada ya mpira. Hapa kwetu haijatokea mchezaji wa soka kuhudhuria semina za ujasiriamali na fursa zinazoendeshwa mitaani kila siku.

Kwa leo naomba kusihi hapo huku nikisubiri mrejesho kutoka kwako !