MAONI YA MHARIRI: Wachezaji waepuke mchezo wa kibabe, hasira viwanjani

Muktasari:

Ni mchezo unaohimiza uungwana zaidi uwanjani kwa nia ya kujenga upendo, urafiki na umoja.

SOKA ni moja ya michezo inayotajwa kama ya kistaarabu na yenye kujenga umoja, upendo na urafiki.

Ukitaka kujua soka ni mchezo wa kiungwana fuatilia baada ya kumalizika kwa pambano namna wachezaji wa timu pinzani wanavyokuwa wakikumbatiana, kupongezana kwa furaha bila kujalisha kama upande mmoja umepoteza mchezo.

Ni mchezo unaohimiza uungwana zaidi uwanjani kwa nia ya kujenga upendo, urafiki na umoja. Hata itokeapo baadhi ya wachezaji wakataka kuvuruga uungwana huo, waamuzi wanaochezesha huchukua hatua kulingana na sheria zinazomwongoza kwa nia ya kutaka kufanya dakika 90 za mchezo husika kuwa wa kistaarabu na sio vurugu.

Ndio maana wachezaji wanaovuka mipaka kwa kufanya matukio yanayoashiria kutaka kuvuruga mchezo, huonywa kwa kadi ya njano ama kutolewa kwa kadi nyekundu na wakati mwingine huadhibiwa na mamlaka ya soka ili kutoa funzo kwa wengine wenye akili za kutaka kuharibu sifa ya mchezo huo.

Katika Ligi Kuu Bara kumekuwa na matukio mbalimbali yanayofanyika ndani ya uwanja ambayo huwa ni hatarishi kwa wachezaji na kama sio umakini wa waamuzi ni wazi soka letu lingekuwa likiharibika.

Wapo baadhi ya wachezaji huwa na tabia za kucheza kibabe, huku wakiwakamia wenzao wa timu pinzani kiasi cha kuharibu ladha na sifa ya soka.

Matukio ya wachezaji kufanya matukio yasiyo ya kiungwana ni kati ya mambo yanayopingwa.

Shirikisho la Soka Dunia (FIFA) limekuwa likihimiza mchezo wa uungwana na kila kwenye pambano lolote la soka imekuwa ikishuhudiwa kila mara bendera yenye maandishi yanayosomeka ‘My Game is Fair Play’.

Msimu uliopita aliyekuwa straika wa Stand United, Abaslim Chidiebele almanusura apate ulemavu wa kudumu baada ya kuchezewa vibaya na beki wa Azam, Aggrey Morris aliyekuja kufungiwa na Shirikisho la Soka (TFF).

Msimu huu wiki iliyopita ilishuhudiwa namna winga wa Yanga, Emmanuel Martin alivyozimia Uwanja wa Majimaji, Songea kutokana na kuchezewa vibaya na beki wa Majimaji. Matukio ya aina hiyo ni mengi na yamekuwa yakiharatisha maisha ya wachezaji uwanjani.

Ndio maana tunawakumbusha wachezaji, soka ni mchezo wa uungwana na kama kuna ulazima wa matumizi ya nguvu, waangalie wasihatarishe maisha ya wenzao kwani ni hatari hata kwao wenyewe.

Kuna pambano moja la Ligi Mkoa wa Dar es Salaam lililochezwa Uwanja wa Mwalimu Nyerere, Magomeni, beki wa timu moja alimfuata akiwa na nia mbaya ya kumuumiza mshambuliaji wa timu pinzani, kilichotokea daluga lake lilimkosa straika huyo aliyemkwepa na beki huyo kujikuta akivunja mguu bila kutarajia.

Kwa wale wanaokumbuka Mei 5, 2001 katika pambano la Ligi Kuu Bara kati ya 44 KJ ya Mbeya na AFC Arusha ilishuhudiwa maafa baada ya wachezaji wawili kugongana wakati wakiwania mpira. Tukio hilo lililotokea kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya kipa Nadhir Mussa Mchomba wa AFC Arusha, alipoteza maisha uwanjani hapo baada ya daluga la Kenneth Pesambili wa 44 KJ kulikata koromeo lake.

Tunakumbusha tukio hayo kama njia ya kuonyesha kuwa kuna haja ya wachezaji kuwa makini uwanjani kwa kucheza kistaarabu ili kuepuka kusababisha maafa au kupeana ulemavu wa kudumu kutokana na matumizi makubwa ya nguvu.

Ndio maana Mwanaspoti tunawahimiza wachezaji wetu bila kujali nafasi wanazocheza kuwa ni lazima wacheze kiungwana na kuepuka ubabe na hasira za kukamiana ili kuepuka kusababisha madhara ama maafa bila sababu ya msingi.

Pia tunawakumbusha pia kwenye viwanja vyetu kuna udhaifu mkubwa katika utolewaji wa Huduma za Kwanza na wakati mwingine hata magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) huwa hayapo, hivyo ni vema tahadhari ikawepo.

Tahadhari ni pamoja na wachezaji kucheza kiungwana na hata kama kuna matumizi ya nguvu, basi yasiwe makubwa kiasi cha kusababisha madhara yanayoweza kuleta maafa uwanjani na kuharibu sifa nzima ya mchezo wa soka.