MAONI: Wachezaji wachangamkie fedha, lakini wakiikumbuka kesho yao

Muktasari:

Klabu zimekuwa zikipigana vikumbo kuimarisha vikosi vyao, huku nyingine zikiwapa mapumziko mafupi nyota wao kusudi wakajiweke tayari kabla ligi haijaendelea baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea nchini Kenya.

LIGI Kuu Bara ipo mapumziko, huku kukiwa na pilikapilika za dirisha dogo la usajili. Dirisha hilo lililofunguliwa Novemba 15, limesaliwa na siku kama 10 tu kabla ya kufungwa Desemba 15.

Klabu zimekuwa zikipigana vikumbo kuimarisha vikosi vyao, huku nyingine zikiwapa mapumziko mafupi nyota wao kusudi wakajiweke tayari kabla ligi haijaendelea baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea nchini Kenya.

Michuano hiyo ndiyo iliyoisimamisha ligi hiyo baada ya waandaaji wake Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kuirejesha tena baada ya kushindwa kufanyika tangu ilipochezwa mara ya mwisho mwaka 2015.

Wakati ligi ikiwa mapumziko, kuna baadhi ya wachezaji wa klabu hizo za Ligi Kuu wameanza kuchangamkia dirisha dogo la usajili, huku wengine wakianza kutikisa viberiti kwa vile mikataba yao na klabu zao inaelekea ukingoni.

Hakuna ubishi licha ya dirisha la usajili lipo wazi kwa klabu zote kuanzia zile za Daraja la Kwanza, La Pili mpaka Ligi Kuu, zinazoonekana kuchangamkia zaidi ni za Ligi Kuu Bara.

Kila uchao utasikia mabosi wa klabu kubwa wakipigana vikumbo kunasa saini za nyota wa ndani na nje ya nchi, huku Simba na Yanga zikiendeleza ligi yao ya kila kipindi cha usajili.

Japo Yanga kwa sasa hawana raha hata kidogo, baada ya mifuko yao kukauka, lakini nao wanapambana kuendelea kulinda heshima yao mbele ya watani. Bila ya shaka tunaamini klabu hizo zinachuana hivyo kwa nia ya kufunika michuano ya kimataifa mwakani.

Mwanaspoti limevutiwa na namna baadhi ya nyota wa soka nchini kwa zama hizo wanavyojua kuchangamkia fedha. Nyota ambao wanajua mikataba yao inaelekea ukingoni ama wanahisi wanazinguliwa na klabu zao wamejiongeza, hasa baada ya kutambua kuwa soka ni ajira yao.

Wanachangamka kusaka noti katika madirisha ya usajili ndani ya klabu zao, pia kutafuta fursa nje ya klabu zao ilimradi maisha yao yawe mepesi. Hivi ndivyo inavyotakiwa.

Soka la sasa ni biashara, wasipochangamka watakuja kujuta mbeleni pale watakapoanza kuchokwa viwanjani.

Katika dirisha lililopita tuliona namna Jonas Mkude amesainishwa mkataba mpya Simba wenye donge nono, kina Aishi Manula, John Bocco, Shomari Kapombe, Kenny Ally na wengine kadhalika nao walichangamka kama ilivyokuwa kwa Ibrahim Ajib.

Walichokifanya wachezaji hao ni sahihi, lazima wakusanye chao mapema, japo tunaendelea kuwakumbusha tu, wanachokivuna sasa katika soka, wakumbuke kujiwekea akiba ama kutumia kujijengea misingi wa maisha ya baadaye watakapostaafu soka.

Tusingependa kuona wanarejea yale yaliyowahi kufanywa na kaka ama baba zao waliocheza soka na kupata vipato vya kutosha, lakini wakajisahau kujiwekea misingi na baada ya kustaafu wamekuwa kero kwa ndugu, jamaa na rafiki zao kwa kupiga mizinga kila wanayekutana naye.

Ndio maana tunawasisitizia kina Mkude, Ajib, Kenny, Kapombe na wengine, wasilaze damu...mamilioni wanayovuna waitumie kama mitaji ya miradi ya maendeleo ili ije iwakomboe watakapotundika daluga.

Wasizuzuke na mamilioni hayo...hicho wanachokipata ni sehemu ndogo sana ya lile jasho wanalovuja uwanjani ama kipato wanachoziingizia klabu zao, lakini ni kingi kama watakitunza na kukitumia kwa maarifa.

Hiki ni kipindi cha kutengeneza maisha yao ya baadaye na katu wasilaze damu, wachangamke kuzikusanya noti sasa na kuendelea kutunza viwango vyao ili wavune zaidi na wasifanye makosa na kupita njia iliyopitwa na mastaa wa ndani na hata wale wa kimataifa kama kina Paul Gascoigne ‘Gazza’ wa kule England ama Eric Djemba Djemba wa Cameroon.

Nyota hawa waliogelea fedha na kuvuna mamilioni enzi wakicheza soka la kusisimua, lakini walijisahau na sasa wanaishi kidhalili kiasi cha kutia huruma.

Kwa vile mtu hujifunza kutokana na makosa ni wazi wachezaji wetu wataamka sasa na kujipanga kwa mustakabali wa maisha yao baada ya kustaafu kwa kujiwekea akiba na kutumia fedha zao kwa akili.