MAONI: Wachezaji Stars wazitendee haki mechi zijazo za kirafiki

Muktasari:

Kwa muda mrefu wadau wa soka nchini wamekuwa wakipiga kelele juu ya uwepo wa mechi ngumu za kirafiki ambazo zinaweza kuiimarisha zaidi Taifa Stars, kilio ambacho Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) sasa wamekitendea haki.

KWA mara ya kwanza baada ya kipind kirefu, Taifa Stars itacheza mechi mbili kubwa za kirafiki wiki ijayo dhidi ya Algeria na DR Congo.

Kwa muda mrefu wadau wa soka nchini wamekuwa wakipiga kelele juu ya uwepo wa mechi ngumu za kirafiki ambazo zinaweza kuiimarisha zaidi Taifa Stars, kilio ambacho Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) sasa wamekitendea haki.

Baada ya kipindi kirefu kucheza mechi za kawaida za kirafiki, sasa tunakabiliwa na michezo migumu ambayo inahitaji umakini mkubwa kuikabili.

Kipindi cha nyuma tuliona Taifa Stars ikicheza michezo mikubwa ya kirafiki kama dhidi ya Ghana, Cameroon, Afrika Kusini na mingineyo lakini hivi karibuni mambo yaligeuka kabisa.

Kwanza, tunapenda kuipongeza TFF kwa kazi kubwa waliyofanya ya kutafuta michezo hiyo ambayo bila shaka itakuwa na manufaa makubwa zaidi kwetu.

Mchezo wa kwanza utakuwa ugenini dhidi ya Algeria ambayo inaundwa na mastaa wengi wakubwa wanaotamba kwenye Ligi za Ulaya.

Tunakwenda kwenye mchezo huo na kumbukumbu mbaya ya kufungwa mabao 7-0 kwenye mchezo wa mwisho tuliokutana na Waarabu hao hivyo umakini mkubwa unahitajika ili kuwakabili tena.

Stars ilipokea kipigo hicho cha aibu mwishoni mwa 2015 wakati huo ikiwania kusaka nafasi ya kuingia kwenye hatua ya makundi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia litakalofanyika baadaye mwaka huu nchini Urusi.

Kipigo hicho mpaka sasa ndiyo kikubwa zaidi kwa timu ya Taifa tangu Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961.

Wakati huu ambapo Taifa Stars inakwenda tena Algeria, ni mwafaka kutafakari historia hiyo mbovu tuliyoweka kwenye mchezo wa mwisho dhidi yao.

Hakuna ubishi kwamba wachezaji wote wa Taifa Stars pamoja na benchi la ufundi wanatakiwa kuweka uzito mkubwa kwenye mchezo huo vinginevyo historia mbovu zaidi inaweza kuandikwa.

Ikumbukwe kwamba Taifa Stars iliyocheza na Algeria kipindi kile ilikuwa imara kuliko ya sasa hivyo umakini ndiyo kitu pekee ambacho kitatusaidia.

Ni wazi kwamba Algeria imekuwa na anguko kubwa la soka tangu kipindi hicho, lakini bado uwepo wa wachezaji mahiri kama Islam Sliman, Riyard Mahrez, Yacine Brahim na wengineo ni hatari kwenye mchezo huo.

Tunapenda kuwahimiza nyota hao wa Taifa Stars kuuchukulia mchezo huo kwa uzito mkubwa, kucheza kwa utulivu pamoja na kujituma ili tuweze kuandika historia safi.

Kwa upande mwingine tutakuwa na mchezo mwingine mzuri nyumbani dhidi ya DR Congo ambayo kwa muda mrefu sasa imekuwa miongoni mwa timu nne bora Afrika.

Wakongomani hao walikaribia kufuzu Kombe la Dunia mwaka huu kabla ya kutibuliwa dakika za mwisho.

Pia wamekuwa mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) na pia wamefanikiwa kufika nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika mara tatu mfululizo.

Hii ni ishara tosha kuwa tunakwenda kucheza na timu nyingine bora Afrika na ambayo itatupa ushindani wa kweli.

Pamoja na kwamba michezo hii inasaidia katika kupanda kwenye viwango vya Fifa, pia tunapaswa kuitumia kama sehemu ya kuimarisha uchezaji wa timu yetu ili iweze kuwa na ushindani zaidi.

Tufahamu kwamba tunakabiliwa na michezo migumu ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika (AFCON) dhidi ya Uganda na Cape Verde hivyo michezo hii inapaswa kutufungulia milango.

Kama tutaweza kujenga timu ya kushindana na Algeria ugenini na kisha Congo hapa nyumbani, kwanini tushindwe kupata matokeo dhidi ya Uganda na Cape Verde.

Pamoja na yote, tuendelee kuisapoti timu yetu ya Taifa kwa nguvu kubwa ili iweze kuandika historia mpya na kuondokana na unyonge.

Kwa miaka mingi sasa Taifa Stars imeonekana kama daraja la timu nyingine kubwa Afrika, kitu ambacho si kizuri.

Kila Mtanzania anataka kuona timu ya Tanzania ikifanya vizuri, na kuanza kwa sare ya 1-1 na Lesotho katika mechi ya Kundi L kwa kweli imewavunja nguvu mashabiki na imani yao kubwa itatokana na matokeo ya mechi zijazo za kirafiki.