MAONI YA MHARIRI: Wachezaji Ligi Kuu watumie mapumziko yao kujipanga upya

Friday December 1 2017

 

LIGI Kuu Tanzania Bara imesimama mpaka wakati wa Sikukuu za krismasi na wachezaji wa timu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo wamepewa mapumziko marefu ili kuweka miili yao sawa kabla ya kuanza kwa duru la pili.

Ligi hiyo kubwa zaidi nchini imewekwa kando ili kupisha mashindano ya Kombe la Chalenji yanayotarajiwa kuanza nchini Kenya wikiendi hii.

Hilo limekwenda sambamba na mapumziko ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) pamoja na Daraja la Pili (SDL) ili kusubiri mzunguko wa lala salama.

Ligi hizo zimekwenda mapumziko wakati wa usajili wa dirisha dogo pia ili kutoa fursa kwa timu zao kusajili wachezaji ambao wanaweza kuwa msaada kwao katika mzunguko wa pili.

Usajili huo ni mahususi kwa kurekebisha maeneo ambayo yameonyesha mapungufu katika mechi ambazo wamecheza mpaka sasa, hivyo unapaswa kufanyika kwa umakini mkubwa sana.

Kutokana na ligi hizo kwenda likizo, nyota wanaocheza katika timu hizo pia wamepewa mapumziko mafupi ili kuweka miili yao sawa kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili ambao ni mkali na ndiyo wa lala salama.

Wapo waliopewa mapumziko ya wiki moja huku wengine wakipewa wiki kadhaa kutokana na ratiba ya kocha husika na malengo ya timu wakati utakapoanza mzunguko wa pili.

Ni wazi pia hata mazoezi yatakapoanza hayatakuwa magumu kama yale ya wakati msimu ukiendelea ama wakati wa maandalizi ya mwanzo wa msimu, kwani bado kuna muda mrefu kabla ya pazia hilo la Ligi Kuu kufunguliwa wakati huo wa Krismasi.

Hii inamaanisha wachezaji watapata muda mwingi zaidi wa kupumzika, jambo ambalo huwagharimu nyota wengine hasa waliokuwa na viwango bora wakati wa mzunguko wa kwanza.

Kila sehemu duniani mapumziko ya katikati ya msimu ama mwishoni mwa msimu huwa sumu kwa baadhi ya wachezaji, kwani wengine hurejea wakiwa wameshuka viwango na kupoteza nafasi zao katika vikosi vya kwanza.

Tunapenda kuwapa neno wachezaji wa Ligi Kuu pamoja na wale wa madaraja ya chini kuwa wanapaswa kuitumia likizo yao vizuri na kuhakikisha wanaendelea kuwa katika viwango bora.

Wajiepushe na anasa na starehe ambazo zinaweza kuwakwamisha katika mzunguko wa pili hasa kuwarudisha nyuma kisoka.

Hawakatazwi kujiachia na kula bata, bali wafanye hilo kwa kiwango ili kujiondoa na hatari ya kushusha viwango vyao.

Tunafahamu baadhi ya wachezaji wamekuwa wakitumia vibaya likizo hii kwa kwenda kujirusha kwenye kumbi za starehe pamoja na kukesha jambo ambalo huwafanya wachoke zaidi ya wakati ligi inaendelea.

Mwili wa mwanadamu unahitaji muda wa kutosha kupumzika hivyo kwenda kujirusha kulikopitiliza kunaweza kuwarudisha nyuma wachezaji hao ambao wanategemewa na timu zao.

Ikumbuke duru la pili huziweka timu katika nafasi halisi za kuwania ubingwa ama kuepuka kushuka daraja, hivyo viwango vya wachezaji wake ni muhimu sana.

Timu ambazo zipo katika eneo la kushuka daraja zinawahitaji nyota wake kuwa bora zaidi ili kuepuka dhahama hiyo ambayo huenda ikawapoteza katika ramani ya soka.

Timu kama Simba, Yanga na Azam ambazo zinawania ubingwa wa Ligi Kuu zinawahitaji nyota wake wawe bora zaidi ili kuweza kuwapa heshima hiyo kubwa katika soka la Tanzania.

Mchezaji anapojikita katika starehe na kujiachia sana, hujiweka katika hatari ya kuumia pia. Si ajabu kuona mechi za mzunguko wa pili zimeanza halafu wachezaji wanaanza kuwa na majeraha ya mara kwa mara, kutokana na tu kushindwa kuitunza miili yao wakati huu wa mapumziko.

Wachezaji wanatakiwa kutumia muda huu kwa kuufikiria zaidi mzunguko wa pili kwa kuyazingatia yale mazoezi uliyofundishwa na kocha wako.

Pia kuzingatia mambo mengine ikiwemo ulaji wa vyakula na kupumzika kwa wakati ili kuufanya mwili uwe tayari kwa mikikimikiki ya mzunguko huo unaotarajiwa kuwa mkali kutokana na sajili mbalimbali zinazofanywa.