Buswita kiulaini Yanga

Muktasari:

Niweke rekodi sawa mchezaji mwenyewe alikiri ni kweli alisaini mkataba na atarudisha pesa ya Simba.
Elias Mwanjala - M’KITI KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji TFF

KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungulia kiungo wa Yanga, Pius Buswita na sasa atacheza Jangwani.

Buswita aliyejiunga na Yanga akitokea Mbao FC ya Mwanza, alipata kifungo cha mwaka mmoja wiki chache zilizopita baada ya kuonekana kuwa alisaini Simba na Yanga kinyume na kanuni ya 66 ya Ligi Kuu.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Elias Mwanjala alisema baada ya kikao cha kamati yake juzi Jumanne, Simba iliwakilishwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Said Tulliy huku Yanga akihudhuria Kaimu Katibu Mkuu, Baraka Dausdedit.

“Kamati yangu imempa ruksa Buswita kucheza Yanga lakini kabla ya kuanza kucheza anatakiwa kulipa Sh10 milioni ambayo aliichukua Simba na kusaini mkataba,” alisema Mwanjala.

“Niweke rekodi sawa kwamba mchezaji mwenyewe alikiri kuwa ni kweli alisaini mkataba na atarudisha pesa ya Simba,” alisema.