MAONI YA MHARIRI: Wachezaji Ligi Kuu wajifunze sakata la Pius Buswita

Thursday September 7 2017

 

KUNA wakati busara huwa zinatumika ili kuokoa kitu fulani kisiangamie ama kuteketea kutokana na ujinga uliofanywa na mtu ama kikundi cha watu fulani.

Busara hufanyika mahususi kuokoa maisha ya kitu hicho kwani uhai wake unaweza kuwa na manufaa zaidi kwa siku za usoni licha ya kwamba tayari kuna makosa yaliyofanyika.

Wakati huu busara imetumika kusaidia kipaji cha chipukizi, Pius Buswita aliyekuwa amefungiwa kujihusisha na soka kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kupatikana na makosa ya kimkataba ambayo yameainishwa kwenye kanuni za Ligi Kuu Bara.

Buswita alifungiwa baada ya kubainika kuwa alisaini mkataba wa kuzichezea Simba na Yanga kwa wakati mmoja kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni za Ligi Kuu Bara ambazo ndiyo zinatengeneza msingi wa mashindano hayo.

Kanuni ya 66 ya Ligi Kuu inaeleza wazi kwamba mchezaji atakayefanya hivyo, atafungiwa kujihusisha na soka kwa muda wa mwaka mmoja.

Kanuni hiyo imewekwa ili kuzuia vurugu katika kipindi cha usajili.

Baada ya Kanuni kutumika hapo awali kumfungia kiungo huyo aliyeichezea Mbao FC msimu uliopita, hatimaye busara imetumika kutengua adhabu hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Elius Mwanjala ni kwamba wamekubaliana mchezaji huyo aichezee Yanga lakini baada ya kurudisha fedha za Simba kiasi cha Sh 10 milioni.

Katika hali ya kawaida, hakuna sehemu kanuni inaruhusu haya kufanyika ila katika hali ya kibinadamu, TFF imeamua kufanya hivyo ili kumsaidia mchezaji huyo mwenye upeo mdogo wa kufikiri.

Endapo TFF ingeshikilia msimamo wake wa mwanzo, Buswita angeshindwa kucheza soka kwa mwaka mzima jambo ambalo lingeshusha thamani yake na kuhatarisha kiwango chake pia.

Hatutetei maovu kwa wachezaji kuvunja kanuni na TFF kuvunja kanuni pia ili kumsaidia mchezaji, lakini kwa hili tunaona angalau afya ya kipaji cha mchezaji husika imetazamwa.

Kitu cha msingi ni kwamba baada hili la Buswita kumalizika, tusingependa kuona wachezaji wengine wakijiingiza katika matatizo kama haya ambayo yatarudisha nyuma ufanisi wao wa uwanjani.

Tunafahamu kwamba kipindi cha usajili huwa na ushawishi mwingi kwa wachezaji ambapo fedha hutumika kuwarubuni lakini siyo sababu ya wao kulainika kirahisi na kuvunja kanuni.

Licha ya kwamba pesa ni sabuni ya roho lakini ifike sehemu tuheshimu taratibu na mamlaka zilizowekwa badala ya kuwa sehemu ya matatizo.

Wachezaji wanatakiwa kufanya uchaguzi wa timu wanayotaka kwenda mapema na kusaini kisha kuheshimu kile walichopewa kwani ndiyo kitu cha muhimu zaidi kwao.

Masuala ya mikataba ni ya kisheria na hayapaswi kupindishwa, hivyo mchezaji akisaini tu tayari anakuwa amejifunga na timu ambayo imempatia mkataba huo.

Kutokana na hilo, hakuna sababu ya mchezaji kwenda kusaini timu nyingine tena.

Watu wanaowazunguka wachezaji hawa wanapaswa kuwaambia ukweli juu ya masuala haya ili wajiepushe na matatizo ambayo yataua vipaji vyao.

Tuliona msimu uliopita, Mohammed Mkopi akishindwa kucheza kutokana na sakata kama hili ambalo halina manufaa yoyote kwa soka la mchezaji.

Hata kama mapenzi ya mchezaji yapo timu fulani, basi ajichunge asiingie mikataba mara mbili mbili kitendo ambacho kinaweza kumletea matatizo makubwa.

Busara iliyotumika na TFF sasa siyo sheria hivyo mchezaji mwingine atakayepatikana na kosa kama la Buswita anaweza asisamehewe kama mwenzake hivyo ni vyema kujiepusha mapema na matatizo kama haya.

Pamoja na yote, tunapenda kuikumbusha TFF kusimamia kanuni zake ili kutoa nidhamu kwa wachezaji na wadau wengine kwani ndiyo soka imara linavyotengenezwa.