Vigogo Simba watumia akili kudhibiti mastaa

Muktasari:

Mechi hiyo ngumu itapigwa saa 2:30 usiku kwa saa za Tanzania na mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya CAF, Simba ikihitaji ushindi wa aina yoyote ili kuingia raundi ya pili ya play-off ya 16 Bora.

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Simba leo usiku wanakabiliwa na mechi ngumu ya kuwania kusonga mbele dhidi ya wenyeji wao Al Masry ya hapa Misri.

Mechi hiyo ngumu itapigwa saa 2:30 usiku kwa saa za Tanzania na mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya CAF, Simba ikihitaji ushindi wa aina yoyote ili kuingia raundi ya pili ya play-off ya 16 Bora.

Simba inaingia kwenye mchezo huo kwa tahadhari kubwa baada ya sare ya mabao 2-2 jijini Dar es Salaam.

Umuhimu wa mchezo huo uliifanya Simba isafiri mapema kuwahi mjini hapa ili kuweka hesabu zake sawa kabla ya mchezo huo wa marudiano ambao, unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.

Simba iliwasili hapa Port Said, alfajiri ya juzi Alhamisi na kuunganisha kupata chai kisha wachezaji kutakiwa kupata muda wa kupumzika ili kuwa fiti na mazoezi ya jioni.

Hata hivyo, wachezaji wengi hawakutaka kupumzika na badala yake walianza kujinafasi kwenye maeneo mbalimbali ya hoteli wakichati.

Hali hiyo ni kama haikumfurahisha Kocha Mkuu, Pierre Lechantre na mabosi wa Simba ambao walifanya mikakati ya kimya kimya kuhakikisha intaneti inazimwa ili nyota hao wakose cha kufanya na kuingia vyumbani kupumzika.

Mkakati huo ulifanikiwa na nyota hao walilazimika kupumzika hadi baada ya chakula cha mchana ndipo wakafunguliwa mtandao huo ili waweze kujiliwaza.

Mmoja wa viongozi wa Simba alisema; “Tuliona wachezaji hawatapumzika hapa tukaamua kuomba hoteli iwapunguzie kasi ya kuchati na ndio sababu utaona wakati fulani hakukuwa na mtandao. Tunataka wachezaji wapumzike uchovu uishe kabisa kabla ya mchezo.”

TAHADHARI KUBWA

Siku ya kwanza baada ya Simba kutua hapa Misri hawakuwa na presha kubwa ya kufanyiwa fitna kutokana na wenyeji wao kuwa na ukarimu kimtindo, lakini bado mabosi wa timu hiyo wameendelea kuwa na tahadhari kubwa.

Mabosi hao walitaka kitu chochote kinachotakiwa kufanywa kwenye vyumba vya wachezaji ikiwemo usafi vifanywe baada ya kutolewa ruhusa yao.

Pia, wamechukua tahadhari kubwa kwa upande wa vyakula na Alhamisi walikula hotelini hapo, lakini jana Ijumaa waliweka mipango ya kupata chakula sehemu nyingine ili kujiepusha na fitna hizo.

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ pamoja na vigogo wengine wa timu hiyo wamekuwa wakifanya mipango yao kwa siri na kwa ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.

“Kwa upande wa kukwepa fitna zao tuko makini. Tumeona ukarimu wao, lakini hatufahamu wamepanga nini.

“Tutakuwa tukibadilika kila wakati ili tuweze kuwa salama wakati wote kabla ya mchezo.

“Kuna Watanzania wameahidi kuwa hapa kuanzia kesho (Ijumaa) na watatusaidia kulinda vyumba vya wachezaji na kwenye mambo mengine ya muhimu,” alisema Tryagain.

Simba pia ilikuwa na tahadhari kwenye basi la wachezaji kwani liko chini ya Al Masry.

ULINZI MWANZO MWISHO

Hapa mjini Port Said maofisa usalama wako makini na msafara wa Simba kuliko kitu kingine chochote. Tangu Simba ifike hapa, maofisa hao wamepiga kambi nje ya hoteli ya Nora and Style ili kuhakikisha kila mtu aliyetua na msafara huo yupo salama.

Askari hao wameegesha gari lao pamoja na farasi nje ya hoteli hiyo na wamekuwa makini kuhakikisha wanafahamu muda ambao, watu wametoka na kama wanakwenda mbali ama karibu.

Mmoja wa maofisa hao alitueleza kuwa kila sehemu tunayokwenda tunatakiwa kupata eskoti yao ili kuhakikisha usalama unakuwa juu. Timu inapokwenda mazoezini imekuwa ikipewa gari ya polisi ili kuongoza msafara pamoja na kusindikizwa na maofisa kadhaa ambao, wamekuwa wakihakikisha usalama upo.

Maofisa wengi ambao wamevalia suti na kubeba bastola, walizunguka kila kona ya uwanja na kuwaondoa watu wote wasio na shughuli maalumu.

MSOSI FRESHI

Kama kuna mtu analalamika kuhusu chakula cha hapa Port Said, basi atakuwa na lake kwani ni wa kawaida na unalika vizuri.

Chakula ambacho wamekuwa wakipewa wachezaji wa Simba hakina tofauti kubwa sana na kile cha Dar es Salaam japokuwa kimeongezwa nakshi kidogo za Kiarabu.

Kama unavyofahamu Waarabu kwenye kula huwa hawarembi hivyo, mapishi yao yameongezwa ufundi na kama umetoka kijijini unaweza kushindwa kula, lakini kwa wale wa mjini wala hakuna tatizo.

Mbali na chakula cha hoteli, maeneo mengi hapa Port Said yanafanya biashara ya chakula kwani, ndiyo inayoonekana kutoka kwa haraka zaidi.