STRAIKA WA MWANASPOTI: Vifo vya mashabiki hawa viwe funzo kote

Muktasari:

Zaidi ya mashabiki wanne wanatajwa kufariki katika ajali hiyo.

NCHINI Kenya kwa sasa, anga lake la soka lina majonzi yanayotokana na vifo vya mashabiki vilivyotokea wikiendi iliyopita katika ajali ya barabarani. Vifo hivyo viliwakuta walipokuwa wakielekea Machakos kutazama mechi baina ya Gor Mahia na Thika United iliyochezwa juzi Jumapili. Zaidi ya mashabiki wanne wanatajwa kufariki katika ajali hiyo.

Ni jambo la kusikitisha kusikia kwamba mashabiki hao walikuwa sehemu ya waliokuwa wakining’inia katika basi lililohusika kwenye ajali hiyo.

Ajali hii imerejesha nyuma kumbukumbu zangu. Miaka miwili iliyopita niliwahi kuandika katika mtandao wa kijamii na kushutumu tabia hii ambayo hakika imekita mizizi si Kenya tu, bali hata Tanzania ambako nimewahi kuishi na kucheza soka.

Ni tabia ambayo tumekuwa tukiishuhudia zaidi Kenya zinapochezwa mechi zinazozihusu Gor Mahia na AFC Leopards, ni kama vile Tanzania kunapokuwa na mechi za Simba na Yanga, zenyewe kwa zenyewe au dhidi ya timu nyingine kali.

Yaani unaweza kuwaona mashabiki wamejazana kwa hatarimkatika gari wanalotumia kwenda uwanjani au wanaporejea, hali huwa mbaya zaidi kama timu yao imeshinda, maana huzidiwa na furaha hadi kujiweka katika mazingira hatari barabarani.

Katika taarifa yangu ya miaka miwili iliyopita, nilisema ni jambo la hatari kwani linahatarisha maisha yao na hata ya wengine pia. Nilichosema ndio hiki kimetokea Kenya.

Ndugu zanguni mashabiki nawasihi sana kuachana na tabia hii. Soka ni mchezo wa furaha, hivyo tunapaswa kutunza pia usalama wetu ili tuendelee kufurahi.

Nakumbuka nilipokuwa Tanzania wakati ule nikiichezea Yanga, kuna baadhi ya mechi zilichezwa Morogoro, Arusha na Dodoma. Misafara ya mashabiki ilikuwa na sura kama hii, hata kwa pale pale Dar es Salaam.

Katika hili, nawasihi wakati wowote tunaposafiri kueleka kutazama mechi, tuzingatie usalama wetu kwanza, hivi unapofanya mambo ya kukatisha uhai wako, utaendeleaje kuishabikia klabu yako?

Tuheshimu sheria zote za barabarani maana sisi wote tunamhitaji kila mmoja wetu. Ushabiki upo, tena ushabiki ni uwanjani. Barabarani ni lazima kuheshimu sheria zake.

Kuhatarisha maisha yetu kila wakati timu zetu zinaposafiri ni jambo ambalo tunafaa kuliepuka.

Hebu fikiria, vifo vya mashabiki hao vimesababisha shida gani katika familia zao. Fikiria kuhusu watoto wao na wake zao, nini kitafanyika?

Katika misafara hiyo ya mashabiki kuna wengine hutoa hadi vichwa nje gari wakati wa mwendo mkali. Kelele nyingi barabarani kiasi cha kumchanganya dereva kujua nini kinachoendelea katika gari lake.

Pia ninapenda kuwasihi viongozi wa klabu nao wawaonye mashabiki wao kuacha tabia hii. Nao maofisa wa Polisi watilie mkazo sheria za barabarani, sijui kwa Tanzania udhibiti wa Polisi ulivyo sasa, lakini kwa Kenya suala hili linahitaji mkazo zaidi.

Hebu fikiria, kutoka Nairobi hadi Nakuru ni safari ya kilomita 165. Hivi shabiki ana usalama gani wa kusafiri umbali huo akiwa juu ya gari?

Sote tunapenda soka. Tunazipenda klabu zetu na ndio maana tunazishabikia. Kweli soka lina raha yake, lakini maisha yetu ni muhimu zaidi. Furahia soka lakini kumbuka usalama wako na maslahi ya familia pia.

Ushabiki wa kuning’inia katika magari hauna maana. Vifo vinatokea nasi tunabaki kujiuliza nani wa kulaumiwa. Dereva? Polisi? Aliyeendesha gari? Au shabiki?

Unaning’inia juu ya basi, dereva akifunga breki za ghafla utafanya nini? Utajinusuruje? Safari za mashabiki ziwe kama za abiria wa kawaida kwamba kila mmoja aketi katika kiti na magari yabebe mashabiki kwa kiwango kinachoruhusiwa kisheria. Lazima tuzingatie sheria za barabarani.

Bila hivyo ushabiki wetu hautakuwa wa maana kama kazi itakuwa kuomboleza vifo tu kwa ajali za barabarani.

Kibinadamu tunajua kwamba kifo hakizuiliki, yaani kila nafsi itaonja mauti.

Lakini tuache tupatwe na vile vifo vya kupangwa na Mungu na si hivi vinavyotokana na uzembe wa wazi wazi.

Kwa huzuni kubwa, nachukua fursa hii kumuomba Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi.

Lakini pia nitumie fursa hii kuzitakia kila la heri timu za Simba na Yanga katika mechi yao ya kukata na shoka ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa mwishoni mwa wiki hii.

Zipo katika mbio za kuwania ubingwa na ushindi kwa kila mmoja wao ni muhimu.