Vichwa hivi vimekipiga Man United na Chelsea

Muktasari:

Nemanja Matic, Romelu Lukaku na Juan Mata wakali wote hao wapo kwenye kikosi cha Man United ambapo watakuwa huko Old Trafford kucheza dhidi ya waajiri wao wa zamani, Chelsea kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, ambao utakuwa na vita matata kabisa katika mchakamchaka wa kuwania kumaliza ligi ndani ya timu nne za juu.

MANCHESTER, ENGLAND. MANCHESTER United na Chelsea zitaumana jino kwa jino Old Trafford kesho Jumapili katika mchezo wa Ligi Kuu England, mechi ambayo itashuhudia baadhi ya mastaa wakicheza dhidi ya waajiri wao wa zamani.

Nemanja Matic, Romelu Lukaku na Juan Mata wakali wote hao wapo kwenye kikosi cha Man United ambapo watakuwa huko Old Trafford kucheza dhidi ya waajiri wao wa zamani, Chelsea kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, ambao utakuwa na vita matata kabisa katika mchakamchaka wa kuwania kumaliza ligi ndani ya timu nne za juu.

Hata hivyo, mastaa hao watatu si wao tu peke yao waliowahi kucheza kwenye timu hizo zote mbili kwa nyakati tofauti kwenye Ligi Kuu England.

Nemanja Matic

Kiungo mkabaji, Nemanja Matic aliichezea Chelsea katika awamu mbili tofauti, lakini awamu yake ya mwisho ilikwisha Julai mwaka jana baada ya kuondoka na kutua Old Trafford kwa ada iliyotajwa kuwa ni Pauni 40 milioni. Matic aliuzwa na Chelsea mara mbili, ya kwanza ni ile alipohusika kwenye dili la kubadilishana na David Luiz, ambapo alipelekwa Benfica na hili la pili la kutua Man United. Akiwa Chelsea, Matic alibeba mataji mawili ya Ligi Kuu England.

Mark Hughes

Hughes, ambaye kwa sasa ni kocha maarufu alianzia soka lake katika kikosi cha Man United na baada ya kuondoka hapo, alikwenda Barcelona na Bayern Munich kwa muda mfupi kati ya 1986 na 1988 na kurudi tena Old Trafford kwa ada iliyoweka rekodi wakati huo, Pauni 1.8 milioni na kubeba mataji mawili ya Ligi Kuu. Baadaye, kocha Sir Alex Ferguson akaanza kusafisha na kuamua kumuuza Hughes huko Chelsea kwa ada ya Pauni 1 milioni ambako pia alikwenda kushinda mataji mengi, si Ligi Kuu.

Juan Sebastian Veron

Mwaka 2001, Muargentina Veron alitua Man United kwa ada ya Pauni 28.1 milioni, ambayo ilikuwa rekodi kipindi hicho aliponunuliwa kutoka Lazio. Hata hivyo, Veron alidumu Old Trafford kwa misimu mwili tu na kuuzwa Chelsea kwa ada ya Pauni 15 milioni, ambako pia maisha hayakwenda kuwa mazuri huko Stamford Bridge, ambako aliishia kucheza mechi saba tu za ligi kabla ya kuanza kuandamwa na majeruhi. Aliishia kutolewa kwa mkopo tu kabla ya kuondoka jumla klabuni hapo mwaka 2007.

Romelu Lukaku

Man United imemsajili Lukaku kwa ada ya Pauni 75 milioni kutoka Everton mwaka jana, wakiwabwaga Chelsea kwenye vita ya kuwania huduma ya mshambuliaji huyo. Lakini, kabla ya hapo, Lukaku alipoingia kwenye Ligi Kuu England, timu iliyokuwa imemsajili ni Chelsea, ambapo alishindwa kuingia kwenye kikosi cha kwanza na kuishia kutolewa tu kwa mkopo kabla ya kuondoka jumla kwenda Goodison Park alikocheza soka lake la nguvu na kubamba dili la kutua Old Trafford.

Juan Mata

Fundi wa mpira Mhispaniola, Juan Mata alikuwa kipenzi cha mashabiki huko Stamford Bridge, lakini alipokuja kocha Jose Mourinho hakufiti kwenye mfumo wake na kuamua kumuuza kwenda Man United. Mata alitua Old Trafford Januari 2014 kwa ada ya Pauni 37.1 milioni, mahali ambako yupo hadi sasa akiwa chini ya kocha aliyewahi kumuuza huko nyuma, Mourinho. Akiwa Chelsea, Mata alipata mafanikio makubwa kitu ambacho atapenda sana kukifikia baada ya kutua Man United, ambako sasa amekuwa mtu muhimu kwa Mourinho.

Radamel Falcao

Mengi sana yalitarajiwa kutoka kwa Falcao wakati alipotua kwenye kikosi cha Man United kwa mkopo wenye thamani ya Pauni 6 milioni akitokea AS Monaco. Baada ya msimu mmoja, Falcao alifunga mabao manne tu kwenye Ligi Kuu na hivyo Man United kuamua kumrudisha kwenye klabu yake mama ya Monaco, ambao waliamua kumrudisha tena kwenye Ligi Kuu England na safari hii wakimpeleka Chelsea kucheza chini ya Mourinho. Mambo yalikwenda kuendelea kuwa yale yale, Falcao Ligi Kuu England haikumtaka kwani huko Stamford Bridge ndiyo alikuwa hovyo zaidi. Kwa sasa amerudi Monaco na amekuwa moto kweli kweli.

Mark Bosnich

Kipa, Bosnich alikuwa na awamu mbili katika kikosi cha Man United, lakini hakuna hata moja iliyokuwa na matokeo mazuri kwa upande wake. Aliisaidia Man United kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 1999/2000, lakini ghafla tu akaondoshwa golini na kuletwa kipa mpya. Chelsea waliamua kumsajili Januari 2001 na matatizo ya majeruhi yamemfanya ashindwe kufanya vizuri.

Nyakati zake za Stamford Bridge zilikuwa mbaya zaidi na Septemba 2002 aliondolewa kwenye timu baada ya kufeli kwenye vipimo vya dawa za kulevya.

Wachezaji wengine

Kuna orodha ya wachezaji kibao waliowahi kutupia jezi za timu hizo mbili, Man United na Chelsea na miongoni mwao alikuwapo beki Mal Donaghy, ambaye alianzia Old Trafford kabla ya kutimkia Stamford Bridge kwa ada ya Pauni 100,000. Mchezaji mwingine ni beki wa pembeni, Paul Parker, George Graham na Ray Wilkins, ambaye alianzia kuichezea Chelsea alikofanywa pia nahodha kabla ya kutimkia Man United, iliyomnasa kwa ada ya Pauni 800,000 alikobeba taji la Kombe la FA mwaka 1983.