Uzalendo ni kipimo halisi cha mchezaji

Muktasari:

Katika soka la kulipwa mchezaji anapaswa kuheshimu matakwa ya uongozi wa timu kama ambavyo mfanyakazi katika sekta rasmi anavyowajibika kwa waajiri wake kila dakika anapokua ofisini.

KWA mchezaji yeyote wa ngazi za juu za mchezo wowote anapaswa kuelewa suala la nidhamu na heshima katika kutekeleza majukumu yake ndio vitu muhimu vinavyoweza kumweka matawi ya juu.

Katika soka la kulipwa mchezaji anapaswa kuheshimu matakwa ya uongozi wa timu kama ambavyo mfanyakazi katika sekta rasmi anavyowajibika kwa waajiri wake kila dakika anapokua ofisini.

Wachezaji hasa wa Afrika wamekuwa na tabia ya kutumikia maslahi zaidi na wakati mwingine kufikia hatua ya kukataa kabisa kuziwakilisha nchi zao kwenye michuano mikubwa kwa kutoa sababu mbalimbali za kiafya.

Mfano mzuri ni tukio la hivi karibuni Mabingwa wa Kombe la Afrika 2016, Cemeroon karibu nyota wake nane walikataa wito wa kujiunga na nchi yao kwenye michuano hiyo ili tu waendelee kutumikia klabu zao.

Mastori Leo yanaturudisha mpaka mchana wa Novemba 11, 1987 katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Ulaya (Euro 1988), uliochezwa jijini Prague baina ya wenyeji Czechoslovakia (kabla ya kugawanyika) dhidi ya Wales. Straika wa nchi ya Wales, Mark Hughes wakati huo akicheza kwa mkopo katika klabu ya Bayern Munich, alicheza dakika zote 90 za mchezo huo, kisha kusafiri kwa ndege binafsi hadi Munich ambako jioni ya siku hiyo hiyo aliichezea Bavarian yaani Bayern dhidi ya Moenchengladbach katika pambano la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) akiingia kama mchezaji wa akiba.

Hata huko Marekani Juni 16, 1996, katika Uwanja cha Rose Bowl ilipangwa kufanyika michezo miwili. Mchana ulipigwa mchezo wa Ligi kati ya LA Galaxy dhidi ya Tampa Bay na usiku wake ulichezwa mchezo mwingine kati ya timu ya taifa ya Marekani dhidi ya Mexico.

Kipa wa taifa la Mexico, Jorge Campos ndiye aliyekuwa langoni wakati klabu ya LA Galaxy ikipambana na Tampa Bay na usiku wake alirejea tena uwanjani kulitumikia taifa lake. Huu ni uzalendo wa hali ya juu kwa mchezaji huyo. Kipa huyo alicheza mechi mbili ndani ya siku moja tena kwa muda mfupi, ni mchezaji gani wa Afrika anayeweza kufanya hivyo?

Wachezaji hawa kama Mark Hughes na Jorge Campos walijitoa na kuonyesha uzalendo wakati huohuo wakiheshimu kazi zao, uimara wao wa miili na akili kuweza kubadili mitazamo yao haraka kutoka pambano moja kwenda lingine.

Hiki ni kitu cha pekee na cha kuigwa na hata katika mafunzo ya nadharia ya soka (theory) bado yanahitajika sana hapa nyumbani na Afrika kuwajenga wachezaji.