Usajili ulivyosepa na nafasi zao Stars

Muktasari:

  • Hata hivyo, wapo ambao wamefanikiwa kuendelea kuichezea Stars baada ya kusajiliwa na timu hizo kutokana na kufanya vyema na wengine wamechemka kwa sababu ya kutozichanga vyema karata zao.

ILIKUWA kama mazoea, kila timu ya Taifa. Taifa Stars inapoitwa, wachezaji wengi hutokea timu za Simba, Yanga na Azam FC na wachache sana wanaofanya vizuri kutoka klabu nyingine nje ya hizo.

Hata hivyo, wapo ambao wamefanikiwa kuendelea kuichezea Stars baada ya kusajiliwa na timu hizo kutokana na kufanya vyema na wengine wamechemka kwa sababu ya kutozichanga vyema karata zao.

MOHAMED IBRAHIM-

SIMBA

Alitokea Mtibwa Sugar kabla ya kutua Simba. Huko Mtibwa alikuwa tishio na tegemeo akicheza kwa kiwango bora kabisa. Anaujua mpira na ni fundi na alizitesa kweli timu pinzani ikiwamo hiyo Simba. Haikuwa ajabu kwa Kocha Mkuu wa Taifa kipindi hicho, Salum Mayanga kumwita kwenye kikosi cha Stars.

Hata hivyo, tangu atue Simba kulikojaa nyota wengi, tabia zake ndogo ndogo na utovu wa nidhamu alizoonyesha, zilianza kumwondoa taratibu kwenye kikosi cha kwanza na hivyo kuwafanya makocha wa timu ya Taifa kutomjumuisha tena.

JUMA MAHADHI- yanga

Akiwa Coastal Union ya Tanga, alikuwa kwenye kiwango kizuri na alihusika kikamilifu kuzisulubu vigogo vya Azam, Simba na Yanga pale Uwanja wa Mkwakwani akicheza vizuri nafasi ya winga mshambuliaji.

Haikuwa ajabu sana kwa Yanga kuamua kumsajili na bahati aliikuta Yanga ikiwa kwenye michuano ya kimataifa.

Mechi yake ya kwanza tu akikutana na TP Mazembe Uwanja wa Taifa na alifanikiwa kukoga mioyo ya Wanayanga.

Kasi yake na mashuti ndiyo vilivyomshawishi Kocha wa Taifa Stars wa wakati huo, Charles Boniface Mkwasa kumwita kikosini mwaka 2016 na angalau alikaa akiangalia wenzake wanafanya nini.

Hata hivyo, Mahadhi wa sasa sio yule tena, kiwango kimeshuka ghafla na haikushangazi kuona akiachwa kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga na kuacha kuitwa kikosi cha Taifa Stars.

SALMIN IDD HOZA- AZAM

Kama kuna watu walioisimamisha Mbao FC ya jijini Mwanza kuwa imara ni huyu jamaa. Akishirikiana na wenzake waliifanya Mbao kuwa tishio Ligi Kuu msimu wa kwanza tu na kila aliyekutana nayo alijuta hasa ikiwa uwanja wake wa nyumbani, CCM Kirumba.

Akitumia mguu wake wa kushoto, Hozza alikuwa kwenye kiwango bora na haikushangaza kuona akiwaniwa na klabu kubwa kabla ya AzamFC kufanikiwa kumnasa huku pia Kocha wa Stars, Mayanga akimwita Stars.

Kitendo cha kusajiliwa Azam na kuwakuta nyota wa nafasi ya kiungo kulimpunguzia muda mwingi wa kucheza na hivyo taratibu kiwango chake kikashuka na kushindwa kuitwa tena Stars.

RAPHAEL DAUDI- YANGA

Pale Mbeya City alikuwa na pacha wake, Kenny Ally. Unaambiwa waliwasha moto wa hatari na katika nafasi ya kiungo na kufunga mabao mengi huku Daudi akiwa mchezaji wa nafasi hiyo aliyefunga mabao mengi zaidi.

Kutokana na kiwango chake, Yanga walipambana na kuwahi saini yake msimu wa 2017/18, pia aliitwa kikosi cha Stars cha Kocha Salum Mayanga na kumjumuisha kwenye safari ya michuano ya Cosafa nchini Afrika kusini.

Hata hivyo, pale Yanga alikuwa akitumika kama mshambuliaji namba mbili nyuma ya mshambuliaji mkuu, nafasi iliyompa tabu, akicheza leo vizuri, kesho anachemsha, hali iliyomfanya kushuka kiwango.

Ni wazi kama angeendelea kubaki Mbeya City, leo hii asingekosa nafasi ndani ya Stars.

ADAM SALAMBA - SIMBA

Huyu hakusubiri asajiliwe na timu kubwa ndio apate nafasi ya kuitwa Stars. Alikuwa Lipuli FC lakini kwa kiwango alichokuwa nacho, nguvu na aina ya uchezaji, ni wazi hakuhitaji kupitia timu kubwa Kuitwa Stas. Alionwa huko huko Lipuli na kutua Stars. Alizisumbua sana timu kubwa za Ligi Kuu kama mshambuliaji wa kati.

Kwa sasa yuko Simba alikosajiliwa msimu huu na bila shaka kiwango alicho nacho kingetosha kumpeleka timu ya Taifa.

Hata hivyo, kutokana na kuingia kwenye kikosi kilichosheheni wachezaji wengi bora wa eneo lake, tena bora wanaotoka nje ya nchi, kumeifanya nafasi yake kuwa finyu sana.

Iwapo tu angekuwa na jicho la pili kuangalia wapi angeenda kupata nafasi ya kucheza muda mwingi, ni wazi leo hii angekuwa ameitwa timu ya Taifa.

ELIAS MAGULI - AS KIGALI

Jamaa kazurura timu kibao kabla ya sasa kwenda Kigali Rwanda kujiunga na AS Kigali.

Ni mmoja wa washambuliaji wenye umbo la kiuchezaji linalokubalika. Alicheza vizuri Simba kisha baadaye akaenda nje ya nchi kusakata soka la kulipwa kabla ya kurudi na kuzunguka timu kibao

Kama unakumbuka, Maguli alionyesha kiwango safi kwenye mechi ya kimataifa dhidi ya Morocco na kufunga bao zuri.

Hata hivyo, kwa sasa ni kama ameisahau Stars kutokana kutojumuishwa kwenye kikosi hicho kilichocheza jana na Uganda kwenye Michuano ya kuwania kufuzu fainali za Afcon.

Unaweza kusema ni mmoja kati ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi walikosekana katika kikosi cha Taifa na hii ni kutokana na aina ya ligi anayocheza.

MBARAKA YUSUF - AZAM

Kama kuna mshambuliaji ambaye alisababisha Simba wakalala na viatu misimu miwili iliyopita, basi ni huyu.

Simba hawatakaa wamsahau. Unajua kwa nini? Ndiye aliyezima ndoto za Simba kukaribia ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2016/17 kwa bao lake lililoipa timu yake ya Kagera Sugar pointi tatu.

Ni mshambuliaji hatari na anajua kuliona goli.

Katika dirisha kubwa la usajili mwaka juzi, Mbaraka Yussuf alikuwa gumzo na kiwango chake, kikimshawishi hadi Kocha Mkuu wa Taifa Stars wa kipindi hicho Charles Bonifas kumjumuisha kwenye kikosi chakes na alifanikiwa kucheza na kuifungia Stars bao zuri kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi.

Kitendo cha kusajiliwa na Azam FC ukiachana na majeraha yake ya muda mrefu, pia matumizi yake ndani ya kikosi hicho pamoja na wachezaji waliomzunguka ni wazi kumemfanya ashuke kiasi kiwango cha uchezaji wake na kushindwa kuitwa Stars.