NINACHOKIAMINI: Unabet? Yanga inaweza kusonga mbele, Simba hapana

Tuesday March 13 2018

 

HUWA siamini sana katika kitu kinaitwa ‘bahati. Kila kinachotokea katika maisha huwa ni mipango ambayo mtu amejiwekea.

Huwezi kuwa tajiri ukasema ni kwa sababu ya ‘bahati’. Kama umepata kitu kwa sababu ya kuwa na ‘bahati’ hakiwezi kudumu.

Jambo ambalo linafanywa kwa mipango na mikakati huwa linadumu zaidi kuliko kitu ambacho kinapatikana ‘kibahatibahati’.

Simba na Yanga zinashiriki mashindano ya Afrika ambayo yanaandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Zimekuwa hazifanyi vizuri sana, na hata pale zinapofurukuta huwa ni ‘bahati’ ambayo nimesema huwa siamini sana.

Hata hivyo, unaweza kuamini kwamba ni ‘bahati’ kwa sababu ushindi wenyewe huwa haudumu sana. Ni timu ambazo huwa hazifiki mbali sana.

Ukiondoa mafanikio ya Simba ya mwaka 1993 na 2003 na yale ya Yanga ya mwaka 1998 hakuna mafanikio makubwa kutoka katika timu hizo ndani ya miaka 30 iliyopita.

Huhitaji kutumia nguvu kujua hilo, ni wiki hii tu unaweza kujua ninachomaanisha kwa sababu Yanga na Simba zitakuwa ugenini kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Yanga wanahitaji kuifunga Township Rollers ya Botswana kwa mabao 2-0 ili kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo uliopita jijini Dar es Salaam, Yanga walifungwa mabao 2-1 na hivyo wanahitaji kushinda 2-0 mjini Gaborone au washinde mabao 2-1 ili kuruhusu penalti.

Simba wanahitaji kushinda 1-0 dhidi ya Al Masry watakaporudiana nchini Misri katika Kombe la Shirikisho.

Timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 jijini Dar es Salaam, kwa hiyo kwa Simba kusonga mbele wanahitaji kushinda angalau bao 1-0.

Tatizo kubwa kwa mashabiki wengi, wanadhani Yanga ina wakati mgumu kuliko Simba. Ni kweli Yanga wanahitaji kushinda 2-0, Simba wanatakiwa kushinda 1-0. Lakini hali ni tofauti.

Kwa mtazamo wangu baada ya kuona mechi za Dar es Salaam, naona Yanga ikiwa na nafasi kubwa ya kusonga mbele kuliko Simba.

Licha ya kiwango kizuri cha Township, bado inapitika na wachezaji wake wanafanya makosa ya kujisahau kiasi kwamba Yanga wanaweza kusonga mbele wakiwa makini katika mchezo huo wa Jumamosi ijayo.

Township ni timu nzuri sana, ina vijana wengi wanaojua mpira, hata hivyo, wana udhaifu pia katika ukabaji, wanafunguka na kuacha nafasi kwa timu pinzani kucheza inavyotaka jambo ambalo ni hatari na hasa mpinzani akiwa makini.

Licha ya uzuri wote wa Township, wachezaji wake wengi ni chipukizi, hawana uzoefu na wanakosa nidhamu.

Hawaheshimu timu pinzani kama walivyofanya Dar es Salaam, ambako Yanga walishindwa kutumia nafasi hiyo ya kutoheshimiwa nyumbani.

Yanga wakienda Botswana na dhamira ya kweli, wanaweza kushinda zaidi ya mabao mawili na kusonga mbele bila wasiwasi.

Tofauti na watu wengine, licha ya Simba kuhitaji ushindi wa bao 1-0, naona wakiwa na mlima mrefu wa kupanda kuliko Yanga.

Niliwaangalia Al Masry ni timu ambayo imekamilika na inaweza kucheza aina yoyote ya mchezo kutokana na mpinzani alivyojipanga.

Mabeki wao wametulia na wanaweza kuanzisha mashambulizi ya haraka, huku viungo wao wakiwa tayari kuchukua mipira ya nyuma na kuunganisha na washambuliaji wenye uwezo wa kukimbia kushoto na kulia kwa ajili ya kuwavuruga mabeki wa timu pinzani.

Kwa jumla, Al Masry wamekamilika zaidi na hata wakati mwingine Simba wanastahili pongezi kwa sare ya mabao 2-2.

Tuwaache makocha wa Simba na Yanga wafanye kazi yao vizuri bila kuwaingilia, kwa sababu kinachoendelea sasa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ni kama kuingilia ufundi wa makocha hao.

Wao ndio wanakaa na wachezaji, wanakuwa nao mazoezini, wanajua udhaifu na ubora wa kila mmoja, hivyo tuwaache wafanye kazi yao na wapange kikosi kwa mitazamo yao.

Tunachopaswa kufanya kwa sasa ni kusubiria matokeo ya michezo hiyo kwa jinsi makocha hao walivyowaandaa wachezaji wao kutokana na mipango yao.

Hata hivyo, kama ningelazimishwa nichague timu ambayo nadhani itasonga mbele, nahisi ningeitaja Yanga kuliko Simba. Samahani kwa hilo.