Ukishangaa ya Ajib unakutana na ya Haruna Niyonzima

Tuesday June 20 2017

 

By Edo Kumwembe

TUNAKOSA vitu vingi katika mpira wetu. Tunakosa akili, tunakosa pesa, tunakosa maarifa.

Ukishamaliza kushangaa ya Ibrahim Ajib kwenda Yanga, sasa unaweza kushangaa ya Haruna Niyonzima kwenda Simba, hata kama mpaka sasa naandika makala hii uhamisho wake kwenda Simba ulikuwa haujakamilika.

Unaanza kwa Ajib. Sio kwamba Simba hawakumtaka Ajib kama walivyokuja kusema baadaye, hapana, walimtaka. Wameumia Ajib kwenda Yanga. Kuna wengine wamelia. Kuna rafiki yangu wa karibu amelia huku kakunja ngumi.

Simba walianza harakati za kumbakisha Ajib dakika za mwisho. Sijui walikuwa wapi? Hata hivyo, kuna wakati inabidi uwasikilize watu wa Simba ambao walikuwa wanadai kwamba Ajib ni mtovu wa nidhamu na amewasumbua sana.

Nadhani walipaswa kutangaza kutokuwa naye wakati mkataba wake umebakiza miezi sita au mara tu ligi ilipoisha. Tunahitaji kuondoa nguvu kutoka kwa viongozi kwenda kwa kocha au Mkurugenzi wa Ufundi wa timu, nafasi ambayo nadhani kwa sasa inahitajika kwa Simba na Yanga.

Kocha wa Simba, Joseph Omog angetoa msimamo wake mapema kuhusu Ajib. Kama alikuwa hamtaki Simba isingeweza kuwaweka roho juu mashabiki wake. ingetangaza mapema kuachana na Ajib. Kama walikuwa wanamhitaji, basi wangeanza mpango wa mapema kumbakisha Ajib miezi sita kabla ya kumalizika kwa mkataba wake.

Kuwaweka mashabiki roho juu mpaka dakika za mwisho ni usumbufu usio na sababu kwa mashabiki. Ni usumbufu ambao unavinufaisha vyombo vya habari kwa sababu vinauza magazeti, lakini kwa mashabiki ni kero isiyo na sababu.

AC Milan imetangaza mapema kwamba kipa wao tegemeo, Gianluigi Donnarumma hatasaini mkataba mpya klabuni hapo, ingawa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja. Ni ukweli unaouma lakini ndio hali halisi. Simba iliwaweka roho juu mashabiki wake katika hili la Ajib bila ya sababu za msingi sana.

Nenda kwa Yanga sasa. Hadi jana walikuwa wanahaha na mchezaji wao, Haruna Niyonzima. Unahaha vipi na mchezaji ambaye amemaliza mkataba wake? Ulikuwa wapi kuweka msimamo wako kwa mchezaji aliyelala kambini kwako msimu mzima wa ligi?

Haruna alipaswa kuwa na mkataba wa Yanga mkononi miezi sita iliyopita. Kinachoshangaza kuna mabosi wa Yanga wamegawanyika kuhusu Haruna. Kuna ambao wanamtaka na kuna ambao hawamtaki. Hapo hapo hatujui kocha wake, George Lwandamina anasemaje au aliacha maagizo gani kuhusu kiungo huyo.

Matatizo yaliyopo kuhusu Haruna ni yale yale yaliyopo kuhusu Ajib. Kwanza kabisa ni kwamba klabu hizi hazina pesa. Zinategemea mfuko wa mfadhili tu. Kama mambo yalienda kombo kama ambavyo Mwenyekiti wa Yanga alipitiwa na upepo mbaya basi maisha yanakuwa ya shida tu.

Kama Yanga ingekuwa na pesa zao katika akaunti, basi wangekuwa wamemalizana na Haruna miezi mingi kabla ya mkataba wake kumalizika. Tatizo hilo litaendelea kwa miaka mingi ijayo kadiri klabu zetu zinavyoendekeza masuala ya wafadhili kuliko wadhamini.

Lakini pia tatizo jingine la Ajib na Haruna ni hilo nililogusia juu. Makocha hawana nguvu za maamuzi katika masuala la uhamisho wa wachezaji wanaoondoka na kuingia. Mpaka tunafika dakika ya mwisho hatujui kama Ajib na Haruna wanahitajika na makocha wao au vinginevyo.

Viongozi wa klabu wanapogawanyika, basi hatma za wachezaji zinakuwa ngumu mpaka siku ya mwisho. Kama kocha angekuwa anaachia madaraka yake, sidhani kama angekubali masuala haya yaende mpaka siku ya mwisho. Miezi sita kabla angesema wazi kwamba hamtaki Ajib au Haruna.

Mwisho wa siku bado tunaendesha mpira wetu kiswahili sana. Katika dunia halisi hauwezi kupambana kumbakisha mchezaji wako aliyekuwa analala kambini kwako mpaka mkataba wako unaisha. Lazima klabu ijue nafasi yake kwa mchezaji na mchezaji mwenyewe ajue nafasi yake kwa klabu.

Kuna mambo makubwa hatuwezi kuiga kutoka Ulaya kwa urahisi kama vile klabu kubwa na uwanja wa kifahari kama Old Trafford, lakini haya mengine ni ya kawaida kabisa na yanahitaji akili ya kawaida kabisa. Tunahitaji kuiga vitu vya kawaida kabisa katika kuendesha soka. Lakini pia tunahitaji kuanza kununua wachezaji kwa kutumia akaunti za klabu sio wafadhili.