UCHAMBUZI: Uenyeji wa Kombe la Dunia ni habari nyingine

Muktasari:

  • Fainali hizo zina manufaa yake kiuchumi na kijamii kwa mataifa yote kuanzia yake yanayoshiriki hadi yale yanayoandaa fainali hizo.

WIKI iliyopita tulianza kuona umuhimu na ukubwa wa fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea kule Urusi.

Fainali hizo zina manufaa yake kiuchumi na kijamii kwa mataifa yote kuanzia yake yanayoshiriki hadi yale yanayoandaa fainali hizo.

Ndio maana hata utaratibu uliokuwa ukitumika miaka ya nyuma kupata mwenyezi wa fainali hizi umebadilika.

Kwa miaka ya nyuma ilikuwa wajumbe wachache tu kutoka Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Soka duniani (Fifa) ndio waliokuwa wakikutana ili kuamua nchi gani itakayoandaa fainali za mwaka fulani.

Lakini baada ya Gianni Infantino kuchaguliwa kuwa rais wa shirikisho hilo na kuona umuhimu na ukubwa wa mashindanbo haya, utaratibu huo umebadilishwa ndio maana kabla yafainali za Kombe la Dunia za mwaka huu kuanza kule Urusi, tulishuhudia mataifa wanachama yakishiriki katika zoezi la kupiga kura ili kupata nchi itakayoandaa fainali za Fifa za Kombe la Dunia za mwaka 2026.

Katika zoezi hilo nchi za Marekani, Canada na Mexico zimepata fursa hiyo adimu kabisa. Kumbuka kuwa nchi hizo ambazo zitandaa kwa pamoja zilikuwa zikishindana na Morocco.

Lakini kwa uamuzi wa nguvu ya wengi, wapiga kura waliamua kuinyuma fursa hiyo nchi hiyo ya Afrika.

Ukubwa wa mashindano haya ndio umesababisha leo hii kila mtu aliyepo maeneo ya mijini na hata vijijini katika mazungumzo anayofanya kwa siku moja, hawezi kuacha kutaja jina la nchi ya Urusi.

Kwani kinachoendela nchini humo kwa sasa kinafuatiliwa na zaidi ya robo tatu ya wakazi wa dunia ndio maana kwa Lugha ya Kiingereza wanasema ‘Russia is a talk of the town.’

Leo hii tuangalie faida za kuichumi na kijamii ambazo nchi inayoandaa michuano hii inanufaika nazo .

Kuna faida nyingi ambazo huzifanya nchi kadhaa kutaka kupata fursa hii hata kama hazina uwezo. Ndio maana kuna wakati ilidaiwa kuwa baadhi ya nchi zilikuwa zikitumia ushawishi mkubwa kupata frusa hiyo ya kuandaa fainali hizi.

Kama hatoshi suala la rushwa lilitajwa kuhusika ili kuweza kuwashawishi wajumbe wachache waliokuwa wakisimamia zoezi hilo. Hata hivyo kuchaguluwa kwa Infantino kumeondoa hali hiyo.

Mbali na faida za kiuchumi na kijamii lakini pia kuna faida nyingine ambazo hupatikana kutokana na nchi moja au zaidi kushirikiana kuandaa fainali hizo.

Kama mwaka 2002 Japan na Korea Kusini ziliandaa kwa pamoja na Marekani, Canada na Mexico zitakapoandaa fainali za mwaka 2026.

Binafsi nakumbuka kabla ya fainali hizi zinazoendela kule Urusi kuanza, mwishoni mwa Aprili 2018 Mwenyekiti wa Kamati ya Ndani ya Maandalizi ya fainali hizo ambaye ni Waziri Mkuu wa Urusi , Arkady Dvorkovich aliwasilisha taarifa ya maandalizi na kutaja faida ambazo nchi yake ilizonufaika nazo kiuchumi, kijamii na katika eneo la utunzaji wa mazingira kutokana na kuandaa fainali hizi za Kombe la Dunia.

Moja kati ya eneo alilolitaja kuwa nchi yake imenufaina nalo ni ongezeko la taaluma ya uandaaji wa matukio makubwa kama haya ambapo idadi ya Warusi wapatao 210,000 ilibidi waongezewe ujuzi na maarifa katika elimu ya mapokezi.

Warusi wengine wanaokadiriwa kufikia 38,000 wakiongezewa ujuzi katika eneo la uungwana (Hospitality) na utoaji wa huduma za vyakula (Catering).

Na kama vile haitoshi, zaidi ya Warusi 18,000 wameongezewa ujuzi katika sekta ya mawasiliano na usafirishaji na wengine zaidi ya 5,000 wakiongezewa ujuzi katika eneo la mpangilio wa matukio (Tournament Organiation).

Bado kuna Warusi wengine zaidi ya 52,000 wamepewa mafunzo ya kujitolea kufanya shughuli mbalimbali za kuwahudumia wageni ambao waliofika Urusi kwa ajili ya kushuhudia fanili hizo moja kwa moja viwanjani.

Wakati ukiangalia hayo bado kuna suala la ajira kwa Warusi zaidi ya 10,000 katika suala la ujenzi wa viwanja vinavyoendelea kutumika katika fainali hizo. Kama utaangalia kwa undani utabaini kwamba maandalizi ya fainali hizo yana faida kubwa kwa nchi inayoandaa. Ndio maana nchi zimekuwa zikipigana vikumbo kushindana kwa kila hali na mali kuweza kupata fursa hiyo.

Kwa leo naomba kuishia hapo huku huku nikisubiri mrejesho kutoka kwenu, sehemu ya tatu ya makala hii itaendelea wiki ijayo !