Tunapojidanganya tutajifunza kitu Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Wengi watajidanganya tutajifunza kitu Russia. Uongo. Russia zinakutana timu kubwa za mataifa ya mbalimbali zikiwa katika kilele cha maandalizi ya muda mrefu ya mpira. Hazikufika Russia kwa kubahatisha kwa usiku mmoja tu.

SIAMINI katika miujiza. Naamini katika ukweli. Tatizo Watanzania wengi wanaamini katika miujiza. Haiwezekani. Miujiuza ilipita zama za Yesu na mitume wengine. Tupo katika zama za uhalisia. Hakuna kitu cha maana cha kujifunza katika michuano ya Kombe la Dunia pale Russia.

Wengi watajidanganya tutajifunza kitu Russia. Uongo. Russia zinakutana timu kubwa za mataifa ya mbalimbali zikiwa katika kilele cha maandalizi ya muda mrefu ya mpira. Hazikufika Russia kwa kubahatisha kwa usiku mmoja tu.

Tuna maeneo yetu ya kuanza kujifunza na siyo Russia. Kama kuna timu ya ukanda huu inakaribia kufuzu Kombe la Dunia au inaweza kunusa michuano hiyo, basi ni Uganda.

Tumejifunza nini kutoka kwa Waganda? Mpaka leo hakuna tulichojifunza. Kwanini tusianze kwa Waganda kwanza.

Katika nchi zote ambazo ambazo zimekwenda Russia, ni Saudi Arabia na England tu ambazo zinatumia wachezaji wanaocheza nyumbani tu.

Tunaweza kuitumia ligi yetu kwenda Russia. Uongo? Waarabu wa Saudia na Wazungu wa England wamewekeza katika ligi zao. Sisi ligi yetu ina nini?

Kabla ya kufikiria habari za Kombe la Dunia tujiulize tunaifikiaje Afcon.

Mara ya mwisho tulifika mwaka 1980. Miaka 38 iliyopita. Tunahitaji kwenda kushiriki tu na wala sio kushinda. Kama ni kushinda basi kikosi cha Zambia kilichotwaa ubingwa wa Afrika 2012 kilikuwa na wachezaji wachache wanaocheza Ligi Kuu ya Zambia. Wengi walikuwa wanatoka nje ya mipaka yao ingawa si Ulaya.

Katika kila eneo hatupaswi kulifikiria Kombe la Dunia kama sehemu ya mafunzo.

Tunapaswa kuifikiria michuano ya Chan, Afcon kama sehemu ya kujifunza kitu. Kombe la Dunia ni mbali sana.

Tanzania inaweza kwenda au kujifunza kabla ya Zambia haijafanya hivyo? Zambia ambayo tunaiona inacheza na Ghana, Nigeria, Mali, Senegal na wengineo huku ikiwa inashindana.

Siye tuangalie Kombe la Dunia kama burudani tu inayofurahisha macho na kukonga moyo. Kisha tukakae vijiweni na kuanza kusimuliana kile tulichokiona katika fainali hizo.

Hebu jiulize ni wakati gani tuliweza kuheshimu vipaji vijana wetu? Kama timu kubwa nchini hazina viwanja vya mazoezi tunataka kwenda Kombe la Dunia kufanya nini?

Au tutatazama Kombe la Dunia tukijifunza nini? Kama Simba na Yanga zimeshindwa kujifunza ya Chamazi pale nyumbani kwa Azam tutajifunza nini Kombe la Dunia?

Kama tunashindwa kuwa na makocha wazawa wenye viwango tunataka kujifunza nini kwenye fainali za Kombe la Dunia?

Ajabu! Makocha takribani wote wa Ligi Kuu wenye nguvu wanatoka nje ya nchi. Mbaya zaidi hata wale wa timu zinazogombea kushuka daraja sio wazawa. Hatuna makocha tutajifunza nini Kombe la Dunia?

Ujumbe upo wazi. Kombe la Dunia ni dunia nyingine. Kabla hatujafikiria kujifunza lolote katika Kombe la Dunia tuwe bize kidogo kujifunza kutoka kwa majirani kama Zambia na Uganda ambao huwa wanajaribu kutuonyesha njia. Huwa wanafanya nini kujaribu kushindana na wakubwa?

Kuamini kama tunaweza kujifunza kitu katika Kombe la Dunia kuanzia katika vitu kama aina ya mpira unaochezwa, maandalizi ya michuano yenyewe, uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, ni mambo ya kujidanganya kwa sasa.

Kuna kiwango inabidi tukifikie kabla ya kufikiria huko.

Unapopita katika viwanja vya Shule ya Msingi pale Johannesburg Afrika Kusini na kukuta shule ina viwanja vinne safi ambavyo vinamwagiliwa vema na kutunzwa vema kama uwanja wetu mkubwa wa Taifa ndipo unapogundua kuwa tuna safari ndefu.

Hasa unapofungiliwa Azam TV na kutazama mechi za ligi katika viwanja vya Njombe Mji au Majimaji Songea. Kama tunajidanganya kuwa tutajifunza kitu kipitia Kombe la Dunia tunajidanganya. Sidhani kama tutakuwa tunafikiria kwa kutumia akili sahihi za kibinaadamu.

Tutakuwa tunaamini katika miujiza. Tena miujiza ya kuamini jiwe linaweza kugeuzwa kuwa mkate.Tutakuwa tunazidanyanya nfasi yetu kwa mambo yasiyowezekana.

Tuurudishe mpira katika misingi yake kisha tuanze kuota ndoto za taratibu. Tukimaliza ndoto moja tuhamie katika ndoto nyingine.

Klabu zetu zipo hoi, ligi yetu ipo hoi, wachezaji wetu wengi wa timu ya taifa wanacheza ndani. Tunawazaje kuiga mambo yatakayoanza keshokutwa Russia. Kama si kujidanganya ni nini?