MAONI: Tunaamini wawakilishi wetu wa Afrika, hamtatuangusha ugenini

Muktasari:

Timu hizo nne mbili kutoka Tanzania Bara na nyingine za visiwani Zanzibar siku kumi zilizopita zilikuwa nyumbani na kucheza mechi zao za mkondo wa kwanza za raundi ya awali na wageni na kupata matokeo ya kuridhisha kiasi chake.

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Simba, Yanga, Zimamoto na JKU wapo ugenini kwa ajili ya kucheza mechi zao za marudiano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Timu hizo nne mbili kutoka Tanzania Bara na nyingine za visiwani Zanzibar siku kumi zilizopita zilikuwa nyumbani na kucheza mechi zao za mkondo wa kwanza za raundi ya awali na wageni na kupata matokeo ya kuridhisha kiasi chake.

Ndio tunasema ya kiasi chake kwa sababu Yanga ilipata ushindi kiduchu cha bao 1-0 dhidi ya Washelisheli, St Louis, wakati JKU na Zimamoto zililazimishwa sare na Zesco United ya Zambia na Welayta Dicha ya Ethiopia.

Ni Simba pekee ambayo ilianza kwa kishindo michuano hiyo ya Afrika inayoishiriki tena tangu mwaka 2013 baada ya kuifumua Gendermarie National ya Djibout kwa mabao 4-0.

Matokeo ya mechi za awali kwa kiasi kikubwa zinazipa nafasi finyu Zimamoto iliyotoka sare ya 1-1 na Welayta Dicha, JKU ilitoka suluhu na Zesco na hata Yanga iliyoshinda 1-0 kwani zitalazimika kupata ushindi ugenini ama sare zitakazowavusha raundi ya kwanza ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi za klabu.

Simba sare yoyote kwao ni faida na kwa aina ya soka waliocheza Gendermari ni wazi ni timu inayojijenga kupata uzoefu katika soka la Afrika, tofauti na Simba ambao ni wazoefu wa michuano hiyo hata kama haikushiriki kwa muda mrefu.

Mwanaspoti linaziombea kila la heri timu hizo nne katika mechi zao zitakazochezwa kuanzia leo Jumanne na kukamilishwa kesho Jumatano ili zipate matokeo mazuri na kusonga mbele.

Kitu muhimu kwa wawakilishi wetu ni kushuka kwenye viwanja hivyo vya ugenini wakitambua Watanzania wapo nyuma yao katika dua kuhakikisha wanafanya vyema na wajibu wao ni wachezaji wa timu hizo kujitoa kusaka matokeo mazuri.

Rekodi za timu za Tanzania katika michuano ya CAF hazivutii, lakini bado zina kila sababu ya kupambana kusaka matokeo mazuri kwa nia ya kujiweka katika nafasi nzuri za kusonga mbele katika michuano hiyo.

Klabu zetu lazima zitambue kuwa, kusonga mbele kwenye michuano hiyo kutazipa nafasi ya kuyasogelea mamilioni ya fedha za zawadi zinazotolewa na wadhamini wa CAF ambazo ni fedha nyingine zinazoweza kuzifanya zijiendeshe kitajiri.

Tunaamini timu zetu zina uwezo mkubwa wa kupata matokeo mazuri licha ya kucheza ugenini kwa sababu soka ni mipango na kujitoa uwanjani kwa wachezaji, hivyo hata wao wakiamua wataweza kuwafurahisha mashabiki wa soka nchini.

Michuano ya kimataifa hutoa nafasi nzuri ya kuwatangaza wanasoka wetu nje ya nchi na kuonwa na mawakala wa kimataifa na mwishowe kuingia sokoni.

Simon Msuva, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Mrisho Ngassa na hata Abdi Banda walionwa kupitia mechi za kimataifa iwe na klabu zao ama timu ya taifa, Taifa Stars, kuonyesha mechi za kimataifa zina faida kubwa kama zitatumiwa vyema.

Hivyo wachezaji wa klabu zote nne wanapaswa kujituma na kujitoa uwanjani kusaidia kuzipa matokeo mazuri klabu zao sambamba na kujitangaza ili kujiweka sokoni kwa soka la kimataifa.

Wachezaji wasishuke uwanjani kwa kuzidharau timu pinzani kwa matokeo ya awali, timu pinzani zinapocheza ugenini mara nyingi huwa zinaficha makucha na kupenda kulazimisha sare, hivyo wawakilishi wetu wachukue tahadhari mapema.

Pia wachezaji waepuke kuwa na hamaki ama kulumbana na waamuzi kwani vitendo hivyo vinaweza kuwatoa mchezoni na kuziponza timu zao na kujikuta zikitolewa michuanoni.

Wachezaji wacheze kwa tahadhari, wawajibike kusaka matokeo na wasikubali kirahisi kuondolewa mchezo na maamuzi ya waamuzi ama hila za timu pinzani kwa sababu ni utamaduni uliozoeleka kwa timu zilizopo nyumbani kutumia faida ya uenyeji kulazimisha matokeo.

Tunaamini makocha na viongozi walishawaandaa wachezaji wao mapema kwa ajili ya kuhimili vishindo vya mechi hizo za ugenini na wadau wa soka wajiandae tu kuyapokea matokeo mazuri kwa mechi hizo za leo na kesho katika michuano hiyo.

Mwanaspoti linawatakia kila la heri wawakilishi wetu, Simba, Yanga, Zimamoto na JKU kwa mechi zao za marudiano ili kuweza kupenya hatua hiyo na kurejesha heshima ya soka la Tanzania.

Tunaamini jambo hilo linawezekana.