MAONI YA MHARIRI: Tumevuna tulichopanda, tujipange kivingine

Friday August 11 2017

 

By MWANASPOTI

TANZANIA imeaga mashindano ya Riadha ya Dunia yanayoendelea jijini London, Uingereza baada ya wanariadha wake, Emmanuel Giniki na Gabriel Gerrard kushindwa kufurukuta katika mbio za mita 5000.

Ilikuwa ni bahati mbaya kwa Giniki, kwani alionekana wazi angerejea na medali kama sio kuumia mguu wake wa kulia na kusababisha kupoteza uelekeo na kumaliza nafasi ya 13 akishindwa kufuzu fainali za mbio za mita 5,000.

Mwanariadha mwenzake, Gabriel Gerrard alishindwa kuanza kabisa mbio hizo za mita 5,000 na kufanya Tanzania ipoteze tumaini la kuiongezea medali baada ya ile ya Alphonce Simbu, aliyenyakua medali ya shaba katika mbio marathoni.

Tanzania ilituma wawakilishi wake wanane katika mbio hizo za dunia na tumaini kubwa lilikuwa kwa Simbu na Giniki, ambao kwa yamkini waliipigania nchi ila basi tu.

Medali ya Shaba ya Simbu ni ya kwanza kwa Tanzania tangu Christopher Isengwe alipotwaa medali ya fedha miaka 12 iliyopita katika mashindano ya mwaka 2005 yaliyofanyika mjini Helsinki, Finland.

Katika mashindano hayo ya mwaka 2005 Tanzania ilishuhudia pia mwanariadha wake, Samson Ramadhan akimaliza katika nafasi ya tano, akizidiwa kidogo na Wajapan wawili waliomtangulia mbele yake.

Hivyo, kwa miaka 34 ya mashindano hayo ya riadha ya dunia, Tanzania imevuna medali mbili tu, japo kila msimu wa kufanyika kwake tumekuwa tukipeleka wanariadha ambao, mwishowe wamekuwa wakirudi mikono mitupu huku wakiwa na lundo la utetezi.

Mwanaspoti kama wadau wa michezo linawapongeza wawakilishi wetu walishiriki mashindano ya mwaka huu na tunazitoa pongezi za dhati kwa Alphonce Simbu kwa kuiifuta machozi Tanzania na kurudi na medali ya shaba kwani, haikuwa kazi rahisi kabisa.

Kadhalika tunampa pole Giniki kwa kushindwa kufanikisha ndoto zake za kuiletea Tanzania medali kupitia mashindano hayo kutokana na kupata majeraha akiwa kazini na tunamtakia kila la heri aweze kupona haraka mguu wake na kuendeleza mapambano.

Hata hivyo, pongezi za dhati ziende kwa uongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) ambao, tangu uingie madarakani mwishoni mwa mwaka jana, umejitahidi kuonyesha tofauti kubwa kati yao na uongozi uliopita.

Tunaamini kilichotokea kule London ni muendelezo wa moto uliowashwa kwenye mashindano ya dunia ya Mbio za Nyika zilizofanyika Kampala, Uganda na utaendelezwa kwenye mashindano mengine makubwa yaliyopo mbele yetu.

Mwaka mmoja ujao itafanyika Michezo ya Jumuiya ya Madola kule Australia, kabla ya miezi michache baadaye kuwepo kwa Michezo ya Afrika (All Africa Games) itakayofanyika kule Guinea ya Ikweta kisha kufanyika kwa Michezo ya Olimpiki 2020.

Mashindano yote hayo ni lazima Tanzania ishiriki vyema na kushinda hivyo, ni wakati wa kusahau yote yaliyotokea London, Uingereza na kuanza kujipanga upya kwa mashindano hayo yajayo ili kuhakikisha hatuanguki tena kwa sababu kufanya kosa sio kosa.

Tunaamini wanariadha na wanamichezo wengine wa Tanzania wana uwezo wa kufanya vizuri kama watafanya maandalizi ya mapema na yenye uhakika, kama ambavyo Simbu na wenzake wamekuwa wakifanya kabla ya kwenda London.

Kitu muhimu ni wasimamizi wa michezo na hasa hiyo itakayoshirikishwa kwenye mashindano hayo kutengeneza mipango kazi ya kuandaa wanamichezo ambao, wataibeba bendera ya Tanzania na kuiletea sifa nchi.

Ndivyo ambavyo mataifa mengine yamekuwa yakijipanga kabla ya kutuma watu wao kuwawakilisha na mafanikio yamekuwa yakionekana.

Hatuwezi kusubiri muda wa kufanyika mashindano ukifika ndipo tukurupuke kuanza kukimbizana kusaka washiriki ama wadhamini wa kutusaidia wakati wa mashindano. Ndiyo maana tunasema yaliyotokea London, yamepita na tumevuna tulichopanda na sasa ni zamu ya kujiandaa upya ili tuongeze idadi ya medali katika mashindano makubwa duniani.

Tukianza kufanya maandalizi kamambe kuanzia sasa, hakika hatutakuwa na la zaidi bali wanamichezo wetu watarejea nyumbani na medali za kutosha na dunia itaanza kuitambua Tanzania kuwa sio kisiwa cha amani tu, bali wakali wa kuwanyoosha ndani ya uwanja. Tukiamua kila kitu kinawezekana hivyo, tuanze sasa.