Tumeona Simba Day kwa miaka 10, kuna kitu gani kipya!

Tuesday August 8 2017

 

NI zaidi ya miaka10 tangu Simba ianzishe siku yao ambayo huitwa ‘Simba Day’ na huwa inafanyika kila mwaka wakati wa sherehe za Nane Nane.

Lilikuwa wazo zuri, aliyeanzisha alifikiria jambo zuri, lakini sijui kama alichokifikiria wakati huo ndicho hiki kinachofanyika sasa.

Huwa ni siku nzuri, kwa maana wachezaji karibu wote wa Simba huwa wanatambulishwa uwanjani, jezi mpya zitakazotumika huwa zinatambulishwa na hatimaye huwa inachezwa mechi kati ya timu hiyo ya Msimbazi na timu nyingine mara nyingi huwa kutoka nje ya nchi.

Huwa ni siku muhimu kwa Simba na mashabiki wake kwa sababu, huleta picha ya kikosi chao cha msimu mpya na ndio maana ni siku muhimu sana hii kwao.

Nimewahi kushauri miaka ya nyuma kuwa klabu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zinapaswa kuiga mfano huo ingawa si lazima iwe katika mfumo huo wa Simba.

Jambo ambalo Simba wanalifanya kwa sasa ni zuri, lakini wanapaswa kuwa wabunifu zaidi ili waachane na mtindo wa kufanya mambo yaleyale kila inapofika Nane Nane.

Jambo ambalo linaumiza ni kuona jezi ambazo zinauzwa siku hiyo uwanjani, zikimilikiwa na watu binafsi na si klabu.

Utashangaa kuna jezi chache za klabu, lakini kutakuwa na jezi nyingi za watu binafsi ambazo zitakuwa zikiuzwa kila kona uwanjani na jambo la kushangaza hakuna mtu atakayekamatwa kwa kuuza jezi hizo.

Ni jambo zuri Simba wanalifanya na hasa kuanzia miaka ya karibuni kwani wamekuwa wakipita maeneo mbalimbali kufanya shughuli za kijamii kama kuwatembelea wagonjwa hospitalini, kwenda kwenye vituo vya watoto na maeneo mbalimbali ya kijamii.

Tumeona kila mwaka baadhi ya fedha ambazo zimekuwa zikipatikana kwenye mechi ya Nane Nane hutolewa kwa ajili ya kusaidia kundi fulani la watu lenye uhitaji na hiyo ndio maana ya mpira wa miguu.

Hayo mambo kwa Simba tumeyaona kwa muda mrefu, sasa tunataka kuona mambo mapya yatakayovutia watu wengi zaidi kuitamani siku hii.

Tunataka kuona mambo mapya zaidi ambayo yataifanya Simba iwe inatengeneza shilingi bilioni moja kwa siku moja tu ya Simba Day.

Soka sasa ni biashara, na ndio maana unapoona usajili wa matrilioni ya fedha wa Neymar kutoka Barcelona kwenda PSG usidhani ni kwa ajili ya uwanjani tu, kuna biashara kubwa.

Je, Simba wanatumiaje nafasi ya kupata fedha kupitia kiungo wao mpya, Haruna Niyonzima? Je fedha walizompa wamepanga kuzirejesha kwa mtindo gani? Je, wamemsajili kwa ajili ya uwanjani tu?

Wanapaswa kuwa na akili hiyo kwa kila mchezaji waliyemsajili. Wafikirie jinsi ya kuzirudisha fedha hizo kibiashara zaidi na tena si kurudisha tu fedha hizo, ila wafanye hivyo ikiwa ni pamoja na kutengeneza faida juu.

Kwa hiyo unapokuwa na siku kama hii ya Simba Day, klabu hiyo inapaswa kufikiria kibiashara zaidi badala ya kufikiria mchezo dhidi ya Rayon Sports.

Wakianza kufikiria kibiashara zaidi na kuwa na mfumo mzuri wa uendeshaji wa fedha, itachukua miaka michache kuifanya klabu hiyo kuwa na mafanikio makubwa.