HISIA ZANGU: Tshabalala, Haji Mwinyi wana kesi ya msingi ya kujibu

Tuesday February 13 2018

 MCL

By Edo Kumwembe

SITAANDIKA kuhusu ushindi wa Simba dhidi ya Gendarmarie. Sio habari ya mjini. Jana niliandika kuhusu Yanga ilivyochemsha kwa Washelisheli. Ile ilikuwa habari ya mjini. Unamfungaje Saint Louis bao 1-0? Tumeshuka kisoka au wao wamepanda kisoka?

Kwa Simba ilichokifanya kilichotarajiwa. Mechi mbili zijazo naamini Simba na Yanga zitamalizia kwa ushindi, halafu zitaanza rasmi michuano kwa kucheza soka la ukweli katika hatua inayofuata. Kwa sasa zipo katika fungate tu.

Acha na hao, sasa tujifunze kuhusu mpira. Pale ninapomtazama Mchezaji Bora wa msimu uliopita, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ analikalia benchi Simba. Nafasi yake kwa sasa inachezwa na Asante Kwasi kutoka Ghana. Maisha yanaenda kasi sana.

Tujifunze kuhusu mpira wa kisasa. Pale unapomuona Haji Mwinyi anakali benchi Yanga na nafasi yake inachezwa na Gadiel Michael. Na Gadiel anacheza vizuri kwelikweli. Shuti lake dhidi ya Azam lilisisimua sana. Maisha yanaenda kasi sana.

Wote walikuwa na uhakika wa namba zao msimu uliopita, msimu huu hawana uhakika wa nafasi zao. Msimu uliopita tulikuwa tunajiuliza nani alikuwa anastahili kuanza katika kikosi cha timu ya taifa baina yao, msimu huu hawana uhakika na nafasi zao.

Tshabalala hajarudi kuwa yule tunayemfahamu tangu alipoumia msimu uliopita. Wakati mwingine ni tatizo la kisaikolojia zaidi na kujihofia. Inatokea kwa wachezaji ambao wanapata majeraha yao makubwa ya kwanza katika soka.

Hata hivyo, kwa chochote ambacho kinawatokea Tshabalala na Mwinyi, ukweli ni kwamba wanapitia katika kipindi ambacho Jonas Mkude alipitia katika miezi ya karibuni katika utawala wa kocha aliyepita, Joseph Omog.

Unachopaswa kufanya katika nyakati hizo ni kuwa mchezaji hasa wa kulipwa. Unapaswa kupambana na kuipigania nafasi yako. Unaipigania mazoezini na katika dakika chache unazopewa. Hii ndio maana halisi ya mchezaji wa kulipwa kwa sababu mwisho wa siku soka ni maisha yako.

Wanasoka wetu wengi hakuna wanachoweza kufanya nje ya soka. Soka ni maisha yao, lakini bado tunaishia kuwabembeleza kufanya kazi yao. Kila mtu afanye kazi yake kuhakikisha haichukuliwi na mtu mwingine. Ndio maana Ulaya wachezaji hawakai kambini.

Nilikuwa natembea na Mbwana Samatta katika mitaa ya Genk siku moja kabla hawajacheza mechi yao ngumu ya Ligi Kuu ya Ubelgiji, Oastende Machi mwaka juzi. Tulikuwa tunajadili suala hili hili la wachezaji kutokaa kambini.

Unapoipambania nafasi yako hauhitaji kuambiwa muda wa kulala au kula. Hauhitaji kubembelezwa. Hiki ndicho ambacho unaweza kuona kinapaswa kutokea kwa Tshabalala na Mwinyi wakati watakapokuwa wanawania kuzirudisha nafasi zao.

Tatizo kubwa ambalo tunalo katika mpira wetu ni wachezaji hawashindani kuanzia katika ndani ya timu zao. Na baadaye wachezaji hawashindani nje ya timu zao pindi wanapocheza mechi za michuano mbalimbali.

Wachezaji wengi wanakuwa na uhakika na nafasi zao. Hawana hofu sana. Ni sawa na kusema kuwa wachezaji wengi wanakuwa na uhakika na maisha yao. Katika hali halisi maisha hayapaswi kuwa hivi. Maisha yanahitaji kugombaniwa.

Tshabalala na Mwinyi wanapaswa kurudisha nafasi zao kwa kuzipigania. Nilikuwa nawashangaaa watu waliokuwa wanalalamika kwanini Omog alikuwa hampangi Mkude. Ukweli ni kwamba James Kotei alikuwa anacheza vizuri na timu ilikuwa inashinda.

Wazungu wanasema hauwezi kubadilisha kikosi kinachoshinda. Kwa sasa Mkude amerudi na amejifunza adabu maisha yanaweza kubadilika wakati wowote ule bila ya matarajio. Ukijifunza hilo unakuwa mwanasoka halisi wa kulipwa.

Napenda kuona Tshabalala na Mwinyi wamepata changamoto katika nafasi zao. Inaleta ushindani ndani ya timu na baadaye changamoto hii inakuwa na afya kwa maendeleo ya soka na kwa timu ya taifa.

Pale Yanga anacheza Hassan Kessy badala ya Juma Abdul ambaye yupo majeruhi. Kama Juma Abdul haumii kuona Kessy anafanya vizuri katika nafasi yake basi Juma Abdul hawezi kuwa mchezaji wa kulipwa kamwe katika maisha yake.

Inabidi aumie na kuharakisha kurudi uwanjani kwa sababu nafasi yake ipo hatarini. Kama nafasi yake ipo hatarini ina maana maisha yake yapo hatarini. Sizioni kazi nyingine ambazo Juma Abdul anaweza kufanya nje ya soka. Na wala sioni kama anaweza kuridhika kwenda kuchukua mshahara wa Kagera Sugar kama akitemwa Yanga.