Timu zimeomba kuumia Ligi Kuu

LIGI Kuu Bara inatarajia kuanza Agosti 22 tu hapo pale nyasi za viwanja mbalimbali zitakapoanza kuwaka moto. Ni ligi ya timu 20, tofauti na msimu uliopita ambapo ilikuwa na timu 16 na msimu wa mwaka juzi zilikuwa na timu 14.

Katika maandalizi ya ligi, kwa kawaida timu huanza na usajili wa kuimarisha vikosi na kurekebisha safu mbalimbali ambazo msimu uliotangulia zilionekana kuwa na shida.

Usajili wa msimu huu ulitikisa zaidi kwa timu chache hasa Simba, Azam ambao wameonekana kuwa na pesa ya uhakika. Timu nyingine usajili wao umekuwa wa kawaida sana, haukuwa wa kutikisa kama msimu uliopita ambapo hata timu zilizopanda daraja zilisumbua kwenye usajili zikiwamo Singida United na Lipuli FC.

Lakini sasa timu kama Mbeya City iliyokuwa na mashabiki wengi hakuna usajili wa maana iliyoufanya, yote haya ni kutokana na timu nyingi kukabiliwa na ukata.

Timu nyingi hazina fedha, maisha yamekuwa ya kuungaunga tu, hazina wadhamini kwani chanzo chao kikuu cha mapato ni fedha za getini wakati wa mechi, lakini hivi sasa klabu zimebadilisha mfumo huo wa mgawanyo wa mapato.

Awali utaratibu kwenye mapato ulikuwa timu mwenyeji kupata asilimia 60 huku mgeni akichukuwa asilimia 40, lakini hivi sasa mambo yamebadilika.

Msimu mpya unaokaribia kuanza una mabadiliko kwenye mgawanyo wa mapato siku ya mechi, mabadiliko haya yamepitishwa na viongozi wa klabu wenyewe ambao hupiga kura chini ya kitengo kinachosimamia uendeshaji wa ligi nchini ambacho ni Bodi ya Ligi.

Bodi ya ligi haikuamua yenyewe juu ya kupitisha mgawanyo huu wa timu mwenyeji ndiye anayestahili kuchukua mapato yote siku ya mechi na mgeni haambulii kitu, bali klabu wenyewe huenda walitafakari na kubaini itakuwa sahihi.

Lakini kimahesabu hii itawaumiza wengi wanaoshiriki ligi hasa klabu ambazo hazina mashabiki na uwazi ni kwamba timu za mikoani ndizo zitaumia zaidi kimahesabu kwani mechi pekee ambayo zinaweza kupata pesa nyingi ni pale zitakapocheza dhidi ya Simba au Yanga na si vinginevyo.

Faida itakayopata ni mechi moja tu ya nyumbani, lakini itakaposafiri hadi Dar es Salaam kukutana na timu hizo kongwe zenye mashabiki wengi wataambulia patupu kwani hawatapata mgawo wowote katika mechi zitakazochezwa Uwanja wa Taifa au hata Uhuru.

Hili ni pigo kwao kwani watakuwa na maumivu makali zaidi kusafiri umbali mrefu bila kupata chochote huku hata maandalizi yao wanayafanya kwa shida, baadhi hata usajili wa maana wameshindwa kuufanya na mbaya zaidi hata mapato wataingiza kidogo sana kwa msimu mzima.

Gharama waliyotumia kujiandaa na kile watakachoingia kwa msimu hakitalingana hata kidogo japokuwa hata msimu uliopita mapato hayakuwa kwa kiwango kikubwa. Leo hii Simba ambayo imesheheni. Kikosi kipo imara kwa kukiangalia, mashabiki wao wana mzuka mkubwa wanataka kushuhudia kila mechi yao kwa kufika uwanjani, Simba ina uwezo wa kujaza mashabiki Uwanja wa Taifa na kupata pesa nyingi, lakini pesa hiyo itakuwa inawahusu wao tu timu ngeni haitahusika nazo.