Timu zifanye usajili wa kuleta tija kwenye timu dirisha dogo

Muktasari:

  • Ni usajili wa timu za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na la pili (SDL), ikiwa ni nafasi ya kufanyia marekebisho maeneo yenye upungufu kwenye timu zao.

ZIMEPITA siku mbili sasa tangu dirisha dogo la usajili lilipofunguliwa Novemba 15 na litadumu kwa mwezi mmoja hadi katikati mwa mezi ujao.

Ni usajili wa timu za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na la pili (SDL), ikiwa ni nafasi ya kufanyia marekebisho maeneo yenye upungufu kwenye timu zao.

Usajili huu uliwekwa mahususi kusaidia timu kuondoa dosari ambazo hazikuweza kuondoka moja kwa moja katika usajili wa dirisha kubwa.

Wakati huu wachezaji ambao hawana nafasi za kucheza katika timu zao, huomba pia kutolewa kwa mkopo kwenda timu nyingine ili kuokoa viwango vyao ambavyo kimsingi ndiyo vinatengeneza ugali wa familia zao.

Ni usajili mdogo lakini wenye tija kubwa kwa timu kama utafanyika kwa kuzingatia weledi na mapungufu ya timu.

Benchi la ufundi la kila timu linatakiwa kutoa ripoti ya mapungufu waliyoyaona katika vikosi vyao, ili mabosi wao waweze kurekebisha kwa kuwaleta wachezaji wanaowahitaji.

Kwa kifupi, dirisha dogo siyo wakati wa kufanya usajili wa wachezaji wengi kama timu zinavyofanya kwenye dirisha kubwa.

Haikatazwi kufanya hivyo, lakini kiufundi siyo jambo zuri kwani wachezaji hawapati fursa ya kukaa pamoja na kuzoeana kwa kuwa hakuna maandalizi makubwa kama yale ya mwanzo wa msimu.

Mwaka jana, Mbeya City ilifanya usajili wa wachezaji 11 katika dirisha dogo lakini wengi walishindwa kufanya vizuri kwani kocha hakupata muda wa kuwaandaa vya kutosha.

Hili lilisababisha kundi kubwa la wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo kukatwa mwishoni mwa msimu, na kuitia hasara timu hiyo ya Mbeya.

Timu zinatakiwa kutazama upungufu wa aina mbili ama tatu tu na kuyarekebisha kwa kutafuta wachezaji sahihi katika nafasi hizo.

Azam FC nayo iliingia mkenge kwenye usajili wa dirisha dogo lililopita kwani ilifanya usajili wa wachezaji watano kutoka Ghana lakini ni mmoja tu aliyejihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza huku wengine wakiwa wameachwa kabisa.

Azam iliwasajili Yakubu Mohammed, Yahya Mohammed, Samuel Afful na Stephane Kingue huku usajili mwingine wa Enock Atta Agyei ukikamilika msimu huu.

Katika usajili huo ni Yakubu pekee alifiti mara moja huku Kingue naye akionekana kuwa mchezaji muhimu lakini hali ikawa mbaya kwa Yahya na Afful ambao tayari wameachwa.

Ni wazi kwamba usajili wa dirisha dogo ni mgumu, na unapaswa kulenga mahitaji muhimu na ndiyo sababu tunaendelea kuzikumbusha timu za Ligi Kuu pamoja na madaraja ya chini kuangalia mapungufu machache tu.

Kwa timu za Ligi Daraja la Kwanza, zimebakisha michezo mitano tu kabla ya kukamilisha ligi hiyo hivyo nazo hazina ulazima wa kufanya vurugu kubwa sokoni.

Kama timu ya FDL imeshindwa kuwa katika njia ya kupanda mpaka sasa, hakuna maajabu itaweza kufanya kwa kusajili wachezaji wengi kwenye dirisha dogo.

Timu ambazo zimeonyesha mwanga ndizo zinapaswa kuimarisha maeneo machache, ili kupanda.

Kama timu ina upungufu kwenye ulinzi, iimarishe eneo hilo pekee na siyo kujikita katika usajili mkubwa ambao utawapa hasara.

Tunapenda pia kuzikumbusha timu kubwa siyo lazima kufanya usajili kila dirisha linapofunguliwa, kwani zipo timu ambazo zimetimia kila idara na mapungufu yao yanaweza kurekebishwa ndani kwa ndani.

Siyo vizuri kuwa na lundo la wachezaji wengi kama kocha mwenyewe hawezi kuwatumia vizuri.

Makocha wengine wamekuwa wavivu wa kufundisha na kupenda wachezaji waliokamilika, hivyo kuzitia timu hasara kwa kutaka kusajili kila dirisha linapofunguliwa.

Makocha wana wajibu wa kuwaelekeza wachezaji waliopo ili wafanye vizuri na siyo kupapatikia dirisha la usajili na kuzigharimu timu zao fedha nyingi.

Tunapenda kuchukua nafasi hii kuzikumbusha pia timu zikamilisha sajili zao kwa wakati, na siyo kusubiri hadi siku ya mwisho ndipo zianze kukimbizana na upepo. Ni aibu kwa timu kushindwa kukamilisha usajili wake kwa wakati na kujikuta ikipigwa faini za kizembe.