Timu za Ligi Kuu zikumbuke programu za vijana

Friday June 30 2017

 

KATIKA soka la nchini, usajili bado unaendelea na timu mbalimbali hasa zile za Ligi Kuu Bara zinaimarisha vikosi vyao kabla ya kuanza msimu mpya wa mashindano hayo baadaye Agosti.

Timu hizo zinaongeza wachezaji wapya huku zikiachana na walioshindwa kufanya vizuri msimu uliopita baada ya kuonyesha viwango vya chini.

Timu kama Majimaji na Stand United, zimefanya mabadiliko makubwa ya vikosi vyao kwa kuwatema karibu wachezaji wote ambao walisababisha mwenendo mbovu wa timu zao ambapo zilikuwa katika hatari ya kushuka daraja.

Kwa timu za Simba na Yanga zimekuwa na vita kubwa ya kuimarisha vikosi vyao kutokana na kwamba zitashiriki mashindano ya kimataifa mwakani.

Kila moja inajitahidi kupata wachezaji wazuri ili waweze kuwa na ushiriki mzuri kulingana na kiwango cha ushindani wa kimataifa cha mashindano hayo.

Wakati huu ambapo usajili unaendelea, tunapenda kuzikumbusha timu zetu kuwa zisisahau kuimarisha timu zao za vijana pia, kwani ndipo msingi wa soka ulipo na faida kwa baadaye..

Timu nyingi zinatazama zaidi namna ya kuimarisha timu kubwa na kusahau zile za vijana ambazo zipo kikanuni.

Tumeona mpaka sasa ni timu ya Azam tu ambayo imeonyesha nia ya kutoa kipaumbele kwa timu za vijana hasa kwa kuwapandisha vijana wengi kwenda katika timu yao ya wakubwa.

Azam imeamua kufanya hivyo kutokana na mpango wake wa kutoa fursa zaidi kwa vijana kutoka katika akademi yao. Mpango huo unaanza rasmi msimu ujao na huenda ukawa na msaada mkubwa kwa timu ya taifa, Taifa Stars, pia.

Ifahamike kwamba Azam tayari imefanya maboresho makubwa katika timu zake za vijana kwa kutembea nchi nzima na kuwafanyia vijana majaribio ili kuona wenye vipaji halisi na ambao wanaweza kuwasaidia.

Maboresho hayo yamesaidia upatikanaji wa vijana wengi ambao sasa wanaunda timu zao za vijana.

Hapana shaka kwamba Azam imetumia vizuri miundombinu yake ya Chamazi kufanya uwekezaji huo wa soka la vijana jambo linalopaswa kufanywa pia na timu nyingine.

Kwa upande wa timu za Simba na Yanga, mpaka sasa hatujaona makeke yoyote kwenye soka la vijana zaidi ya kufanya usajili wa wachezaji wenye majina makubwa. Ni kama zimesahau kwamba uwekezaji wa vijana ni muhimu kwao.

Ni wazi kanuni za Ligi Kuu zinaitaka kila timu kutoa nafasi tano kwa wachezaji kutoka timu za vijana, lakini bado kuna mwamko mdogo hasa juu ya kuwekeza kwenye soka hilo.

Bado timu za Ligi Kuu hazijaweka kipaumbele cha kutosha kwa soka la vijana na ndiyo sababu ambayo inazifanya kuhaha huku na kule kusaka wachezaji wa kuwasaidia msimu ujao.

Timu kama Mbao, msimu uliopita ilifanya juhudi kubwa ya kutengeneza kikosi chenye mchanyato wa vijana pamoja na wachezaji wachache wenye uzoefu jambo ambalo liliwasaidia kufanya vizuri.

Tuliona namna wachezaji wa Mbao walivyokuwa makini katika kazi yao hasa kwenye michuano ya Kombe la FA ambapo walifika hadi hatua ya fainali kabla ya kufungwa na Simba iliyoibuka washindi.

Kwa sasa timu kubwa za Simba, Yanga na Azam zimekuwa zikipigana vikumbo kuwania wachezaji wa Mbao ambao mwaka jana hawakuwa hata wakifahamika.

Ni matarajio yetu kwamba msimu huu Locha wa Mbao FC, Etienne Ndayiragije, atafanya juhudi za kuwapa nafasi vijana wengine wengi zaidi kutoka katika timu yao ya vijana.

Tumeona timu kama Mtibwa Sugar nayo inafanya juhudi za kusajili wachezaji vijana ili kujiimarisha kama ilivyokuwa ikifanya katika misimu ya nyuma.

Mtibwa imekuwa na msingi mzuri wa soka la vijana na inawakuza na baadaye kuwauza kwenda katika klabu nyingine.

Kama siyo juhudi za Mtibwa wachezaji kama Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin na wengineo wanaotamba Taifa Stars sasa wasingekuwa wameonekana na kufikia walipo.

Tuendelee kutoa wito kwa timu nyingine kutoa pia nafasi kwa wachezaji vijana hasa katika mechi ambazo hazina ushindani mkubwa ili kuwasaidia kukua na kuendelea.

Mfano timu ya Simba kwa miaka ya nyuma ilitoa nafasi kwa wachezaji kama Jonas Mkude, Ramadhani Singano, Said Ndemla, Ibrahim Ajibu na wengineo ambao wamekuwa mastaa wakubwa sasa.

Timu za Ligi Kuu zikumbuke kuwa baadaye mwaka huu kutakuwa pia na Ligi ya Vijana hivyo ipo haja ya kuziimarisha timu zao kwa ajili ya kuongeza ushindani katika mashindano hayo.