MAONI: Tatizo la nidhamu katika VPL, litafutiwe ufumbuzi mapema

Saturday January 6 2018

LIGI Kuu Bara kwa sasa ipo mapumziko kwa muda kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar.

Mpaka ikienda mapumziko, Simba ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na alama 26 sawa na ilizonazo Azam ila wanatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa, huku Singida United na Yanga zikifuata nyuma yao.

Ligi ikiwa imesimama, kuna baadhi ya matukio ambayo yamekuwa yakijiri tangu ligi hiyo ilipoanza Agosti mwaka jana ikiwamo vitendo vya utovu wa nidhamu ambao umekuwa ukizigharimu timu pamoja na wachezaji, makocha na viongozi wa klabu.

Kwa muda mrefu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kamati zake mbalimbali zikiwamo za nidhamu na Saa 72 zimekuwa zikitoa adhabu kwa klabu, makocha na wachezaji kutokana na makosa yaliyofanyika katika miezi mitano iliyopita.

Jana tu, kamati hizo za TFF zimetoka kuziadhibu Mbao FC na kocha wao, Etienne Ndayiragije na wachezaji kadhaa wa timu mbalimbali akiwamo Obery Chirwa wa Yanga na Lambert Sabyanka wa Prisons kwa kuwasimamisha ama kuwatwanga faini kwa makosa waliyofanya.

Hii ni kuonyesha kuna tatizo la utovu wa nidhamu katika Ligi Kuu, hivyo ni lazima wakati ligi hiyo ikirejea kwa ajili ya raundi tatu za duru la kwanza na nyingine 15 za duru la pili, iwe na mabadiliko ili timu na wachezaji wacheze kwa nidhamu.

Nidhamu ni msingi wa maendeleo ya kila jambo, hata katika maisha ya kawaida mtu asiyekuwa na nidhamu ya jambo lolote hata matumizi ya fedha anazozitafuta kwa jasho ni vigumu kwake kufanikiwa.

Hata wachezaji wa soka kucheza bila ya nidhamu ni jambo linalowakwanza kufika mbali.

Klabu zenye nidhamu mbovu ni vigumu kufikia mafanikio makubwa inayoyaota kwa sababu itaangushwa tu na tatizo hilo katika ushiriki wa michuano yao iwe ya kitaifa ama kimataifa.

Ndio maana kama wadau wa soka, tungependa kuzikumbusha klabu za Ligi Kuu pamoja na wachezaji wote, makocha na hata viongozi wake kuwa ni vyema kujikita katika nidhamu, ili waweze kufika mbali na kusaidia kuinua soka letu.

Inawezekana TFF inashindwa kukemea suala hili kwa vile yenyewe inanufaika kwa faini inazozipiga timu, wachezaji, makocha na viongozi na kutunisha mifuko ya shirikisho hilo, lakini nidhamu mbovu ina athari kubwa kwa soka letu.

Hata kama suala la nidhamu nzuri ama mbovu ni suala linalomhusu mtu mmoja, lakini viongozi na makocha wanawajibu mkubwa wa kuwasaidia wachezaji wao kwa kuwaonya mapema na kuwataka kuingia viwanjani wakiwa na utulivu wa akili.

Kama kocha wa timu hana nidhamu wala kuwa na uwezo wa kuhimili presha za uwanjani na kufanya matendo ya ovyo na utovu wa nidhamu, ni vipi ataweza kuwahimili wachezaji wake. Kiongozi asiyeweza kuhimili vishindo vya uwanjani atawezaje kuanza kuwatuliza wachezaji wake pale wanapokuwa na munkari?

Viongozi, makocha na wachezaji wanapokuwa na mihemko na kushindwa kuhimili presha za uwanjani ni hatari kwa maendeleo ya timu kwa sababu ni rahisi kuingia matatani kwa kosa na utovu wa nidhamu wa kila mara.

Achana na visingizio waamuzi wamekuwa wakichezesha mechi vibaya kwa kukiuka sheria 17 na kusababisha wachezaji, makocha na viongozi wa klabu kupata mihemko na kufanya mambo yanayowasababishioa kuwa na matatani, lakini baadhi yao wahusika ni hulka zao kutokuwa na nidhamu nzuri.

Kwa kuhofia vipaji vya soka vilivyopo katika timu za ligi kuu, tungependa wahusika kujiangalia mapema kwa nia ya kujietengenezea mazingira mazuri hata ya kujiuza nje ya nchi kwa kucheza soka la kulipwa kama ilivyokuwa kwa Mbwana Samatta na sasa Simon Msuva anayecheza nchini Morocco katika klabu ya Difaa el Jadida, ambaye baada ya kufanya kosa la utovu wa nidhamu aliomba radhi.

Kila mara tumekuwa tukitolea mfano nidhamu njema ndio maana tunasisitiza wachezaji wetu wajikite kwenye nidhamu bora na kucheza soka kwa kuifikiria kesho yao, kitu ambacho pia kinafaa kuzingatiwa na makocha na viongozi wa klabu ili kufanya hata mashabiki wakorofi wakose pa kutokea.