MAONI YA MHARIRI: Tangulia Joel Bendera, kwa hakika tutakukumbuka milele

Friday December 8 2017

 

DURU za kispoti jioni ya juzi zilishtushwa na baadhi kushindwa kuamini mapema kufuatia taarifa za kifo cha ghafla cha Kocha wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars, Dk Joel Nkaya Bendera.

Hata sisi Mwanaspoti haikuwa rahisi kuamini taarifa zilizokuwa zikizagaa kwenye mitandao ya kijamii na hasa kutokana na ukweli mitandao hiyo kwa sasa  imekuwa ikitumiwa vibaya na baadhi ya watu kwa kuwazushia wengine.

Hata hivyo, uthibitisho kutoka kwa Msemaji wa Hospitali Kuu ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha kuwa, mwanamichezo huyo wa zamani ni kweli ameaga dunia  kwenye hospitali hiyo baada ya kupokewa kutoka Bagamoyo ulitufanya tuamini.

Na tuliamini kwa kutambua kuwa kila nafsi ni lazima ionje mauti na mwisho kumshukuru Mungu kwa mapenzi yake kwani tulimpenda Joel Bendera, lakini Muumba alimpenda zaidi na kuamua kumuita katika wito kwa kila kiumbe hai.

Kwa hakika msiba huu ni mzito kwa familia, ndugu, jamaa na rafiki wa marehemu Bendera na ni pigo kubwa kwa wanafamilia ya michezo hususani soka kutokana  na rekodi ya kipekee aliyokuwa ameiweka gwiji huyo enzi za uhai wake.

Bendera anakumbukwa kwa kuiwezesha Tanzania kushiriki kwa mara ya kwanza na mwisho katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 1980 akiwa miongoni mwa makocha wasaidizi wa Mpoland, Slawomir Wolk.

Koch  a mwingine mzawa aliyeweka rekodi hiyo sambamba na Bendera ni Ray Gama ambaye naye kwa sasa ni marehemu.

Sio rekodi hiyo tu, lakini enzi za uhai wake Marehemu Bendera licha ya kuwa mnazi mkubwa wa klabu ya Yanga, Mwaka 1979 aliiongoza Simba kuweka rekodi nyingine Afrika kwa kuing’oa Mufulira Wanderers kwa jumla ya mabao 5-4.

Kwa wale waliosahau pambano hilo lililobaki katika historia ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Dunia kwa ujumla ngazi za klabu ni kitendo cha vijana wa Bendera kulala nyumbani mabao 4-0.

Kila mmoja aliamini kuwa safari ya Simba ilikuwa imetimia, lakini Kocha Bendera alikwenda Zambia na vijana wake na kuwashangaza Wazambia na Rais wao enzi hizo, Kenneth Kaunda kwa kupata ushindi wa mabao 5-0.

Ushindi huo wa ugenini na kuwang’oa wenyeji haijawahi kutokea, lakini Bendera kwa kipawa chake cha ukocha alifanikisha akishirikiana na wanasimba na kuitupa nje Mufulira bila ya Wazambia kuamini.

Marehemu Bendera atakumbukwa na wanamichezo kwa ujumla kutokana na kupenda kwake michezo kwa dhati na kutoa mchango mkubwa katika sekta hiyo na hasa soka.

Hata alipokuwa akitumikia nafasi zake za kisiasa hakuficha mahaba yake ya soka na Agosti mwaka 2009 aliweka rekodi nyingine ya kuwa waziri wa kwanza wa  michezo nchini kufanya ziara katika klabu za Simba na Yanga.

Rekodi yake ya kuwa mmoja wa makocha walioipeleka Tanzania katika fainali za Afrika imedumu kwa miaka 37 ikiwasumbua makocha wengi wa wazawa na wa kigeni walifuata baadaye Stars kupambana kuipeleka tena timu hiyo Afcon.

Mwanaspoti kama wadau wakubwa wa michezo, tunaungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Bendera katika msiba huu mzito na tunawaombea kwa Mola kuwapa nguvu na subira katika kipindi hiki cha simanzi.

Kwa wanamichezo hususani wanasoka ni wajibu wao kumuenzi kwa vitendo kocha huyo wa zamani maarufu na mwanasiasa, kuendeleza kila zuri ambalo alilisisitiza na kulifanya katika kuona mchezo huo unasonga mbele. Njia za kumuenzi ni nyingi kwa wachezaji ni kupambana ndani ya klabu wawakilishi na hata timu ya taifa, kuhakikisha timu zetu zinafanya vema kimataifa kama ambavyo marehemu Bendera alipambana kuzipa mafanikio timu alizofundisha.

Viongozi nao wana njia yao ya kumuenzi kwa kutengeneza mipango mkakati ya kuleta mafanikio katika soka na michezo kwa ujumla kama ambavyo Bendera aalipigania.

Ni aibu kwa miaka karibu 40 Tanzania imeshindwa kushiriki fainali za Afrika, ni aibu klabu za Tanzania kunyakua taji lolote la michuano ya Afrika. Hivyo kama njia ya kumuenzi   ni kuweka timu zetu kwenye rekodi kwa kufanya vizuri.