Tajiri Manji alivyoiacha Yanga vipande vipande

Muktasari:

  • Yanga ilikuwa inaweka kambi Uturuki, Simba ilikuwa inahaha na kitu kinachoitwa umaskini.
  • Tofauti ni kwamba Simba inajua kuishi na umaskini nje ya uwanja.
  • Yanga haijui kuishi na umaskini.

JINSI maisha yanavyoweza kwenda kasi. Simba leo ndio inaenda kuweka kambi Uturuki. Yanga iko hoi. Wachezaji wanagoma. Hawana mikataba, hawana mishahara, hawana posho. Hawana chochote. Maisha yapo kasi sana.

Miezi kadhaa iliyopita hali ilikuwa tofauti. Yanga ilikuwa inaweka kambi Uturuki, Simba ilikuwa inahaha na kitu kinachoitwa umaskini. Tofauti ni kwamba Simba inajua kuishi na umaskini nje ya uwanja. Yanga haijui kuishi na umaskini.

Kitu kikubwa cha msingi ni kwamba tajiri Yusuph Manji alitanua lango. Mishahara ya wachezaji ilikwenda juu, manunuzi yao sokoni yalikwenda juu. Ghafla Yanga ikawa timu ghali katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Likizo ilikuwa inakwenda zake Uturuki. Kwa sasa akaunti ya klabu haina ubavu wa kumudu maisha haya.

Kuna viongozi walikuwa wana maneno mengi huku wakionekana kama vile ni mahodari katika kuongoza timu lakini kumbe walikuwa wamejificha katika uwezo wa kipesa wa tajiri. Leo hawapokei simu na wengine wamebadili namba zao.

Kosa la kwanza la kiufundi ni kutegemea pesa za mtu mmoja. Tajiri na mwenyekiti wa timu. walijisahau na walikuwa wanaleta dharau hata kwa pesa nyingine za watu mbalimbali. Fikiria jinsi walivyokuwa wanaziletea dharau pesa za Azam TV.

Kosa la pili la kiufundi ni hili la kutokuwepo na mchakato wa uhakika wa namna ya kuiendesha Yanga katika kujitegemea ndani ya utawala au wakati atakapoondoka. Hili kosa linanishangaza sana. Kwanza ni kwa sababu hata mabadiliko yangefanyika ni yeye ndiye ambaye angeichukua timu.

Katika hali nzuri ya kawaida, kama hili la pili lingefanyika ina maana kwa sasa rais ambaye amepata matatizo angeuza timu kwenda kwa mtu mwingine. Kabla ya hapo tayari timu ingekuwa imeongezeka thamani.

Lakini baada ya bosi kuondoka bado wanachama na uongozi wao wameendelea kufanya kosa la kiufundi. Hawakufungua mchakato wa kuiendesha klabu katika njia za kisasa bila ya kumlenga mtu mmoja. Michakato ya kubadili mienendo ya Simba na Yanga iliwalenga watu walioonyesha nia tu. Haikulenga katika ushindani wa soko uria kwa yeyote ambaye ana pesa zake na anataka kuwekeza katika mpira.

Mpaka leo Yanga inaamini katika tajiri zaidi yao zaidi na haitaki kusikia lolote. Jana Jumapili wanachama walipanga kukutana klabuni kwao wakiwa na lengo na kujadili mustakabali wao. Hauhitaji kuwa na upeo mkubwa kubashiri kwamba mwisho wa siku wangerudi katika ajenda moja tu ya kumrudisha tajiri.

Hapa Yanga walipaswa kupigana vita mbili. Kwanza ni kumrudisha tajiri, sawa, lakini pili ni kuiweka Yanga kama Yanga sokoni na kujaribu kujua nia ya kampuni nyingine ambazo zinaweza kutaka kufanya uwekezaji mkubwa katika Yanga.

Mchakato huu wa pili wanauzungumza kichinichini lakini bado lengo linabakia kuwa lile lile tu la kumpa timu tajiri. Kwanini wasiupeleke mchakato sokoni na kufungua milango wazi kwa kila mtu? Kwanini wasiuharakishe mchakato huu?

Vyovyote ilivyo, Yanga ndani ya matatizo yao au nje ya matatizo yao wanahitaji kuufanya mchakato huu kwa haraka kwa sasa. Ni mchakato wa lazima sio tu kwa sababu ya matatizo yanayowatokea, lakini ndio usasa wenyewe katika soka la kisasa. Klabu nyingine za Ulaya zinaendeshwa hivi.

Yanga wana mtaji mkubwa kuliko hata klabu kadhaa zenye mafanikio dhidi yao. Inachosha kukumbusha silaha ya Yanga ni watu wake. Kwanini katika michakato hii hatuongelei zaidi klabu nyingine kuliko Simba na Yanga ni kwa sababu hatuna uhakika wa mitaji yao.

Yusuph Manji ameaicha Yanga vipande vipande. Ilitabirika muda mrefu. Tatizo kubwa Yanga haiwezi kurudi kuwa chini ilipokuwa kabla ya tajiri huyu. Ndivyo maisha ya kuonja utajiri yalivyo. Inabidi ubakie hapo hapo au uende juu ya hapo.

Baada ya kuwa na wachezaji kama kina Donald Ngoma, Thaban Kamusoko, Obrey Chirwa na wengineo katika ubora wao, watu wa Yanga hawatakubali kuona baadaye timu yao inarudi kwa wachezaji wa kawaida. Hili ndio tatizo la soka.

Simba wana bahati kwamba matanuzi wanayofanya sasa yameenda sambamba na mabadiliko ya katiba waliyoyafanya klabuni kwao. Wanaweza kuhisi wapo salama kwa sababu tajiri hawezi kuiachia timu yao ghafla ghafla.

Na hata kama akiiachia anaweza kufanya hivyo kwa kumuuzia mtu mwingine hisa zake.

Huu ndio mfumo salama ambao unatumiwa na ndugu zetu wa nje. Ni kama ambavyo kwa sasa Roman Abramovich anavyokabiliana na matatizo dhidi ya Serikali ya England na uvumi unazungumzia jinsi ambavyo tajiri anaweza kuiuza timu hiyo na si kuirudisha kwa Wana Chelsea. Ni kawaida katika dunia ya kisasa.

Ni tofauti na ambavyo matatizo ya tajiri wa Mwenyekiti wa Yanga yameiacha Yanga njia panda ikiwa haina tajiri na wala haitegemei kupelekwa kwa tajiri mwingine. Wako maili nyingi nyuma ya mchakato.